Prime
Wengi huoa, kuolewa nje ya machaguo yao

Muktasari:
- Uzoefu unaonyesha watu wengi huingia katika uhusiano wa kindoa kwa vile hawana namna, baadhi wakichelea umri kusonga au kwa presha za ndugu na jamaa.
Zungumza na wanandoa kadhaa uwaulize ikiwa wenza wao walikuwa machaguo ya kwanza maishani au la. Jibu linaweza kukushangaza.
Uzoefu unaonyesha watu wengi huingia katika uhusiano wa kindoa kwa vile hawana namna, baadhi wakichelea umri kusonga au kwa presha za ndugu na jamaa. Hawa hujikuta wakiingia kwenye uhusiano na yeyote yule.
Simulizi ya Abdu Bakari
Mkazi huyu wa jijini Dar es Salaam na mzazi wa watoto watatu, anasema aliamua kufunga ndoa na mwanamke ambaye hakuwa kabisa katika roho yake.
Ilimbidi amuoe baada ya kuunganishiwa na marafiki zake katika kipindi ambacho alikuwa ametoka katika kile anachokiita ‘kupigwa kibuti ‘na msichana aliyekuwa akimpenda kwa dhati.
" Mambo yalikuwa yakienda vizuri na nilishapanga binti huyo aje kuwa mke wangu, lakini ikaja habari ya kusikitisha. Niliambiwa mchumba wangu anaonekana na mwanamume fulani. Kweli siku ya siku nikawafuma, kilichotokea ni binti kuniambia eti sikuwa chaguo lake, yaani sikuwa na sifa ya kumuoa, ‘’ anasema.
Anaeleza kuwa hatua hiyo ilimpa wakati mgumu sana kwani alishajiandaa kuoa. Muda si mrefu anasema akapokea simu ya rafiki yake aliyesoma naye chuo kikuu kuwa lazini kwao kuna binti aende kumtazama ili amuoe.
" Nikaenda kumtazama, kwa kweli hakuwa na vigezo vyangu kama yule wa kwanza, lakini nikajisemea safari hii yeyote aje tu muhimu nioe. Hivyo nilimuoa mwanamke huyo na kuzaa naye watoto wawili.
Kwa kweli hakuwa moyoni, japo niseme kuwa huko baadaye nilianza kuona kama ana vigezo nilivyotaka,’’ anaeleza Bakari na kuongeza kuwa hata hivyo alikaa na mwanamke huyo kwa miaka 10 kisha wakaachana.
Mali kivutio
Wapo wanaovutika kuingia kwenye uhusiano kwa sababu ya mali na mapenzi.
Shinikizo la wazazi
Unajua kuna watu wameoa au kuolewa na wenza waliotafutiwa na wazazi wao?
Wakati baadhi ya watu wakitamani wazazi kujiweka kando na mapenzi ya watoto wao, wapo wanaoamini kuwa mzazi hana haki ya kumchagulia mtoto mwenza anayemuona anafaa.
Athari kuishi na asiye chaguo lako
Mwenyekiti wa taasisi ya ndoa na maadili mkoani Tabora, Shekh Ahmad Kaite anasema miongoni mwa athari kwa ndoa ya namna hiyo, ni kutodumu kwakuwa wenza hao hawatoweza kutekeleza majukumu na haki ya ndoa ikiwamo haki ya tendo la ndoa, kumpatia mke makazi na malazi.
“Athari yake kubwa ndoa haitodumu ndio maana tunasema mtoto wa kiume atakiwi kulazimishwa. Anatakiwa kuwa na hiari na pia mtoto wa kike anatakiwa kuwa na hiari yake. Ili kutekeleza majukumu yake kuna haki za ndoa 10 ambazo mwanaume anatakiwa amtekelezee mkewe na mke amtekelezee mume sasa anapokuwa amelazimisha, atafika kwenye hiyo ndoa na kushindwa kutekeleza hizo haki,”anasema.
Anaongeza: "Kuwa mwadilifu katika kumlisha, kumpatia makazi, kumzika na suala zima la tendo la ndoa, haya ni mambo ya wajibu wa mume kumtendea mke wake na mke wajibu wake mkubwa ni kumtii mumewe na kumpa haki za ndoa wakati wowote pale anapohitaji mume… hatakiwi kubisha, kuguna wala kusema nimechoka."
Ofisa Ustawi jijini Mwanza, Edith Ngowi anasema ndoa za namna hiyo ni miongoni mwa sababu zinazochangia ukatili wa kijinsia kwa wenza na hata watoto, kwani mtu asipokutana na aliyoyatarajia katika ndoa, anaweza kusukumwa kufanya ukatili.
“Tumeona familia zile ambazo mume na mke wameingia kwenye ndoa lakini hawakuridhiana au hawakupendana kwa dhati au wakati mwingine unakuta walikubaliana pasipokujua nini wanakwenda kufanya; hawa ndio wanakuja kuleta shida baadaye kwa maana hawawezi kulea yale matunda ya ndoa yao," anaeleza.
Anaongeza: "Kwasababu wao hawajaridhiana, hawajapendana, hawajakubalina, hivyo wanapopata watoto sasa wanaanza kuwatendea ukatili, mama anakimbia familia au baba anatendewa ukatili kwa kunyimwa tendo la ndoa."
Kwa upande wake, Mzee Amani Said mkazi wa Kwimba mkoani Mwanza, anawataka watu kuwa makini wakati wa kutafuta wenza, hasa wanaochaguliwa na wazazi wao.
“Unakuta mwanaume anatumiwa picha na mama au shangazi yake anayeishi mbali anamwambia kuna binti huku anafaa kuwa mke wako, lakini hujui binti huyo kaambiwa nini hadi kakubali kuolewa na wewe. Unamuoa wiki ya kwanza ya pili unafukuzwa kazi kwa mfano, anaanza visa ikiwemo kukupangia zamu ya kuosha vyombo na kupika. Nawe huna hela, hivyo utapika tu,”anasema.