Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wazazi wanavyoharibu watoto kwa hoja ya adhabu

Muktasari:

  • Je, ni wazazi na walezi wangapi, kwa mfano, tunajua athari za muda mrefu zinazotokana na matumizi ya adhabu katika malezi?

Dar es Salaam. Wazazi wengi hutumia adhabu, wakati mwingine zenye maumivu makali, kama nyenzo ya kurekebisha tabia za watoto. Ingawa lengo huwa ni kupunguza uwezekano wa tabia isiyofaa kuendelea, changamoto kubwa, hata hivyo, ni namna ya kuchora mstari kati ya manufaa ya adhabu yanayoletwa na madhara yake.

Je, ni wazazi na walezi wangapi, kwa mfano, tunajua athari za muda mrefu zinazotokana na matumizi ya adhabu katika malezi?

Pamoja na faida za muda mfupi za kumlazimisha mtoto kufanya kile tunachotaka afanye, ni kwa kiasi gani tunafikiria maumivu ya kimwili na kihisia yanavyoweza kuacha alama zisizofutika?

Katika makala haya, tunachunguza madhara ya adhabu kwa kutumia ushahidi wa kisayansi.


Uchokozi

Umewahi kuwaza kwa nini kuna watoto ni wachokozi wanapokuwa na wenzao? Kwa nini kwa mfano, mtoto anapokuwa na wenzake anakuwa na fujo, uchokozi na ugomvi? Huu ni mfano wa madhara ya mzazi kutumia adhabu kama lugha kuu ya malezi.

Mtoto anayeadhibiwa mara kwa mara anajifunza kuwa matumizi ya nguvu ndio njia ya uhakika ya kutatua matatizo anayokuwa nayo na wenzake.

Mtoto akishaanza kutumia nguvu na kuwa mchokozi anapokuwa na wenzake, ana uwezekano mkubwa wa kuendelea kuwa mchokozi hata anapokuwa mtu mzima.

Mwaka 2016 mshunuzi Elizabeth Gershoff, katika uchambuzi wake wa matokeo ya tafiti zilizokwisha kufanywa (meta analysis), aligundua kuwa watoto wanaochapwa wana uwezekano mkubwa wa kuwa wachokozi ukubwani.

 Gershoff alibaini kuwa adhabu ndiyo inayowafundisha watoto kutatua mizozo yao kwa kutumia jeuri badala ya mazungumzo ya amani. Je, unadhani adhabu ni njia bora ya kumfundisha mtoto tabia njema?


Maumivu ya kihisia

Ukiacha faida zake za muda mfupi, adhabu zinaongeza uwezekano wa kuumiza hisia za mtoto. Hapa hatuzungumzii adhabu zinazosababisha maumivu kwenye mwili tu. Hapana.

Tunazungumzia pia adhabu zinazoumiza hisia mfano kumtenga mtoto, kumkashifu na kumdhalilisha kwa maneno.

Maumivu haya ya kihisia yanaweza kusababisha woga, aibu, na kujistahi kidogo, yakimfanya mtoto ajione dhaifu asiyestahili upendo. Madhara kama haya kihisia yanaweza kuathiri afya yake ya akili kwa miaka mingi.

Elizabeth Gershoff alibaini uhusiano mkubwa kati ya adhabu za kimwili na matatizo ya kihisia kama wasiwasi na unyogovu. Kadhalika, wapo watoto wanaojikuta kwenye mazingira ya kuteseka na majeraha ya kihisia kama matokeo ya adhabu zinazodhalilisha.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Watoto (Unicef), katika ripoti yake ya 2014 “Hidden in Plain Sight,” inabainisiha kuwa watoto wengi wanaoadhabiwa kihisia kukabiliwa na kuzorota kwa maendeleo ya kiakili. Unafikiri tunaweza kupuuza maumivu haya ya kihisia tunapofanya uamuzi wa kumuadhibu mtoto?


Kuzorotesha uhusiano

Fikiria ungekuwa ni wewe muda wote mzazi anakukemea, anakutukana, anakufinya na kukuchapa. Hata kama nia ni kukubadilisha, unadhani unaweza kuwa karibu na mzazi huyo?

Adhabu, pamoja na faida zake kadha, zinaweza kuvunja uaminifu kati ya mtoto na mzazi wake na athari hizi zikaonekana vizuri mtoto atakapojitegemea.

Simulizi za wazazi wengi watu wazima wasio na mawasiliano ya karibu na watoto wao zinaweza kuthibitisha madai haya.

Unicef walionesha kuwa adhabu za kimwili na zile za kihisia zinaathiri vibaya uhusiano wa wazazi na watoto. Kubwa zaidi ni kuzorotesha hali ya mtoto kumuamini mzazi wake. Gershoff niliyerejea utafiti wake hapo awali, aligundua kuwa watoto wanaoadhibiwa wana uwezekano mdogo wa kujisikia salama mikononi mwa wazazi wao. Unaweza kuvumilia kuona mtoto wako anakukimbia badala ya kukukumbatia?


Mzunguko wa ukatili

Ukiacha madhara haya yote, adhabu pia zinaweza kutengeneza mzunguko wa ukatili kutoka kizazi kimoja kwenye kizazi kingine. Mtoto anayeadhibiwa bila staha, anaweza kuamini jeuri ni mambo ya kawaida.

Mtoto huyu anapokuja kuwa mzazi naye atafanya hivyo hivyo akiamini hiyo ndiyo njia sahihi zaidi ya kumrekebisha mtoto.

Tunazo tafiti nyingi zinasema adhabu za kimwili zinahusishwa kwa karibu na tabia za kikatili za watoto baadaye.

Unapokuwa mtu wa kuumizwa na kudhalilishwa, unageuka kuwa mtu mbabe, usiyejisikia hatia kuwa na tabia za ovyo kwa siri unapoamini huwezi kuonekaa. Je, unataka mwanao awe na unafiki huu wa tabia?


Tunachojifunza

Ingawa tumezoea kuadhibu, ukweli wa kitaalam ni kwamba adhabu zinatuweka kwenye hatari ya kuwa watu waoga, wanaoigiza tabia njema lakini tusiweza kuwa watu wa kufanya uamuzi wenye misingi ya utu bila kuogopa macho ya watu hasa mamlaka. Pamoja na faida zake za muda mfupi, tabia ya kuadhibu watoto muda wote inategeneza tatizo kubwa linaloweza kumsumbua mtoto katika maisha yake ya utu uzimani.

 Katika makala ijayo, tutachunguza njia nyingine za kurekebisha tabia bila maumivu.