Hizi hapa sifa za baba bora

Muktasari:
- Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Baba, ni muhimu kutambua nafasi ya baba kwenye maisha ya mtoto.
Dar es Salaam. Wakati dunia ikiadhimisha siku ya baba leo, wito wa wazazi wa kiume kushiriki kikamilifu kwenye malezi ya watoto umetolewa kwa kile kilichoelezwa kuwa baba ana nafasi kubwa katika kumjenga mtoto anayejiamini.
Utafiti uliochapishwa katika tovuti ya Psychology Today unaonyesha kuwa watoto ambao wapo karibu na baba zao wana hali ya kujiamini na wanaona wako salama na kadiri wanavyozidi kuwa wakubwa uhusiano wao na wazazi unazidi kuimarika.
Pamoja na umuhimu huo wakati mwingine kinababa hawasimami kwenye nafasi zao hali inayofanya taratibu thamani yao kupungua na hata kutoweka kabisa na kuacha thamani hiyo itawale upande mmoja.
Kulingana na mshauri wa uhusiano, Deo Sukambi ni muhimu kwa wanaume kutambua kuwa kumsomesha mtoto katika shule nzuri, kumpatia mahitaji yake na zawadi mbalimbali haitoshi kusema umeshiriki kwenye malezi.
Amesema: “Kinanachohitajika ni uwepo wako kama baba, hatima na kesho ya mtoto ipo mikononi mwa baba, hivyo nitoe wito kwamba tunapaswa kujivunia na kusherehekea siku hii kwa kuwa baba ana mchango mkubwa ya kumjenga mtoto kuwa na taswira ya maisha yake ya baadaye na kufanya maamuzi ya msingi.”

Mchungaji na mshauri wa masuala ya familia, Richard Hananja amesema baba bora ni yule anayebeba wajibu wa familia yake na kuitunza kama ambavyo vitabu vya dini vimekuwa vikieleza.
“Baba anatakiwa kujitoa kwa moyo wake kuitunza familia yake hili anapaswa kufanywa bila kulazimishwa tofauti na ilivyo sasa ambapo wengi wamekuwa wakifanya hivyo kwa kulazimishwa. Inashangaza siku hizi unakuta baba anajiondoa kwenye jukumu la kutunza familia yake kisa mama anafanya kazi, hii si sawa baba unapaswa kuonyesha nafasi yako ili hata watoto wajifunze kutoka kwako,”
Sifa nyingine ya baba kulingana na mchungaji huyo ni kutoa majibu ya maswali yanayoikumba familia, kwa kufanya hivyo anajijengea heshima na thamani si tu kwa watoto bali hata mke.
“Sasa usitengeneze mazingira kwamba kila wanachotaka watoto wanakimbilia kwa mama yao na wanakipata ila wewe kila siku huna, hapa utaitengeneza dharau ndiyo tunasikia wanaume wanalalamika kwamba wanawake wanawadharau,”.
Amesema ni muhimu kwa baba kupata muda wa kutosha wa kuwa na watoto ili awajenge katika mfumo unaofaa kinyume na hapo atakutana na watu wengine nje watakaowapandikiza yasiyofaa.
Mchungaji Hananja anaeleza, “Sauti ya baba ni muhimu kwenye familia, wewe kama baba una nafasi ya kumjenga mtoto wako vile unataka, mtengenezee mwelekeo wa maisha. Mtoto kuanzia mwaka 0 hadi 7 ndiyo umri wa kumtengeneza sasa kama huna muda wa kukaa naye ukapandikuza vitu vizuri ndani yake tegemea watu wengine kufanya hivyo,”.
Hilo linaelezwa pia na mtaalam wa malezi wa kituo cha Maadili Senya anayeeleza kuwa nafasi ya baba katika familia nyingi za sasa imekuwa ndogo na mama amekuwa mbadala wake.
Amesema hali hiyo imechangiwa na harakati za kumkomboa mwanamke ambazo zimemfanya awe imara kifikra na kiuchumi hivyo kuwa tayari kubeba majukumu ya familia.
“Hii 50 kwa 50 imetafsiriwa vibaya wanawake wanabeba majukumu yasiyo wao na hilo linawafanya wababa wajisahau matokeo yake wanakuwepo tu kwenye familia lakini hawasimami kwenye nafasi zao.
“Hili limesababisha hata wanawake siku hizi kuwa tayari kulea watoto bila uwepo wa baba lakini uhalisia ni kwamba nafasi ya baba kwenye malezi ni kubwa hivyo ni muhimu kwao kulitambua hilo na kutimiza wajibu wao,”