Watu unaopaswa kuambatana nao ili ufanikiwe kiroho, kimwili

Muktasari:
- Kwenye Maisha haya tuliyonayo ili tufanikiwe tunahitaji watu ambao watasimama na sisi katika hali zote, unapohitaji msaada wao kipindi cha uhitaji watakuwa Pamoja na wewe. Hawa ni aina ya watu ambao Watakuombea utakapohitaji maombi, Watakupa mtaji biashara yako ikianguka, Watalia na wewe kwenye shida, Watakushauri na ukianguka wataanguka na wewe.
Bwana Yesu asifiwe! Karibu katika tafakari ya neno la Mungu. Leo utakuwa na mimi Mwalimu Edson Sanga kutoka KKKT Usharika wa Tandika. Ni maombi yangu kwa Bwana, Roho mtakatifu akuhudumie unaposoma ujumbe huu.
Leo tumepewa ujumbe unaosema “AINA YA WATU UNAOWAHITAJI ILI UWEZE KUFANIKIWA KIROHO NA KIMWILI”. Ukweli ni kwamba tunaishi kwenye maisha ambayo tunahitaji kufanikiwa, lakini ni muhimu kufahamu kwamba asilimia kubwa ya mafanikio yetu yamebebwa na watu waliotuzunguka, kwa maana kwamba kuna aina ya watu ni wa muhimu sana kwenye maisha yako ili ufanikiwe kwenye kile unachokifanya au kule unapotakakwenda.
Aina ya watu unaowahitaji ili uweze kufanikiwa ni hawa wafuatao:-
Watu/mtu atakayeamini kwenye maono uliyobeba/atakayeamini kwenye mipango na malengo uliyonayo
Kwenye Maisha yako ili ufanikiwe unahitaji watu watakaoamini kwenye kile ulichobeba na watakaoamini kwenye mipango na maono uliyonayo. Kuna watu wakikuangalia leo hii watakudharau, watakuona hufai kutokana na mazingira uliyonayo, lakini wapo watu ambao Mungu amewapa neema ya kuona kesho yako, wanauwezo wa kuuona kitu kilichopo ndani yako ambacho watu wengine hawajakiona. Watu waliamini kwenye maono aliyobeba Daudi wakati hana kitu.
1. Samweli 22:1-2 “Basi Daudi akaondoka huko, akakimbilia pango la Adulamu; na ndugu zake na watu wote wa mbari ya baba yake waliposikia habari hiyo wakamuendea huko.”. Hapo utaona baada ya Daudi kuondoka kwa mfalme Sauli, kwa sababu Mfalme Sauli alikuwa anapanga mipango ya kumuua, kuna watu wachache ambao waliamua kumfuata Daudi kipindi hana kitu chochote kwa sababu waliamini kwenye maono ya Daudi kwamba atakuja kuwa kiongozi mkubwa baadaye.
Watu watakaosimaam na wewe katika nyakati ngumu/watu watakaokutegemeza.
Kwenye Maisha haya tuliyonayo ili tufanikiwe tunahitaji watu ambao watasimama na sisi katika hali zote, unapohitaji msaada wao kipindi cha uhitaji watakuwa Pamoja na wewe. Hawa ni aina ya watu ambao Watakuombea utakapohitaji maombi, Watakupa mtaji biashara yako ikianguka, Watalia na wewe kwenye shida, Watakushauri na ukianguka wataanguka na wewe.
Yoshua alimuhitaji Musa ili aweze kushinda vita dhidi ya Waamaleki, lakini Musa pia aliwahitaji Haruni na Huri. Kutoka 17:8-13 “Wakati huo Waamaleki wakatokea, wakapigana na Israeli huko Refidimu. 9 Musa akamwambia Yoshua, Tuchagulie watu, ukatoke upigane na Waamaleki; kesho nitasimama juu ya kilele kile, na ile fimbo ya Mungu nitakuwa nayo mkononi mwangu. 10 Basi Yoshua akafanya kama Musa alivyomwambia, akapigana na Amaleki; na Musa na Haruni na Huri wakapanda juu ya kile kilima. 11 Ikawa, Musa alipouinua mkono wake, Israeli walishinda; na alipoushusha mkono wake, Amaleki walishinda. 12 Lakini mikono ya Musa ilikuwa mizito;basi wakatwaa jiwe, wakaliweka chini yake akalikalia. Haruni na Huri wakaitegemeza mikono yake, mmoja upande hu una mmoja upande huu; mikono yake ikathibitika hata jua lilipokuchwa. 13 Yoshua akawaangamiza Amaleki na watu wake kwa ukali wa upanga”.
Ni maombi yangu kwa Bwana akuinulie Musa wa kwako atakayesimama na wewe kwenye nyakati mgumu unazopitia kwenye maisha yako.
Watu watakaokutambulisha/watakaotambulisha kitu ulichobeba/watakaokuunganisha mahali.
Kwenye Maisha ili uweze kufanikiwa kwenye kile ulichobeba haijalishi una upako mkubwa wa aina gani unahitaji watu watakaokuunganisha kwenye kile ulichobeba. Unahitaji mtu wa kukuunganisha kwenye hiyo kazi unayoitafuta. Unahitaji mtu wa kukuunganisha kwenye hiyo tenda unayoitafuta, Kuna mahali utakwama mpaka atokee mtu wa kukutaja ndipo utafanikiwa, haijalishi upako ulionao. Kuna mahali hautafika na upako wako. Ila utafika kwa sababu kuna mtu mmoja ametaja jina lako. Kwa hiyo ni muhimu sana kuwaombea watu wa aina hii ambao Mungu amewaweka kwenye Maisha yako.
Kuna ofisi ukienda na bahasha ya Cv zako zitawekwa pembeni na inawezekana ukawa umetoka nazo kwenye maombi zimelowa mafuta ya upako zitawekwa kando kwa sababu zimelowa mafuta ya upako! Ila kuna mtu akisema usikilizwe utasikilizwa na kazi utapata.
1 Samweli 16:13-22. Ukisoma hapa utaona namna ambavyo Daudi kapakwa mafuta na Samweli, lakini aliendelea kuchunga kondoo mpaka alipotokea mtu wa kumtaja ikulu kwa Sauli. Kupata kazi kwa Daudi kulitokana na yule mfanyakazi aliyemtaja kwa Farao. Mungu akuinulie mtu wa kwako ambaye atakutaja kila mahali ambapo utahitajika.
Asante sana kwa kujifunza Pamoja nami, Mungu akubariki na akajibu kila hitaji la Moyo wako. Amina.
Mwalimu Edson Sanga. Anapatikana KKKT Usharika wa Tandika
+255 689 336446, 0673 581836