Mungu anapenda ufanikiwe kiuchumi

Mwalimu Mgisa Mtebe.
Katika Neno takatifu la Mungu tunalotumia kwa lugha ya sasa, hakuna mahali neno ‘uchumi’ limetajwa popote. Lakini kutokana na tafsiri halisi ya uchumi, tuliyojifunza hapo juu, uchumi umetajwa katika Biblia Takatifu kwa namna nyingi na kwa mara nyingi. Mungu ndiye muumba wa mali na rasilimali zote za dunia, na anataka mimi na wewe kama watoto wake, tuweze kuzirithi na kuzitumia baraka hizi zote, ili kulitimiza kusudi lake.
Kwa tafsiri rasihi kabisa, ninaweza kusema hivi …
Uchumi ni maarifa au akili ya mtu kutumia fursa na rasilimali zilizopo, na kuzigeuza katika namna ambayo, atatimiza mahitaji yake na matakwa yake, kwa njia bora zaidi.
Hapa chini, nimekuwekea baadhi ya mistri kutoka katika maandiko matakatifu, ili uweze kuona uchumi ulivyotajwa katika Neno la Mungu, ili ujue kuna kusudi la Mungu juu ya mali na rasilimali alizotuwekea duniani.
“26 Ndipo Mungu akasema, “Tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu, wakatawale samaki wa baharini na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia dunia na vyote viijazavyo; na mtu huyu aende kutawala viumbe wote watambaao juu ya nchi.’’
28 Mungu akawabariki (Adam na Eva) na kisha akawaambia (akawaagiza akisema), “Zaeni na mkaongezeke, mkaijaze tena dunia yote na kuitiisha. Mkatawale samaki (wote) wa baharini, ndege (wote) wa angani na kila kiumbe hai kiendacho juu ya nchi (ardhi).’’ (Mwanzo 1:26-28)
Kwakuwa uchumi ni maarifa ya kutumia rasilimali za Mungu, na hapa juu, tunaona Mungu anatuamuru watoto wake, twende ulimwenguni tukatawale rasilimali zake, kama vile samaki wa baharini, na wanyama wa ardhini na ndege wa angani, na nchi yote pia; yaani misitu, migodi, mito, ardhi, anga, n.k.
Kusudi la Mungu juu ya uchumi
Madhumuni makuu, ya umiliki mzuri wa nchi (uchumi) ni mwanadamu aweze kumwabudu Mungu vizuri zaidi, kwa moyo uliotulia, moyo usio na mahangaiko, kutokana na masumbufu ya mahitaji mbalimbali ya maisha.
Tangu mwanzo wa uumbaji, Mungu alipomuumba Adam na Eva, Mungu alitaka wanadamu tuzitumie rasilimali za nchi, kwa kuzigeuza ziwe majibu ya mahitaji yetu, ili tuishi maisha mazuri, hatimaye tuweze kumwabudu Mungu vizuri, bila kuwa na masumbufu ya moyoni, kutokana na kukosa mahitaji muhimu ya maisha.
Uchumi na Ibada
Katika maisha ya mwanadamu, wito maalumu ambao ni mkuu kabisa, ni kumsifu na kumwabudu Mungu. ‘Maisha ya Ibada’ ni wajibu mkuu kabisa na ni wito Mtakatifu, tuliobebeshwa na Mungu, kwa sababu hiyo, Mungu ametupa uchumi, ili tusiishi maisha ya dhiki, ili wanadamu tuweze kumwabudu Mungu vizuri zaidi, bila usumbufu na mahangaiko ya moyoni (ambako ndipo ibada halisi inapotokea). Neno la Mungu linasema hivyo katika kitabu cha Mithali, kwamba; ‘Linda sana moyo wako, kuliko vitu vyote, kwani huko ndiko zitokapo chemchemi za uzima’ (Mithali 4:23).
Kwa hiyo, uchumi (rasilimali zote) ziliwekwa na Mungu hapa duniani, maalumu kabisa, kwa ajili ya kutuwezesha wana wa Mungu, tuwe na maisha mazuri, kwa madhumuni ya kumtengenezea Mungu ibada nzuri.
Utauona ukweli huu katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati 28:47-48, inasema; ‘kwakuwa haukumtumikia Bwana Mungu wako kwa moyo wa furaha katika wingi wa vitu nilivyokupa (rasilimali za dunia), sasa nitakupeleka utumwani, ukamtumike adui yako, katika hali ya njaa, kiu, na uchi; na katika hali ya uhitaji wa vitu vyote. Tena ukiwa huko utumwani, nitakuvika kongwa, mpaka uangamie’
Hilo neno ‘wingi wa vitu’ limebeba uchumi wa mtu, na hilo neno ‘kumtumikia kwa furaha’ ndio maisha ya ibada. Kumbe, moja ya sababu ya Mungu kukupa wingi wa vitu, ni ili uweze kumtumikia Yeye kwa furaha na kwa moyo wa shukurani. Ndio sababu, shetani anatafuta sana kuvuruga mazingira ya mtu, maana anajua, akivuruga mazingira, atakuwa amevuruga na maisha ya mtu, na moja kwa moja atakuwa, amevuruga na ibada yake pia. Mathayo 15:8-9 na tunaona Bwana wetu Yesu Kristo, anasema kwamba;
"… Watu hawa wananiabudu kwa midomo tu, lakini mioyo yao iko mbali nami; nao wananiabudu bure … " (Mathayo 15:8-9).
Watu wengi wanapokuja ibadani, wanakuja kimwili zaidi, kwasababu mioyo yao iko mbali, ikiwaza mahitaji na masumbufu ya Maisha, badala ya kumtafakari Mungu. Na ndio maana Bwana Yesu anamalizia kwa kusema, “… Nao wananiabudu bure …” (mstari wa 9). Kumbe, usipotawala vizuri mazingira yako na maisha yako, lazima moyo wako, utakosa utulivu wakati wa ibada. Kitabu cha Wakorintho. Imeandikwa;
8 Naye Mungu aweza kuwapa kila baraka kwa wingi, ili katika mambo yote na kila wakati, mwe na kila kitu mnachohitaji, ili mweze kushiriki vizuri kwa wingi katika kila kazi njema yenye kuujenga Ufalme wa Mungu (2Kor 9:8,11)
Kwahiyo, njia ya Mungu ya kutufanya watoto wake, kuishi maisha ya ziada na utoshelevu, ni kutupa akili na maarifa ya kugeuza hizi rasilimali zote alizotuwekea humu humu duniani, katika namna ambayo zitaweza kutimiza mahitaji yetu na matakwa yetu; hatimaye maisha yawe bora zaidi.
Mwalimu Mgisa Mtebe ambaye pia ni mchumi, anapatikana kwa Mawasiliano +255 753 497 655, baruapepe: [email protected]
www.mgisamtebe.or.tz