Wanaume tusijifanye poa kumbe tunaangamia

Muktasari:
- Takwimu vinaonyesha sisi wanaume ndio tunaoongoza Kwa kujitoa uhai
Dar es Salaam. Mwezi huu pekee, tumeshuhudia ongezeko la matukio ya wanaume kujitoa uhai; kwa Tanzania tu, yametangazwa zaidi ya matukio manne, mengi yakiwa ya vijana.
Lakini tukubaliane: hili si jambo jipya. Takwimu zimekuwa zikituonyesha kwa muda mrefu kuwa wanaume ndiyo tunaongoza kwa kujitoa uhai.
Sababu ni nyingi; msongo wa mawazo, majukumu ya maisha, kutokuwa na watu wa kuwaeleza changamoto zetu, hofu ya kuhukumiwa, na ukosefu wa sehemu salama za kutoa ya moyoni.
Leo, naomba kuwakumbusha wanaume wenzangu kitu kimoja: tujuliane hali, tena tujuliane hali kwa dhati.
Sio zile salamu za "vipi bro?" halafu tunaendelea na maisha kana kwamba kila kitu kiko sawa. Tuwe tayari kusikiliza, na pia kusema ukweli wetu. Wakati mwingine mtu anaweza kukwambia “niko poa”, lakini moyoni anazama, anaangamia, anateketea.
Takwimu zinasema: wanaume wanaonekana na nguvu, wanaume wanaonekana na furaha, wanaume wanaonekana wamejipanga na wamejipata kimaisha, wanaume wanaotabasamu kwenye mitandao ya kijamii, wanaume wanaochangamsha vikao na wacheshi zaidi vijiweni, mara nyingi ndiyo wanakuwa kwenye hatari zaidi.
Kwa nini? Kwa sababu tunaamini sura wanazotuonyesha nje. Tunadhani “ni mcheshi” hivyo hawezi kuwa na huzuni.
“Ana akili sana” hivyo hawezi kusumbuliwa na mawazo madogodogo. “Ana connection” hivyo ana watu wa kumpa msaada.
“Ana biashara zake”, au “ana familia nzuri” kwahiyo lazima atakuwa sawa tu. Lakini hatujiulizi, je, kweli yuko sawa? Je, kuna mtu huwa anamuuliza ‘vipi bro’ akitegemea jibu la ‘ukweli?’ jibu la dhani.
Watu kama hawa wanabeba mzigo mkubwa. Wanabeba familia, marafiki, kazi, ndoto na matarajio. Na kwa sababu wanaonekana ‘wakomavu’, hawapewi nafasi ya kuwa dhaifu. Hakuna anayefikira kwamba hata wao wanahitaji kusikilizwa. Hapa ndipo tunaposhindwa kama jamii.
Tunahitaji kubadili mtazamo wetu. Tukubali kwamba hata “wanaume wa shoka” huvunjika.
Ukiona rafiki yako ambaye kila siku anatuma ujumbe wa kuhamasisha, au yule jamaa ambaye kila wakati anakuwa na stori za kufurahisha, usiishie tu kusema kumjibu kwa emoji za kucheka, siku moja moja tuwe tunawauliza wanaume wenzetu tunaodhani wako vizuri kwamba “Bro, hali yako ikoje?” Tena tuwaulize kwa dhati.
Tujifunze kusikiliza bila kutoa hukumu. Tujifunze kuwa mabega ya kupumzikia hata kwa waliotuzoesha kuwa mabega yao.
Kwa sababu wakati mwingine, watu wanaoonekana kama miamba ya jamii, wanahitaji msaada zaidi ya tunavyodhani.
Na kama wewe ni mmoja wa hao unaoonekana uko sawa, lakini kwa ndani unaumia, jua kwamba si lazima uvumilie peke yako. Kuna watu watakusikiliza, watakuelewa, na kukuzingatia ikiwa tu utajaribu kufunguka yanayokusibu.
Tusisubiri kupoteza mtu ndipo tuanze kusema, “Jamaa alikuwa anakuja hapa kijiweni anatuchekesha kila siku…”