Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Aliyefukuzwa Magereza miaka 25 iliyopita agonga kisiki mahakamani

Muktasari:

  • Kwa miaka 25 sasa, aliyekuwa askari wa Jeshi la Magereza, Arcado Rugohe amekuwa akifuatilia nakala ya uamuzi wa kufukuzwa kwake kazini bila mafanikio, jambo lililosababisha kwenda mahakamani kuomba amri ya kumlazimisha Kamishna wa Magereza ampatie nakala ya uamuzi wa kufukuzwa huku Mahakama ikitupa maombi yake kwa sababu za kiufundi.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Kuu imetupilia mbali maombi ya ofisa wa zamani wa Jeshi la Magereza, ambaye alifukuzwa kazi miaka 25 iliyopita, Arcado Simon Rugohe ya kumlazimisha Kamishna Mkuu wa Magereza (CGP), kumpatia nakala ya uamuzi huo.

Rugohe aliyekuwa amefikia cheo cha WDR alifukuzwa kazi Agosti 26, 1998, lakini hakupewa nakala ya uamuzi huo wa kumfukuza.

Hivyo Oktoba 12, 2023 alifungua maombi ya kibali dhidi ya Kamishna Mkuu wa Magereza na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akiomba aruhusiwe kufungua shauri la maombi ya mapitio ya mahakama (judicial review), ili mahakama itoe amri ya kumlazimisha Kamishna Mkuu wa jeshi hilo ampatie nakala ya uamuzi huo.

Hata hivyo, mahakama hiyo katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Abdi Kagomba aliyesikiliza shauri hilo la maombi namba 49/2023, imeyatupilia mbali maombi yake hayo, baada ya kukubaliana na hoja za pingamizi la awali lililowekwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Jaji Kagomba katika uamuzi huo alioutoa jana Alhamisi, Novemba 23, 2023 amesema askari huyo hajatimiza moja ya vigezo vinne ili kuruhusiwa kufungua shauri la mapitio, yaani kutumia kwanza fursa zinazopatikana ndani ya taasisi inayolalamikiwa kabla ya kwenda mahakamani.

Amesema katika hoja hiyo mtizamo ingekuwa ni kama askari huyo aliomba nakala ya uamuzi huo na kama alinyimwa basi alipaswa kuwa amekata rufaa kwa mamlaka ya juu ya kamishna huyo si tu lengo la kupingwa kufukuzwa kazi bali pia kunyimwa huo uamuzi.

Akirejea kiapo cha mwombaji, Rugohe, Jaji Kagomba amemnukuu askari hiyo akisema kwa tafsiri isiyo rasmi kuwa: "La kushangaza sana mjibu maombi wa kwanza (Kamishna) bila kufuata utaratibu na bila kuzingatia matakwa ya sheria aliniondoa katika ajira bila kunipatia nakala ya uamuzi huo...”

"Kutokana na kutokuridhishwa na uamuzi wa mjibu maombi wa kwanza nilichukua hatua za ndani kwa kukata rufaa kwa mjibu maombi wa kwanza na kufuatilia bila mafanikio. Kisha nilikata rufaa kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ambapo Mei 3 ilifikia maamuzi yake (kuikataa rufaa yake).” Amesema Jaji.

Ingawa Rugohe alidai ameambatanisha nakala ya uamuzi huo wa Wizara, lakini Jaji Kagomba amesema amedurusu kwa umakini kiapo chake na viambatanisho na kwamba kuna upungufu unaojionesha dhahiri.

Kwanza amesema rufaa aliyosema alikata Wizara ya Mambo ya Ndani, haijaambatishwa kwenye kiapo.

"Hii ni muhimu kubaini kama mwombaji (Rugohe) alimlalamikia mjibu maombi wa kwanza (Kamishna)...alimlalamikia kumpa nakala ya maandishi ya uamuzi wake au alikata rufaa dhidi kuondolewa katika ajira," amesema Jaji Kagambo.

Amesema viambatanisho vilivyotajwa A.2 havilalamikii kunyimwa nakala ya uamuzi bali vinazungumzia kuondolewa katika ajira na kwamba viambatanisho hivyo ambavyo vinaonekana kuwa mawasiliano ya Kiserikali havikuelekezwa kwa Kamishna huyo.

"Hivyo haviwezi kusemekana ni uamuzi wa mwisho kwa kutumia njia za ndani kutafuta nafuu hiyo, kiasi cha kustahili mwombaji (Rugohe) kugonga milango ya Mahakama," amesema Jaji Kagomba na kuhitimisha;

"Kwa sababu hizo ninaona kwamba hoja ya pili ya pingamizi ina mashiko na inakubaliwa. Hivyo maombi haya yanatupiliwa mbali kwa kufunguliwa mahakamani kabla ya wakati. Hakuna amri kuhusu gharama za kuendesha shauri."

Awali, Jaji Kagomba aliikataa sababu ya kwanza ya pingamizi la Serikali kuwa shauri hilo limefunguliwa nje ya muda, yaani miaka 25 baadaye uamuzi wa kuondolewa katika ajira badala ya ndani ya miezi sita kama ambavyo kanuni ya sita Tangazo la Serikali namba (GN) 324 ya mwaka 2014 inavyoelekeza.

Jaji Kagomba amesema kwamba licha ya kutambua matakwa ya kanuni hiyo lakini pia kila shauri linaamuriwa kwa mazingira yake.

Wakati wa usikilizwaji wa pingamizi hilo wajibu maombi waliwakilishwa na Wakili wa Serikali Nkamba Nshuda na mwombaji, Rugohe aliwakilishwa na Wakili Mohamed Menyanga.