Prime
Umewahi kujishtaki kwa mwenza wako?

Muktasari:
- Ukienda kituo cha polisi kujiripoti, hata kama utawekwa ndani au vinginevyo, itachukua muda kwa polisi kukuamini kama siyo kudhani una changamoto za kiakili.
Je, kuna mtu anayeweza kutenda kosa na kwenda kujiripoti kituo cha polisi au kujishitaki?
Katika mazingira ya kawaida, hili haliwezekani. Ukienda kituo cha polisi kujiripoti, hata kama utawekwa ndani au vinginevyo, itachukua muda kwa polisi kukuamini kama siyo kudhani una changamoto za kiakili.
Maana, katika hali ya kawaida, hili si jambo la kawaida. Mfano, ukienda mahakamani kujishitaki, kama utapata hakimu mwenye busara, ima utaambiwa sheria haifanyi kazi hiyo au utaambiwa uende ujiadhibu au kujisamehe, au kujishitaki kwa uliyemkosea.
Hata hivyo, katika ndoa, mambo ni tofauti kabisa. Tofauti na kwenye maisha ya kawaida, mwanandoa anapomkosea mwenzake, ama anaweza kukana na kuongeza tatizo, au matatizo au kuamua kujishitaki kwa mwenzie ili wapata namna ya kushughulikia kosa husika.
Je, ni wangapi wanajishitaki wanapowakosea wenzao? Pamoja na kuwa waja kama wewe, sisi, kama wanandoa, huwa tuna tabia ya kujishitaki.
Mfano, ukimuudhi mwenzio, usingoje alalamike au kuchukua hatua. Unachopaswa kufanya ni kujiwahi na kujishitaki kwa dhati.
Je, unaanzaje? Ni rahisi. Kawaida wanandoa huongea mambo mengi makubwa na madogo, muhimu na hata yasiyo muhimu.
Pia, wana namna yao ya kuwasiliana. Inapotokea ukagundua kuwa kuna ukimya au utofauti katika mazoea haya, unapaswa kujiuliza ni wapi umeteleza au kukosea.
Baada ya hapo, unaweza kumkabili mwenzio na kumueleza mawazo yako. Kama huwezi, unaweza kumtumia ujumbe hasa wakati huu wa simu za rukono. Zamani, kama hali hii ikitokea, sisi tulizoea kuandikiana barua kana kwamba tunaishi mbali.
Katika barua hii, ‘mkosaji’ alielezea alichofanya au kusema na namna alivyodhani kingeeleweka. Baada ya mwenza wake kusoma ile barua au ujumbe, naye alitoa namna alivyoelewa hiki chanzo cha makosa au mtanziko.
Hapa, mkosewa anaweza kulalamika, kupinga uelewa na malengo ya mwenzake na mengine mengi.
Kimsingi, kuandika barua au kutuma ujumbe siyo jibu bali fursa, mbinu, sababu, na sehemu ya kuanzia majadiliano.
Katika kila kutoelewana au mgogoro hata uwe baina ya taifa na taifa, njia ya kwanza ya kuleta maelewano na kurejesha amani na hali ya kawaida ni majadiliano. Hata hivyo, majadiliano ambayo, mara nyingi, huzaa maridhiano, hayawezekani bila ya aliyekosea kuanza kuchukua hatua ili kumuonyesha mkosewa kuwa anaelewa alichofanya na anamthamini mwenzake.
Hii njia ya kujishitaki na kujitetea kwa kuandikiana kusema ukweli ni tulivu na huwawezesha wanandoa kusomana na kujua tatizo ni nini au nani kwa haraka na urahisi.
Falsafa yetu ni kwamba usiende kazini, kulala, au safarini ukiwa na hasira kwani, itavuruga kila kitu bure ukizingatia kuwa hasira ni hasara.
Pia, hasira ina madhara mengi kwa afya ya binadamu ilhali furaha ina faida nyingi kwake. Chagua furaha badala ya hasira kuepuka kupata karaha na hasara. Hivyo, kwa kuzingatia unyeti huu, tumeona tudurusu taasisi hii adhimu na tamu japo wakati mwingine yaweza kuwa chungu ya ndoa ili kuwasaidia wale inaowakwaza au wanaoiingia bila kuelewa wanachofanya kwa undani zaidi.
Kuna msemo kuwa waliomo wanatamani kutoka na walio nje wanatamani kuingia. Wengine huiita ndoa ndoana ingawa siyo hivyo.
Msemo huu humtahadharisha yule anayedhamiria kufunga ndoa kujiandaa. Kama watu wangejali mafundisho ya baadhi ya nahau, methali na misemo, basi msemo huu ungewafumbua macho kutafiti kwanini wanataka kuingia kwenye kitu ambacho waliokwishaingia wanatamani watoke?
Wahenga wanaasa kuwa kiburi si maungwana na hewala si utumwa. Kwa kuzingatia busara na nasaha hizi, wanandoa wajue wazi kuwa, kama waja wengine, na wao wanatenda makosa si mara moja wala mbili jambo ambalo ni asili ya utu wao.
Hivyo, lazima wanandoa wajitengenezee nyenzo za kukabiliana na asili hii ya ubinadamu wao. Wakati wakifanya hili, wajue kuwa wagombanao ndiyo wapatanao na majembe yalimayo konde moja, hayakosi kugongana.
Mwisho, je ni wanandoa wote wana mawazo au uthubutu wa kujishitaki kabla ya kungoja washitakiwe na wenza wao waliowakwaza au kuwakosea? Hakuna lisilowezekana chini ya jua.
Anza kufanyia kazi mbinu hii. Utaona mafanikio yake tena haraka. Kwa miaka takribani 30 ya ndoa, tumegundua kuwa mbinu hii ni mujarabu.
Hapa ndipo kunabidi kujiuliza zaidi na zaidi. Je, mnao utaratibu huu? Kama hamna, mko tayari kuujaribu? Ujaribuni. Hamtajuta. Tukutane wiki ijayo.