Prime
Wanandoa kuweni kama maji na samaki, mfaidi

Muktasari:
- Hakika busara ikiwa siyo haba, hakuna maisha yenye raha kama maisha ya ndoa, muwe matajiri au maskini.
Je, unakijua kisa cha samaki na maji? Viumbe wote walipoumbwa, walichagua sehemu za kuishi.
Wapo waliokwenda mwituni. Wapo waliochagua kufanya kazi usiku na kupumzika mchana. Samaki alichagua maji na maji yalimchagua yeye.
Siku moja, samaki alivuliwa akayaambia maji: “Mpenzi wangu buriani maana, hatutaonana tena.” Maji nayo yalijibu: “Mpenzi huna haja ya kuniaga maana, nitakuwa nawe maisha yangu yote kama ambavyo utakuwa nami.”
Kwa kujua kuwa ndoa ya wawili hawa ni ya kudumu, samaki alipata faraja na kuondoka na mvuvi.
Akiwa mpweke asione samaki hata mmoja wa kumfariji, mara mvuvi alimpa mkewe yule samaki akampike. Mama alichukua maji na kuanza kumsafisha kwa maji yule samaki aliyeshangaa na kuamini maneno ya rafiki yake kipenzi yaani, maji.
Hata hivyo, furaha ya samaki ilikwisha baada ya kumaliza kuoshwa na kuwekwa kwenye chombo tayari kwenda kukatwa katwa.
Hapa, samaki alimwambia tena rafiki yake maji kuwa wasingeonana tena. Maji, kama ada, yalisema asitie shaka, kwani, hatakuwapo wa kuwatenganisha. Maana, aliyewaunganisha ni mmoja.
Mama alimkatakata yule samaki na kumweka kwenye chungu tayari kumpika.
Samaki akiwa amekata tamaa asingemuona tena rafiki yake, alistuka pale mama alipomimina maji kwenye chungu na kuweka mekoni.
Mara samaki anamuona mpendwa wake tena! Mambo yalikuwa hivyo hadi chakula kilipoiva na kukutana tena mezani ambapo baada ya samaki kuwekwa mdomoni mwa binadamu alijua huu ndiyo ungekuwa mwisho wa kuwa na rafiki yake maji.
Kabla hata ya kumaliza kuwaza, mlaji aliomba glasi ya maji asukumizie mlo wake. Kwa mara nyingine, samaki na maji walijikuta pamoja. Mlaji aliendelea kula.
Baada ya kumeza tu, samaki alikutana tena na maji tumboni na wakakaa wote huko. Je, wenza wa kweli siyo sawa na maji na samaki?
Anayatakakuwatenga, hutenda jambo baya kwa vile hakuwaunganisha. Usipoteze muda na maisha yako kutaka kuua usichoweza kukiumba.
Wala usijisumbue kutenganisha kilichounganishwa na Mungu. Ukifanikiwa, kuna siku nawe utauawa au kutengwa kama ulivyotenga na kuua. Je, busara hapa ni nini?
Tunajifunza mini?
Mara nyingi, wanapokufa wenza huzikwa karibu ya wenza wao. Hakuna azikwaye na watoto wake vinginevyo wafe bila wenza au wakiwa wachanga. Watoto wenu, hasa waliopata waliowachagua katika maisha yao, huzikwa kwao ama kwa waume zao au kwako lakini na wake zao.
Hili ndilo somo kuu la ndoa ambalo limewashinda wengi. Hakika busara ikiwa siyo haba, hakuna maisha yenye raha kama maisha ya ndoa, muwe matajiri au maskini.
Mababu zetu walioana kwa majembe na mikuki. Hawakuwa na vyeti vya ndoa wala mapadri na masheikh wa kuwafungisha ndoa. Hwakujimwagia Champagne, kwenda fungate wala kubeba mashada ya maua.Hawakukodisha kumbi na magari ya bei mbaya.
Walijua mashada huwa ya makaburi na ni makabauri yahitajiyo mpambaji. Hawakuvishana pete za fedha wala dhahabu. Hawakuvaa suti wala shela lakini bado walioana wakatutuza japo baadaye tuliwaona na kuwaita waliopitwa na wakati!
Nani kapitwa na wakati kati yao na sisi tusiojua hata wakati ni nini kiasi cha kuupoteza tena kwenye ujinga na uovyo? Ama kweli shukrani ya punda ni mateke.
Huwa busara anashangaa jinsi tulivyoongoza njia kwenda kwenye maangamizi ambayo yamekuwa chanzo cha mmomonyoko wa maadili.
Bibi zetu hawakuvaa sidiria ili maziwa yao yaonekane bado wamo. Ya nini iwapo kuzaa na kunyonyesha ilikuwa heshima na jambo la kujivunia? Wangevaa sidiria ili wamvutie nani?
Bibi na babu hata mama na baba hawakukata keki zaidi ya kushikana mikono na kujinywea pombe. Wala hawakwenda kanisani kuimbiwa na kupigiwa vigelegele.
Kwao, Mungu alikuwa kila mahali. Wangeendaje kanisani wakati kanisa lilikuwa nyoyo zao? Wala hawakula viapo. Wangeapia nini iwapo walikuwa wakipendana kweli kweli bila kujali alichokuwa nacho mtu zaidi ya utu wake?
Leo watu wanalishana viapo. Kesho wanavivunja na kutimuana tena kwa kashfa na aibu. Bado wanasema ni usasa wakati ni kuvunjika mioyo! Nani anaichukia jana iwapo leo yake ni mazabe matupu? Tusionekane tunazusha. Angalia idadi ya ndoa zinazovunjika na jinsi wanandoa wanavyozidhalilisha. Zamani hapakuwapo na nyumba ndogo. Zamani watu walikuwa wakweli. Walioa na kuolewa mitala bila kificho na unafiki. Wanandoa kuweni kama maji na samaki mfaidi ndoa na maisha yenu.