Prime
Mike Msudani aliyemkimbia bi mkubwa wa Kizungu

Muktasari:
- Kama vijana wengine wengi wageni wasio na elimu wala uzoefu wa kutosha, Mike aliangukia kwenye mikono ya mama mzee wa Kizungu ambaye mwanawe alikuwa anakaribiana na umri wake.
Mike (si jina lake) ni kijana kutoka Sudani ya Kusini aliyekimbilia mapigano kwao na kuhamia Canada kama mkimbizi.
Kama vijana wengine wengi wageni wasio na elimu wala uzoefu wa kutosha, Mike aliangukia kwenye mikono ya mama mzee wa Kizungu ambaye mwanawe alikuwa anakaribiana na umri wake.
Baada ya kuhamia Canada, bibi huyu tutakayemuita Molly (si jina lake) alitokea kumsaidia Mike asijue mwisho wa takrima hii ingekuwa ndoa ya mateso.
Kwa vile Mike alikuwa mgeni na mhitaji, alijiona kapata asijue amepatikana. Mapenzi motomoto yalianza baina yake na kibibi kilichomzungusha kila mahali na kumfundisha hata kuendesha gari na mambo mengine kama vile lugha ya Kiingereza.
Mike alifurahi sana na kujihisi mwenye bahati asijue alikuwa ameangukia kwenye mdomo wa chatu kama siyo mamba.
Hata hivyo, kadri muda ulivyokwenda, Mike alianza kustuka na kujutia uamuzi wake wa kuishi na bi Kizee aliyemzidi umri mbali na kwamba asingeweza kumzalia mtoto japo hakutaka kuzaa.
Kadri walivyozoeana, kizee kilianza kummilki Mike kiasi cha kuhisi hakuwa na uhuru tena. Kila alipokwenda, ama kibibi kilitaka waandamane au ajieleze anakwenda kufanya nini na kukutana na nani. Mbali na kubanwa, Mike alianza kuhisi vijana wenzake wa Kiafrika wakimsengenya hata wengine kumsuta mbali na kumtenga.
Mwanzoni, aliwachukia akidhani walikuwa wakimuonea wivu asijue walikuwa wakimuonea huruma kwa alivyokuwa amenaswa asifurukute.
Woga ulianza kukitanda kile kibibi bila kumsaza Mike aliyejihisi kauza uhuru wake na kuwa mtumwa wa mapenzi.
Mapenzi aliyotafuta yaliishia kuwa karaha, majuto na mateso. Mike alianza kukonda, kusongwa na mawazo hadi akaanza kunywa pombe na kugeuka mlevi.
Taratibu, Mike alianza kuamrishwa kama mtoto mdogo, kumilikiwa kwa hofu angechukuliwa na mimama mingine tena iliyokuwa vijana kuliko huyu mzee wake. Kimaisha, Mike alianza kuwa kama mfanyakazi wa ndani.Kimsingi, Mike alijikuta kashikwa na kushikika asijue namna ya kujinasua. Alitegemea kupata akaishia kupatikana.
Akiwa ameanza kuchukia na kukata tamaa, rafiki yake mwingine aliyewahi kupitia maisha hayo alimshauri atoroke mkoa na mji ule.
Mike hakuwa na la kufanya bali kumtoroka yule mama na kwenda kuishi mkoa mwingine. Hata hivyo, alikwishaudhika, kukata tamaa, na kuteseka kimawazo. Maana, baada ya kuwa amezoea maisha ya ughaibuni, Mike alipata shinikizo la wazazi wake waliokuwa kwao wakimtaka arudi na kumchukua mke waliyekuwa wamemtafutia.
Hii ni baada ya wenzake kuwatonya kuwa mtoto wao alikuwa ameangukia mikononi mwa shankupe la Kizungu. Mama yake Mike alitishia kumwachia laana kama angeendelea kuishi maisha ya namna ile.
Kwa upande mwingine, kumuacha yule mama wa Kizungu, kwanza, ilikuwa vigumu. Pili, Mike hakutaka mkewe mtarajiwa aliyechaguliwa na wazazi wake kutoka nyumbani ajue uhusiano huu.
Tatu, Mike alishagundua udhaifu mwingi hasa uhusiano wa mkewe na wanyama, mgawanyo wa madaraka kwenye nyumba, na ukosefu wa umakini katika kufikia uamuzi uliosababishwa na tamaa na ukosefu wa uzoefu, hata ushauri.
Wakati Mike alipoamua kuishi na yule bi kizee, alisukumwa na kitu kimoja kuwa alikuwa amevuka umri wa kuzaa.
Hivyo, asingekumbwa wala kupambana na tatizo na kuzalisha watoto na kuachana na aliyezaa naye lakini sheria ikambana popote atakapokuwa ughaibuni kuwatunza.
Kimsingi, Mike aliangalia upande mmoja wa sarafu sawa na wengine wengi kama yeye waliojiingiza kwenye vinywa vya chatu wasijue namna ya kujinasua. Pia, Mike hakujua kuwa wenzake aliotoka nao kwao wangevujisha taarifa kwa wazazi wake, ambao walikasirika sana na kumshinikiza aachane na kibibi kile.
Je hapa tunajifunza nini? Kwanza, ughaibuni kuna mila chafu ya wazee ‘kushobokea’ vijana japo hii imeanza kujitokeza kwenye nchi za Kiafrika kutokana na kuigiza usasa usio usasa bali ushenzi.
Pili, kuna ubinafsi na uhuru wa kupita kiasi. Tatu, kuna unyanyasaji na unyonyaji kimapenzi vinavyotokana na ubaguzi ambapo mtu mweupe, siku zote, ni bora na mkombozi wa mtu mweusi.
Nne, mfumo wa huku usiojali maadili unachochea na kuruhusu vitu kama hivi. Kwani, kila mtu anafanya vyake bila wasi wasi wa kusutwa au kuaibika.
Mwisho, pamoja na kuwa mambo haya yameshaanza kutokea katika baadhi ya nchi, jamii inapaswa kuingilia kati na kukemea hata kuzuia ukatili na unyanyasaji wa kimapenzi unaowakumba wanaume wengi hasa wa Kiafrika.