Prime
Chunga usiolewe majuu ukidhani umeoa!

Kisa cha jamaa yetu toka tena kwetu Tanzania (mji hatutaji) kinafikirisha na kufundisha kwa wale ambao hawajaingia mkenge kama huyu bwana. Baada ya mambo kuwa magumu na kuwepo misifa mingi juu ya majuu, vijana wetu wanaolewa na wanawake wa Kizungu ili iwe passport ya kupandia majuu. Katika kisa hiki, picha hii inajitokeza kama tutakavyoidurusu.
Tupo kwenye supermarket na jamaa toka Sudani. Bila hili wala lile, anatujia mama Kizungu akiwa na watoto machotara wa Kiafrika na Kizungu. Anatusalimia kwa uchangamfu. Nasi, bila ajizi tunajibu salamu zake. Anatuuliza “nyie mnatokea Afrika?” Tunamjibu kwa bashasha “haswa.”
Mama wa Kizungu anatuuliza swali ambalo si Wazungu wengi huuliza. Anauliza “mnatoka nchi gani Afrika?” Swali lake linanishangaza na kunifikirisha. Nami nauliza “umewahi kwenda Afrika? Anajibu “ndiyo, naijua Tanzania ambako ndiko anakotokea mume wangu ambaye bahati mbaya nilimzuia kuja nasi ili akae na watoto.”
Msudani mmoja anadakia huku akionyesha kidole kwangu “huyu jamaa anatokea Tanzania.” Mama anatabasamu. Napigwa na mshangao kutokana na Wazungu wengi kudhani Afrika ni nchi moja. Hivyo, wengi hawajui kuwa Afrika ina nchi zaidi ya hamsini walizotengeneza japo sasa wanaziunganisha. Namuuliza “ni wapi unajua Tanzania?” Anajibu “Arusha, Zanzibar, na Darasalam.”
Baada ya maongezi mafupi, nawataka radhi tuondoke. Yule mama anatuaga kwa furaha akisema “kama mnaishi hapa, tutakutana tena na mtaongea na mume wangu.” Nami namjibu, “hatuishi hapa. Tunaishi mpakani na Marekani kama kilomita 40 toka hapo, japo huwa tunakuja mara nyingi hapa kununua bidhaa.”
Baada ya kuachana na yule mama, Msudani mmoja anasema “wallahi huyu mama kanifurahisha. Anaipenda Afrika.” Namkatalia. Namuuliza “umesikia alivyosema kuwa anasikitika alimzuia mumewe kuandamana nao ili akae na watoto?” Naongeza “huoni kuwa mwenzetu kaolewa?” Jamaa anastuka. Namwambia “huyu Kawajia, yaani mama wa Kizungu hafai.” Tunaachia maongezi hapo na kwenda zetu. Nilipofika nyumbani, nilimpa Nesaa kisa kizima yakaishia hapo.
Baada ya kama mwezi mmoja, tulirejea na familia kununua mahitaji kawaida. Bila hili wala lile, mwanetu mmoja anasema “naona Waafrika wale.” Kugeuka, tunamuona yule mama wa Kizungu na mumewe Mwafrika wakitujongelea. Mama wa Kizungu ananisalimia kwa bashasha. Anamwambia mumewe “ni yule jamaa niliyekwambia.” Tunapeana mikono, jambo ambalo Wazungu wengi huwa hawafanyi. Namgeukia Nesaa na kumwambia “huyu ndiyo yule mama niliyekwambia.”
Familia mbili zinachangamkiana wazazi na watoto. Mume wa Mzungu ananiuliza kwa Kiswahili fasaha na mshangao “hii ndiyo familia yako?” Namjibu “naam.” Anajibu kwa kunyong’onyea “heri wewe umekuja na mkeo.” Nilimuuliza “mwenzetu Tanzania unatokea wapi na ilikuwaje ukawa huku?” Jamaa alitaja atokako Tanzania na namna alivyokuwa akifanya kazi kwenye utalii walipokutana na mkewe wa Kizungu wakaamua kufunga ndoa.
Japo hakusema, lengo la kufanya hivyo ilikuwa ni kuukata kwa kuja majuu ambako uliishia kumkata. Japo si wote, wengi wa vijana waliojiingiza kwenye ndoa hizi huishia kuolewa na kutumikishwa mbali na kutumiwa kuzaa watoto ambao kwa nchi zenye upungufu wa watu ni mali, huyu jamaa unaweza kumuweka kwenye kundi hili. Isitoshe, si yeye tu. Wapo wengi ambao, mara nyingi, hujutia uamuzi wao pale wanapojikuta wakimilikiwa na kutumikishwa kama mashine za ngono na watumwa wa mapenzi.
Kufupisha kisa kirefu, yule bwana, pamoja na kutuchangamkia, hakuonyesha nia ya kutaka tumjue lau kutukaribisha siku moja tutembeleane. Hakutoa namba yake ya simu. Nami, kadhalika, sikutoa namba yangu ya simu. Kwa lugha ya mwili, hakuwa tayari kuwa karibu nasi. Nami nilifahamu ni kwa nini. Angependaje tuwe karibu tuone anavyoishi? Pia, tunadhani alijua tunajua waume wa namna hii wanavyoishi kama tutakavyobaini kwenye kisa kingine cha Mfilipino aliyeolewa na mama wa Kizungu.
Kwa nini tunadhani au kusema hivi? Kwanza, tumeishi huku kwa muda mrefu. Pili, tunajua mengi ambayo walioko nyumbani hawajui kuhusiana na kuula majuu. Tatu, namna jamaa alivyoonyesha kutotaka kujuana zaidi, kunasema mengi kuthibitisha haya tunayosema. Nne, tumeyaona mengi tu. Tunaandika kisa hiki kuwapa darasa wasiojua wajue watakapoamua kufunga ndoa wakitegemea kuukata lau wapate picha ya kinachowangojea.