Prime
Mume wangu kanifedhehesha, nidai talaka?

Anti habari za kazi, hongera kwa kujibu maswali yetu na kutupa ufafanuzi unaoponya. Leo nina changamoto ambayo nahisi itanipasua kifua.
Mume wangu amenihisi nina uhusiano na mwanamume, akamtafuta mke wa huyu bwana na kumueleza kuhusu hisia (kuwa natoka na huyo mwanamume kimapenzi) juu yangu.
Kibaya zaidi huyo mwanamke bila kufanya uchunguzi kaamini na wakashirikiana kuja nyumbani akiwa na jamaa zake kunilaumu kuwa mimi ni mhuni.
Mbaya zaidi wote aliokuja nao, wakiwamo jamaa zake wanaamini kweli ninatoka na huyo mwanamume aliyetajwa, ilhali kiuhalisia hakuna kitu kama hicho wala namna yoyote ya kuwa karibu naye zaidi ya kujuana kama majirani huko tunakoishi.
Huyo kijana na familia yake walikuwa wakiishi jirani na sisi kabla hawajahamia kwenye nyumba yao na watoto wetu walikuwa wakisoma shule moja. Tulijuana nao kwa kuwa mume wangu alikuwa akiwapa lifti na mkewe kwa nyakati tofauti tulipokutana nao njiani. Kwa kifupi hatujawazoea zaidi ya kusalimiana na kukutana nao kwenye masuala mbalimbali ya mtaani kama misiba na matukio mengine kama hayo.
Walipokuja hawakuwa na huyo mwanamume na nilipigwa butwaa, ilibaki kidogo haja ndogo initoke, kiasi nimefedheheka sana na sina pa kuuweka uso wangu kutokana na hili.
Kinachoniuma jamaa zake mume wangu wanaamini hilo na imekuwa kama fimbo, maana wananipiga mafumbo kila wanapopata wasaa. Ninataka nidai talaka ili niwe huru maana sioni kama ninaweza kuishi kwenye ndoa ya namna hii.
Mume wangu baada ya kubaini ninataka kuondoa ananitisha niwaache watoto wetu wawili, hilo kwa sasa si tatizo kwangu kwa sababu ninaweza kujidhuru, kila nikikumbuka ile kadhia ninachukia, ninajichukia, ninaumia na kuona karaha hata ya kuishi.
Ninachoomba kwako unishauri nianzie wapi kudai talaka na haki ya kuondoka na watoto wangu kwa sababu ni wadogo. Nimefunga ndoa ya Kiislamu, ila ninavyomjua huyu mwanamume atanisumbua sana kunipa talaka, sasa nataka niipate kisheria.
Pole sana. Mumeo alikutendea kitendo kibaya na ninakubaliana na wewe kabisa, ila natamani usiondoke ukiwa na hasira, kwani zikiisha utatamani kurudi lakini utashindwa kwa sababu uliondoka mwenyewe. Jambo la kwanza la kufanya tulia hasira zipoe kabisa, kisha ndiyo uanze taratibu za kudai hiyo talaka ambayo licha ya dini kuiruhusu kutolewa, lakini haijampendeza Mwenyezi Mungu.
Pia kabla hujafanya uamuzi wowote ya talaka wafikirie watoto namna watakavyolelewa na mumeo kwa namna unavyomfahamu, kama una mashaka na malezi yao fikiria mara mbili, kwani kudai haki hiyo kisheria uamuzi hautatoka mara moja, utachukua muda, hivyo watakuwa wanaendelea kulelewa na baba yao kwa wakati huo.
Nachelewa kukupa mbinu za pa kuanzia kudai talaka kama ulivyosema kwa sababu naamini ni mapema mno, kwanza ungeshitaki kwa wazee kuona namna unavyoweza kujitetea, licha ya kuonyesha wasiwasi kuwa jamaa wa mumeo wameungana na ndugu yao kuamini uongo wake.
Ila kwa shingo upande nakueleza ukitaka kudai talaka kama unaona mumeo hatokupa nenda kwenye ofisi za Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), popote ulipo huko huwa kuna ofisi za kadhi au wanajua zilipo watakuelekeza kisha utapeleka madai yako kuhusu talaka, haki ya watoto nenda Ustawi wa Jamii, wao watakupa mwongozo wa nini cha kufanya.
Muhimu usifanye uamuzi kwa hasira, unaweza kujilaumu baadaye, tafuta wasaa myamalize kwa amani.