Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tunahitaji makongamano ya kitaifa kujadili maadili ya Taifa

Muktasari:

  • Naona umefika wakati, na hata huenda tumechelewa, kuwa na kongamano la maadili katika Taifa letu. 

Dar es Salaam. Katika nchi yetu huwa tuna makongamano mara kwa mara kuhusu mada mbalimbali hasa zinazohusu mustakabali wa nchi. 

Hali hiyo sio tu inasaidia Taifa kimaendeleo, pia ni utekelezaji wa falsafa kwamba hatuna budi kujiendeleza siku zote kifikra na kielimu. Makongamano yanaelimisha, yanatoa maarifa mapya, yanafikirisha na kutafakarisha. 

Katika muktadha huu naona umefika wakati, na hata huenda tumechelewa, kuwa na kongamano la maadili katika Taifa letu. 

Makongamano ya aina hii yanapaswa kuwa endelevu tukizingatia kwamba hilo ndilo kongamano mama la makongamano yote. 

Bila uadilifu katika taifa, makongamano yote yatakosa misingi sahihi ya kutekeleza fikra mpya na  kuchukua uamuzi.

 Bila uadilifu katika nyanja zote za maisha yetu, tutafanana na mtu anayejenga nyumba lakini hazingatii umuhimu wa msingi wake. 


Kwa nini makongamano haya?

Tuna sababu lukuki za kuwa na makongamano ya kitaifa kuhusu maadili. Tuainishe chache hapa. 

Kuna msemo kule Ghana kwamba anguko la taifa huanza na anguko la familia zake. 

Ni wazi kwa yeyote anayefikiri kidogo tu, atabaini kwamba tuna changamoto nyingi katika familia zetu. 

Tunashuhudia wazazi wakishindwa kutekeleza wajibu wao kama wazazi na wengine kuwatelekeza watoto wao au wenzi wao. 

 Tunaona talaka zikiongezeka siku hadi siku na wanandoa wengi wakiishi bila amani nyumbani. 

Tumefikia mbali hata tunaona mauaji ya kikatili katika familia na pia unyanyasaji wa kingono, kijinsia na kiumri katika familia zetu. 

Haya ni matatizo ambayo hayakuwahi kutokea kwa kiwango hicho zama za mababu zetu.

Tunashuhudia pia matukio ya utawala mbovu nchini. Tunaona mali za wananchi zikiibiwa na kuporwa na baadhi ya wale wenye madaraka, na mbaya zaidi hatuoni kwamba wala rushwa na mafisadi wanawajibishwa kiasi cha kuridhisha. 

Tumekuwa na siasa za kugawanya watu kiitikadi, kikanda na wakati mwingine kidini. Taifa linaonekana kugawanyika.

Tunaona umaskini ukiongezeka katikati ya maendeleo makubwa ya miundombinu kama barabara za kuunganisha mikoa, ujenzi wa madaraja ya kisasa, maendeleo katika kuongeza na kuboresha vianzo vya nishati kama umeme, gesi na kadhalika. Haya yote ni maendeleo makubwa na ya kupongeza. 

Hapa tunakumbushwa na Mwalimu Julius Nyerere kwamba maendeleo ya kweli na ya msingi ni ya kujenga utu, kujenga utawala bora, kuwasaidia wote waweze kujitegemea kiuchumi na kijamii. 

Mwalimu alitoa mifano ya falme na tawala nyingi zilizopiga hatua kubwa katika ujenzi wa majengo ya ukumbusho, barabara, madaraja, na kadhalika lakini hayo yote hayakuzuia tawala kama za Kiajemi, Kirumi na nyinginezo kuanguka. Hata katika zama hizi tunashuhudia mataifa mengine makubwa yakisongwa na mmomonyoko wa maadili. 

 Yapo mataifa yenye uwezo mkubwa wa kujenga silaha za nyuklia lakini mataifa hayo yanashindwa kuelewana na mengine tunaona yapo vitani. 

Kumbe basi uwezo wetu wa sasa wa kiteknolojia haujaweza kujenga utu wetu wala kuunganisha mtu na mtu katika uhusiano wa kuridhisha. 


Maendeleo si miundombinu

 Ni jambo moja kuwa na maendeleo ya kiuchumi na kiteknolojia, na ni jambo lingine kabisa kuwa na maendeleo katika utu, heshima kati ya mtu na mtu, heshima kati ya taifa na taifa. 

Ndiyo maana Mwalimu Nyerere akatuasa kwamba maendeleo ya vitu, majengo, madaraja, barabara bila kujenga utu, haya yote yatatuangamiza.

 Kujenga madaraja iwe pia katika kujenga madaraja au uhusiano mzuri kati ya watu katika jamii yao.

Hivyo tunazo sababu nyingi za kuwa na makongamano ya kitaifa kuhusu maadili. Ikiwa kwamba tutafikia huko, na nashauri tufikie huko, tunaweza kuwa na matayarisho kama ifuatavyo:

 Jambo la kwanza: kwa nini tuwe na makongamano hayo? Jibu linapatikana hapo juu kwa kiasi cha kuridhisha. Msomaji unaweza kuongeza hizo sababu zilizoanishwa hapo juu. 

Pili: nani aanzishe au aite kongamano la kwanza? Nadhani mdau yeyote anaweza kufanya hivyo kwa kuzingatia taratibu zote za kiutu, kisheria na kiutawala katika nchi yetu. 

Kwa sasa vipo vikundi fulani vinakutana na kuzungumzia umuhimu wa kujenga maadili katika Taifa letu, na wadau kama hawa wanaweza kuanzisha kongamano la aina hiyo. 

Viongozi wowote wa Serikali, dini, mashirika yasiyo ya kiserikali na kadhalika, wanaweza kuitisha kongamano la kwanza na kuendelea. Kwa kweli mdau yeyote anayekerwa na mmomonyoko wa maadili hapa nchini kwetu na duniani, anaweza kuitisha kongamano la kwanza.

  Ni kina nani waalikwe katika kongamano hilo la kwanza? Hapa waitwe kwanza wawakilishi kutoka serikalini kama mawaziri, makatibu wakuu wa wizara na kadhalika. 

Ni muhumu Serikali ikahusishwa barabara, na ikasaidia kwa kiasi kikubwa katika kongamano kama hilo. 

Ni busara kwamba itikadi za aina yoyote za kisiasa zisiingilie kongamano kama hilo.

 Ni muhimu kwamba kongamano hilo na yote yatakayofuata yasitekwe na itikadi za kisiasa, imani za kidini, kikanda, kikabila, na kadhalika. 

Sisi binadamu tuna utajiri mmoja wa msingi sana: tuna falsafa za msingi zinazounganisha ubinadamu wetu.

Falsafa hizo ni  kama vile kuamini kwamba binadamu wote ni sawa, hata kama hatukosi ubaguzi hapa na pale. Falsafa zote za mataifa mbalimbali zinaamini kwamba heshima kati ya mtu na mtu ni msingi mkuu maishani; wengi tunaamini kwamba  binadamu ana uhuru wa kuongea na kutoa mawazo yake ilimradi afuate sheria, kanuni na taratibu za jamii yake

Tunaamini kwamba ni wajibu wa wazazi kuwajibika kwa watoto wao, na kadhalika. 

Hizi na nyingine ni falsafa za msingi katika mataifa yote na enzi zote. Hizi ndizo falsafa za msingi zitakazoongoza kongamano la aina hii. 

Wengine waanaopaswa kualikwa ni viongozi wa dini au wawakilishi wao. Ningependekeza hapa wawakilishi hao wawe ni wasomi wazuri katika taaluma ya kitheolojia na waliobobea katika maarifa mbalimbali.

 Waalikwe viongozi wanaoelewa vizuri busara ya msomi Thomas Aquinas wa karne ya 12 aliyeamini kwamba katika imani ya dini, ni lazima pia mtu aongeze akili, tafakari na tafakuri (the importance of faith and reason in religion). 

 Pia waalikwe wawakilishi kutoka vyuo vikuu mbalimbali na mashirika mbalimbali ya kijamii.

Lengo la kongamanio kama hili la kwanza liwe ni kusikia mawazo ya wadau wote, na kuwaalika wapendekeze hatua zinazofuata.


Prof. Raymond S. Mosha

(255) 769 417 886; [email protected]