Prime
Hii hapa misingi ya elimu iliyo bora

Muktasari:
- Wahitimu wengi wa zama hizi hudhani kwamba sasa wana shahada ya chuo kikuu hivyo wao ni wasomi.
Arusha. Mara kadhaa wasomaji wengine wamenipigia simu na kuniuliza maswali kama: Nini maana ya elimu? Kuna tofauti gani kati ya maarifa, elimu na busara? Mwingine akauliza: ni vipi vianzo vya elimu?
Haya pamoja na mengine kama hayo ni maswali mazuri. Inaonyesha kwamba wapo wasomaji wanaotafakari vizuri na walio na mawazo mazuri ambayo yananipa nafasi ya kupanua mawazo yangu.
Wananifanya nizidi kuamini kwamba mwalimu asipoulizwa maswali darasani, basi ajue kwamba hajafundisha vizuri. Au atambue kwamba ufundishaji wake siku hiyo haujafanikiwa kuchokoza akili za wanafunzi wake kiasi cha wao kuuliza maswali.
Tena hili linanikumbusha ukweli mwingine ambao viongozi wengi, hasa wa kisiasa wanausahau au wanauogopa.
Anakuja kiongozi, anawazungumzia wana habari (press conference), au wananchi, kisha anaondoka bila kuwapa nafasi ya kuuliza maswali.
Huo si utawala bora. Kiongozi bora hukaribisha maswali, huhimiza wasikilizaji wake waulize maswali. Yu- tayari kukosolewa, yu- tayari kupewa upeo wa mawazo ambayo hana.
Hoja ya leo
Hivyo turudi kwa hoja kuu ya leo: tuanze na maana ya elimu. Kamusi ya Kiswahili Sanifu inasema: elimu ni mfumo wa mafunzo yanayopatikana shuleni, vyuoni, maishani, pia ni taaluma.
Inaongeza: taaluma ni elimu inayopatikana kwa kusoma. Pia inaeleza: maarifa ni elimu, ujuzi, hekima.
Kamusi hii imesema vizuri: elimu ni mafunzo yanayopatikana shuleni, vyuoni na maishani. Hii ina maana kwamba shule si chanzo pekee cha elimu.
Ni kweli kwamba mtu anaweza kupata elimu nzuri shuleni, chuoni au katika shule ya ufundi maalum.
Ni sahihi pia kusema kwamba mtu anaweza kupata elimu au maarifa au ujuzi kutokana na uzoefu wa kile alichokifanya, alichokipitia au alinachokifanya mara kwa mara.
Kwa maneno mengine: elimu au maarifa hupatikana shuleni na pia nje ya shule. Kwa uzoefu wangu naona kwamba elimu ya shuleni haitoshi kumpa mtu maarifa na hekima ya kutosha ili aishi vizuri katika familia, jamii au taifa lake.
Elimu ya shuleni, hasa ya kinadharia (theoretical knowledge) inapaswa ijaribiwe katika chungu cha maisha, katika uwanja wa uzoefu wa maisha ya kila siku.

Ndiyo maana mtu anayeomba kazi anatakiwa aeleze ana uzoefu kiasi gani wa hicho anachoomba kukifanya.
Mtu anaomba kufundisha shule fulani, anaambiwa aeleze uzoefu wake wa ujifunzaji na ufundishaji. Hapa wanataka kujua uzoefu wake. Lakini huenda hawa wanaouliza uzoefu wa mwombaji wanasahau kwamba uzoefu sharti uanze pale mtu apatapo fursa ya kufanya jambo fulani.
Warumi wa zamani walisema katika Kilatini: fabricando fit faber. Yaani, mtu huwa seremala kwa kufanya kazi ya kiseremala. Ni lazima afanye kazi hiyo na polepole anakuwa mbobezi katika kazi hiyo.
Ni hapa tunaona kwamba uzoefu wa kufanya jambo fulani humpa mtu elimu na maarifa makubwa. Inawezekana pia kwamba mtu hajasoma shuleni lakini polepole akajifunza jambo fulani au ufundi fulani hadi kufikia ubobezi wa kutukuka.
Mtu hajaenda shule lakini ni fundi mkubwa katika kukarabati gari, au mashine nyingine. Wapo mafundi mtaani hawajaenda shule ya ufundi wowote lakini ni wabobezi katika lile wanalolifanya.
Wapo mafundi wengi huku mitaani kwetu waliohitimu darasa la saba, wanaishi vizuri kutokana na ujuzi wao, ilhali wapo wahitimu wa chuo kikuu hawana ajira na hawana ujuzi wa kuweza kuajiriwa.
Lakini hebu fikiria mtu aliyehitimu chuo kikuu na kupata shahada ya kilimo ni jinsi gani huyu atakavyoweza kuwa mkulima mzuri.
Hivyo hatubezi elimu ya shuleni lakini tunaona kwamba elimu hiyo ni lazima ikaangwe katika chungu cha maisha ya kila siku ili itoe matunda stahiki.
Waingereza wanasema: experience is the best teacher, yaani, uzoefu ni mwalimu mzuri sana.
Msomi ni nani?
Katika maelezo haya, msomi ni nani? Kwa uzoefu wangu naona kwamba msomi ni yule aliyepata elimu au maarifa kiasi fulani shuleni kisha akajiongeza kwa kuendelea kusoma, kujifunza, kufikiri, kutafakari na kupenda kujishughulisha katika mijadala na watu wengine wa aina yake na hasa wanaomzidi kielimu na kiuzoefu. Kuhitimu tu chuo kikuu hakumfanyi mhitimu kuwa msomi.
Msomi anatambua mambo haya: kwanza: elimu ni bahari, elimu haina mwisho. Akitambua hilo, na akalitekeleza, huyu ni msomi.
Pili, msomi anatambua fika kwamba kile anachokijua ni kiasi kidogo sana kulinganisha ni kile asichokijua. Yaani ni kama kusema: anatambua kwamba anachokijua ni kama asilimia moja ya maarifa na elimu iliyo duniani. Tuliseme hili kwa Kiingereza: a learned person realizes that what she or he knows is a very small fraction of what is there to be known. Mtu anapotambua hili, ataona lazima ya kuendelea kusoma, kujisomea, kufikiri, kutafakari, kufanya utafiti na kadhalika. Huyu ni msomi.
Katika kuandika makala hizi gazetini nimejifunza kwamba wale wanaozifuatilia mara kwa mara ni wasomi wazuri.
Wengi wao ni wale waliosoma zamani, ambao wanatambua kwamba elimu ni bahari. Hawa ni wasomi wanaopenda kufikiri, kutafakari na kuuliza maswali, bila kujali walisoma shuleni hadi ngazi gani.
Wazo langu elimu ya sasa
Hapa ndipo naona inafaa nitoe wazo kuhusu elimu itolewayo sasa. Wahitimu wengi wa zama hizi hudhani kwamba sasa wana shahada ya chuo kikuu hivyo wao ni wasomi.
Si kweli. Wamehitimu chuo kikuu lakini wao si wasomi. Watakuwa wasomi pale watakapotambua kwamba elimu ni bahari na kisha wakajiongeza kwa kuendelea kujifunza, kusoma, kufikiri na kutafakari.
Msomi atakuwa msomi kweli pale atakapotambua maana ya maneno haya ya mwanafalsafa wa Kiyunani, Plato, (428-348 B.C.), aliyesema:
‘’Jambo lolote lile la maana katika maisha ni lazima likolezwe na uadilifu.’’ Msomi anayetuibia hela za umma si msomi, ni mwizi tu kama wezi wengine.
Msomi asiyetusikiliza sisi wananchi si msomi, ni dikteta tu kama vile Hitler na wengineo.
Hivyo tuhitimishe kwa kusema kwamba misingi ya elimu ni pamoja na shule, vyuo, uzoefu katika maisha na katika jambo fulani, elimu endelevu, kufikiri na kutafakari daima, kufanya tafiti, kusikiliza mawazo ya wengine hasa yaliyo tafauti na yetu, na hasa kuishi katika uadilifu ambao ni sifa kuu ya mtu msomi.
Prof. Raymond S. Mosha
(255) 769 417 886; [email protected]