Tanzania yajipanga kuanzisha mfumo shirikishi sekta ya elimu

Muktasari:
- Tanzania inatarajia kuanzisha mfumo shirikishi wa tafiti za elimu wenye lengo la kuboresha viwango vya ufundishaji, ujifunzaji na usimamizi wa takwimu katika sekta ya elimu.
Dar es Salaam. Tanzania inatarajia kuanzisha mfumo mmoja shirikishi wa kuandaa, kuratibu na kuchambua tafiti za elimu, ikiwa ni hatua ya kuimarisha sekta hiyo kwa kutumia ushahidi wa kisayansi katika kufanya maamuzi na kupanga sera.
Lengo kuu la mfumo huo ni kuhakikisha kuwa matokeo ya tafiti mbalimbali zinazofanyika katika sekta ya elimu yanakuwa na mchango wa moja kwa moja katika kuboresha ufundishaji, ujifunzaji, na usimamizi wa elimu kwa wadau wote, wakiwemo watunga sera, taasisi za elimu, na jamii kwa ujumla.
Aidha, kupitia mfumo huo, Serikali imelenga kuwezesha upatikanaji rahisi wa taarifa muhimu za elimu kwa wadau wote kupitia kituo kimoja cha taarifa, hatua itakayosaidia kurahisisha mawasiliano, kupanga mikakati, na kufuatilia maendeleo ya sekta hiyo kwa ufanisi zaidi.
Kauli hiyo imetolewa leo, Mei 15, 2025 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, alipokuwa akifungua kongamano la teknolojia na elimu lililoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) na Taasisi ya Adapt IT, kupitia kongamano la Adapt IT and HESLB Technology.

Profesa Mkenda amesisitiza kuwa matumizi ya teknolojia na tafiti za kielimu ni mihimili muhimu katika mageuzi ya elimu na kwamba ushirikiano baina ya taasisi za umma na sekta binafsi utaharakisha utekelezaji wa dira ya elimu ya taifa.
Kongamano hili limefanyika leo jijini Dar es Salaam likiwa na lengo la kujadili mchango wa teknolojia katika kuimarisha usimamizi wa taarifa, uchambuzi wa takwimu na uzingatiaji wa kanuni katika vyuo vya elimu ya juu na kati nchini.
Akizungumza katika kongamano hilo, Profesa Mkenda amesema kuwa tayari kamati ya wataalamu iliyopewa jukumu la kupitia mifumo ya sasa na kuandaa mapendekezo ya uboreshaji wa mfumo wa takwimu za elimu, ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha kazi hiyo.
Profesa Mkenda ameeleza kuwa mfumo mpya unaotarajiwa kujengwa utahakikisha takwimu zote muhimu za sekta ya elimu zinapatikana kupitia kituo kimoja cha taarifa, hivyo kurahisisha uchambuzi na upatikanaji wa taarifa kwa wadau wa elimu na watunga sera.
“Mfumo huu utakuwa jumuishi na utaunganisha taarifa kutoka katika mifumo mbalimbali ya Serikali,” amesema Profesa Mkenda na kubainisha kuwa mifumo hiyo ni pamoja na ile ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Idara ya Uhamiaji na Ofisi ya Rais Tamisemi.
Amesisitiza kuwa mfumo huo shirikishi utaongeza uwazi na ufanisi katika ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu, jambo litakalosaidia kuboresha sera na mipango ya maendeleo ya sekta ya elimu nchini.
Katika hatua nyingine, Profesa Mkenda amesema wizara yake inajipanga kuanza kutoa Ripoti ya Mwaka ya Takwimu za Elimu (Basic Education Statistics Tanzania – BEST) ambayo itahusisha taarifa kutoka ngazi zote za elimu pamoja na shule na vyuo binafsi, ili kutoa picha halisi ya hali ya elimu nchini kwa mwaka husika.
Amesema ripoti hiyo itakuwa chombo muhimu cha kusaidia wadau wa elimu, wakiwemo wachambuzi wa sera, wahadhiri, na taasisi za kimataifa, katika kupanga na kufuatilia maendeleo ya elimu kwa usahihi na uwazi.
“Timu ya maandalizi ya mfumo mmoja imenieleza kuwa wapo katika hatua za mwisho. Hivyo, tutakuwa na mfumo mmoja utakaobeba taarifa zote za mwanafunzi kuanzia ngazi ya chini hadi za juu. Tunahitaji pia kuwa na takwimu zote muhimu za sekta ya elimu kwenye mfumo mmoja,” amesema Waziri Mkenda.
Amesisitiza kuwa mfumo huo utawezesha kutambua wanafunzi wote, idadi yao na hatua wanazopitia katika masomo yao, pamoja na wale wanaoshindwa kuendelea na masomo.
“Kupitia mfumo huu, tutamtambua kila mwanafunzi kwa umri na hatua anayopitia. Hata vyuo vikuu, tunataka tuwe na uwezo wa kujua idadi ya wanafunzi katika programu fulani na idadi ya wanaoshindwa kuendelea, ili tuweze kutambua sababu,” amesema.
Profesa Mkenda ameongeza kuwa mfumo huo utawezesha kutambua shule ambazo wanafunzi wanaziacha kwa kiwango kikubwa na kuchanganua sababu zinazochangia hali hiyo.
“Lengo letu ni kuwa na mfumo utakaohusisha taarifa za elimu kutoka ngazi zote katika sehemu moja. Tutaendelea kujifunza kutoka kwa wengine, lakini tunataka kujenga mifumo yetu wenyewe kwa gharama stahiki, badala ya kutumia fedha ambazo zingetumika kwa shughuli nyingine muhimu katika sekta,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), Dk Bill Kiwia amesema kuwa mkutano huo umelenga kuonyesha umuhimu wa teknolojia katika kuboresha utoaji wa huduma bora katika sekta ya elimu.
"Kupitia mkutano huu, tutajadili changamoto ambazo wenzetu wa Adapt IT, ambao wana uzoefu mkubwa wa teknolojia, wamekumbana nazo. Pia, tupo na wataalamu wa fedha na wakuu wa vyuo, ambapo tutajadili na kutoa mapendekezo ya kuboresha huduma zetu kupitia mifumo ya kidijitali," amesema Dk Kiwia.
Ameongeza kuwa lengo kuu la mifumo hiyo ni kusaidia upatikanaji wa huduma bora kwa wanafunzi na kupunguza gharama kwa Serikali.
Dk Kiwia amesema kwamba mifumo ya Tehama inayotumika katika HESLB ni ya ndani, na tayari Waziri wa Elimu ametoa maagizo kwa wataalamu wa ndani kushughulikia changamoto za mifumo ya Tehama ya elimu.

“HESLB tumekuwa tukijenga mifumo yetu ya ndani kwa kutumia wataalamu wetu wa ndani, kwani hili ndilo lengo la serikali la kuhakikisha mifumo yetu inaendana. Katika sekta ya elimu, mifumo yetu pia inaenda kusomana kutokana na hatua zinazochukuliwa,” amesema Dk Kiwia.