Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mikopo ya elimu ya juu yaongezeka

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2025 / 2026 jijini Dodoma leo Mei 12, 2025. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Ameliomba Bunge kuidhinishia Sh2.4 trilioni kwa mwaka 2025/26 huku Sh1.74 trilioni zikienda katika miradi ya maendeleo.

Dodoma. Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imewasilisha vipaumbele vitano itakavyotekeleza katika mwaka wa fedha wa  2025/2026,  huku idadi ya wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu ikitarajiwa kuongezeka kutoka 245,314 mwaka 2024/2025 hadi wanafunzi 252,773 mwaka ujao wa fedha.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ameyasema hayo leo Jumatatu Mei 12,2025 wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2025/26.

Ameliomba Bunge kuidhinishia Sh2.4 trilioni kwa mwaka 2025/26 huku Sh1.74 trilioni zikienda katika miradi ya maendeleo.

Katika mwaka 2024/25, Bunge liliidhinishia wizara hiyo bajeti ya Sh1.97 trilioni huku miradi ya maendeleo ikitengewa Sh1.32 trilioni.

Akiwasilisha bajeti hiyo, Profesa Mkenda amesema kati ya wanafunzi hao 252,773, 88,320 ni wa mwaka wa kwanza na wanaoendelea ni 164,453.

Aidha, Profesa Mkenda amesema Serikali itaendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi 10,000 wa ngazi ya stashahada katika fani 86 za kipaumbele kama sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati.

Amesema katika mwaka2025/2026, wataendelea kutoa ufadhili kwa wanafunzi 2,630 wenye ufaulu wa juu katika masomo ya sayansi kupitia  ufadhili wa Rais Samia, ambapo kati ya hao wanafunzi wa mwaka wa kwanza ni  1,220, shahada za umahiri 80 na wanafunzi wanaoendelea 1,330.

Pia amesema wizara itaendelea kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 50 wenye ufaulu wa juu katika masomo ya sayansi hususan wanafunzi wa kike waliohitimu mitihani ya kitaifa ya kidato cha sita na shahada za awali kupitia Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM).

 “Serikali itaendelea kuimarisha ukusanyaji wa mikopo iliyoiva yenye thamani ya Sh210.2 bilioni kutoka sekta za umma, binafsi na zisizo rasmi kwa kuwatambua wanufaika wapya 40,000,”amesema.

Amesema watafanya ukaguzi kwa waajiri 8,000 kuhusu umuhimu wa utii wa Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu.

Bodi ya kitaaluma ya walimu kuanza kazi

Profesa Mkenda amesema Serikali itaanza utekelezaji na uendeshaji wa Bodi ya Kitaalamu ya Walimu.

Amesema lengo ni kuhakikisha walimu wanaohitimu katika vyuo vinavyotoa mafunzo ya elimu ya ualimu vinavyotambulika na Serikali, wanapata usajili utakaowawezesha kutambulika ndani na nje ya nchi pamoja na kuendeleza utaalamu wao.

Aidha, amesema bodi itawezesha usajili na uendelezaji wa walimu wote walioajiriwa katika shule za Serikali na zisizo za Serikali.


Vipaumbele vitano vya bajeti

Profesa Mkenda amevitaja vipaumbele vya mwaka 2025/26 ni kuendelea na utekelezaji wa sera na mitalaa, mapitio ya sheria na kuandaa miongozo ya utoaji wa elimu na mafunzo.

Vingine ni kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa mafunzo ya amali katika shule za sekondari na vyuo vya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi na  kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya awali, msingi, sekondari na ualimu.

Ametaja vipaumbele vingine ni kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya juu na kuimarisha uwezo wa nchi katika utafiti, matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuchangia upatikanaji wa maendeleo endelevu.

Amesema juhudi zaidi zitatumika kupeleka vijana wa Kitanzania kusomea mambo ya sayansi ya nyuklia, mambo ya kompyuta na akili-unde kwenye vyuo bora vilivyo nje ya nchi.

Kuhusu elimu ya amali, Profesa Mkenda amesema Serikali itaimarisha utoaji wa elimu ya amali katika shule za sekondari nchini, huku ikitarajia kupanua shule 55 za sekondari kuwa za amali.

Kwa upande wa wasichana walioacha shule kwa sababu mbalimbali, Profesa Mkenda amesema watawawezesha wasichana 3,000 walioacha shule kutokana na sababu mbalimbali kupata elimu ya sekondari kwa njia mbadala.

Pia amesema Serikali itafanya utafiti wa kitaifa kuhusu hali ya kisomo na elimu kwa umma utakaoboresha utekelezaji wa mkakati wa kisomo na elimu kwa umma.


Sheria kufanyiwa mapitio

Profesa Mkenda amesema Serikali itakamilisha mapitio ya Sheria ya Elimu, Sura 353 ili iendane na matakwa ya Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023.

Pia amesema watakamilisha mapitio ya sheria katika taasisi ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia, Bodi ya Huduma ya Maktaba na Baraza la Taifa la Mitihani.

Mapitio mengine ni ya Sheria za Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Tanzania, Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania, Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Taasisi ya Elimu Tanzania na Mamlaka ya Elimu Tanzania.

Amesema madhumuni ni ili kuendana na sera pamoja na mikataba ya makubaliano ya kikanda na kimataifa.

Kuhusu utafiti, Profesa Mkenda amesema Serikali imeendelea na utekelezaji wa mradi wa kufundisha wanyama (APOPO) hususan panyabuku kupitia Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo ambapo panya 100 wamefundishwa na kufuzu.

Amesema panya hao wamepelekwa Angola (13), Azerbaijan (11), Cambodia (58) na Ethiopia sita (6) kwa ajili kutambua mabomu yaliyotegwa ardhini pamoja na utambuzi wa vimelea vya kifua kikuu.

Aidha, Profesa Mkenda amesema panya 12 wamepelekwa nchini Marekani kama panya wa maonesho kwenye shamba la wanyama.


Michango ya kamati, wabunge

Akiwasilisha maoni kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Husna Sekiboko amesema kamati ilishauri kuwa vigezo vya utoaji wa mikopo ya elimu ya Juu vifanyiwe mapitio, lengo ni kuwa na vigezo visivyosababisha malalamiko na vyenye tija katika azma ya Taifa.

Amesema majibu ya Serikali yameonesha kuwa ushauri huu umezingatiwa kwa kiasi kikubwa, kufikia hatua ya kusubiri maoni ya wadau.

“Taarifa ilionesha kuwa Serikali imekamilisha  mapitio ya muundo na utendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu,”amesema.

Aidha, Husna amesema Serikali imeboresha vigezo vya utoaji wa mikopo ambavyo vitaanza kutumika kuanzia mwaka wa Fedha 2025/2026 baada ya kuridhiwa na wadau.

“Hatua ya Serikali kusikiliza na kuzingatia ushauri unaotolewa bungeni inastahili kupongezwa. Ni hatua ambayo inafanikisha lengo la Serikali kuwezesha ustawi wa watu kwa kuzingatia ushauri wa wananchi kupitia kwa wawakilishi wao,”amesema.

Akichangia makadirio hayo, Mbunge wa Kuteuliwa (CCM) Vuai Ali Nahodha amesema upo msongamano mkubwa wa wanafunzi na kuwa kwa uzoefu wake,  hakuna mwanataaluma ambaye anaweza kufundisha darasa lenye watu zaidi ya 50,

“Ili kukabiliana na msongamano,  wanafunzi wagawanwe katika makundi mawili, kundi la kwanza la wanafunzi wa kuanzia darasa la kwanza la pili na tatu waingie darasani kwa utaratibu wa kawaida kuanzia saa 1.00 asubuhi na wale darasa la nne hadi la sita wawekwe katika ukumbi mkubwa wa mikutano,”amesema.

Vuai amesema kwa mtindo wa kubadilishana, wanafunzi hao wakiwa katika ukumbi mkubwa waonyeshwe filamu mbalimbali za kujifunza Kiingereza, sayansi , midahalo, wafanye majadiliano na mashindano ya ubunifu.

Aidha, ametaja kasoro nyingine katika mfumo wa elimu ni watoto kupewa kazi nyingi za nyumbani mara baada ya kumaliza muda wa kusoma shuleni na kushauri wapunguziwe kazi.

“Sayansi ya makuzi ya mtoto inasema kuwa watoto chini ya miaka 15, ubongo wake unakuwa dhaifu sana kubeba mambo, kusoma mambo mengi kwa wakati mmoja, unataka kutunzwa na kulelewa kwa umakini wa hali ya juu sana,”amesema Vuai ambaye kitaaluma ni mwalimu.

Naye Mbunge wa Kuteuliwa, (CCM), Profesa Shukrani Manya ameshauri walimu wanaofundisha mtalaa mpya wa elimu,  wasiwe walimu ambao hawakupewa mafunzo vizuri ili Taifa liweze kuzalisha wahitimu bora.

“Walimu watakaofundisha mtalaa mpya wasiwe walimu ambao hawakufunzwa vizuri. Wakiwa ni wale waliotokana mtalaa wa zamanim wapewe mafunzo kidogo tu  ili watapeleka ujuzi wao wa zamani katika mtalaa mpya,”amesema.

Profesa Manya ametaka walimu wapewe mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu kwa kuzingatia teknolojia ya sasa ambapo wakishaiva watatoa wahitimu bora.

“Ili jambo la kujifunza teknolojia za zamani inawezekana pia ndio shida inayopatikana katika vyuo vyetu vikuu kwa sababu tuna maabara za zamani,”amesema.