Wahitimu wetu wana mawazo mbadala?

Muktasari:
- Hatuwezi kuleta maendeleo katika nchi yetu ikiwa tutaendelea kukumbatia mawazo yale yale yaliyotufikisha katika umaskini huu wa kutegemea wengine.
Katika nchi yetu jitihada za kuboresha mfumo wa elimu zinaendelea na wengi wetu tunatoa maoni yetu kwa njia mbalimbali.
Ni sahihi kwamba tumeanza kufanya mabadiliko kiasi fulani na hii ni hatua nzuri.
Leo nataka kufanya tafakuri kuhusu uwezo wa wahitimu wetu kutambua na kuheshimu mawazo tofauti ya watu wengine.
Je, wahitimu wetu wanathamini mawazo mbadala? Je, watumishi wa umma wa ngazi zote, na ambao ni wahitimu wa elimu mbovu tuliyo nayo, wanaheshimu na kuthamini mawazo tofauti?
Ninachokiona ni kwamba mfumo wetu wa elimu ulivyo sasa unamfanya mhitimu awe mjinga kuliko alivyokuwa kabla ya kuingia shuleni.
Ni mfumo ambao hufisha uhuru wa kufikiri tuliozaliwa nao na kutufanya tusione ulimwengu kwa mapana yake na kina chake. Ni elimu inayoua ubunifu. Ni elimu hatarishi.
Mfumo wetu wa elimu huwafanya wanafunzi kuwa wabinafsi pale wanaposhindana darasani ni nani wa kwanza kimasomo, nani wa pili, ni nani wa mwisho.
Hawapati nafasi ya kusikiliza na kuheshimu mawazo ya wenzao, hasa mawazo tofauti.
Hebu msomaji jiulize: je, elimu uliyopata ilisisitiza kwamba ni busara kusikiliza na kuheshimu mawazo yanayopingana na yako?
Je, kuna mwalimu aliyekuambia kwamba bila mawazo mbadala huwezi kupata maendeleo chanya ya kiutu, kielimu, kijamii na kiuchumi?
Je, shuleni ulifundishwa kwamba mtu yeyote yule na hasa kiongozi, hawezi kuleta maendeleo ya maana katika jamii yake kama yeye mwenyewe hajabadili mawazo yake?
Hii ni busara ya Nelson Mandela aliyesema: "Kamwe mtu huwezi kuwa na uzito wa kiungozi katika jamii kama wewe mwenyewe hujabadilika."
Dunia yetu kwa sasa ina matatizo makubwa ambayo hatuyaoni katika historia.
Ni matatizo ya sasa, hayakuwepo zama za mababu zetu. Mabadiliko ya tabianchi ni mojawapo ya hatari kubwa ya maangamizi yaliyo mbele yetu.
Tunashuhudia mafuriko makubwa yaletwayo na joto kuongezeka duniani kutokana na viwanda vyetu na shughuli nyingi tunazoziita za maendeleo ya uchumi.
Tunashuhudia misitu mingi duniani ikiungua moto kuliko ilivyo kawaida. Tunaona ukame na janga la njaa katika nchi nyingi. Kwa kiasi kikubwa changamoto hizi hazikuwepo hapo zamani.
Tunaona ulimwenguni ongezeko la watu wengi kuzama katika umaskini kila kuchapo, na wachache wakijinyakulia utajiri unaofanana na kufuru.
Nilipokuwa mtoto kijijini miaka 70 iliyopita sikuona umaskini wa aina hii. Kila mtu alifanya kazi. Kila mtu alizalisha mali, kuanzia watoto wa umri mdogo hadi wazee.
Hawakuwepo ombaomba barabarani. Hawakuwepo panya rodi. Watu walifanya kazi.
Nyerere alipokuja na kauli mbiu: “Uhuru na Kazi” alitamka ukweli ambao wananchi wa zama hizo waliuelewa.
Tunaona ongezeko la watawala madikteta duniani. Tunaona watu wakikimbia nchi zao kutafuta amani na uchumi bora katika nchi nyingine. Nchi zao hazikaliki.
Hebu msomaji fikiria uchungu na maumivu ya familia ya baba na mama na watoto wakichukua nguo zao, godoro au mkeka, na chochote wanachoweza kubeba, wanakimbilia kusikojulikana, wakiamini wataokoa maisha yao huko waendako.
Au labda akili na roho zetu zimefikia mahali hatuna uwezo wa kuona adha hizi wanazozipitia wenzetu? Elimu tuliyopata imetusaidiaje kuzuia changamoto hizi?
Mtaalamu wa elimu, H.G. Wells ameandika: “Historia ya binadamu ni mashindano katika ya elimu na maangamizi.”
Katika mbio hizo, elimu ikishinda, wote tutakuwa salama. Elimu isipokuwa bora maangamizi yatafuata.
Huu ni ukweli tunaouna sasa hivi. Changamoto tulizoziona hapo juu zinaashiria upungufu katika mfumo wa elimu.
Ni sehemu ipi katika elimu tuliyoipata ilitusaidia kuona maana ya watu kuwapenda na kuwajali wengine, hivyo kwamba tukaelewa fika kwamba mmoja wetu akishinda wote tumeshinda na mmoja wetu akishindwa wote tumeshindwa?
Ni kipengele kipi katika elimu tuliyoipata ilitusaidia tutambue, tuainishe na tuendeleze vipaji vyetu?
Mtaalamu mwingine wa elimu, Ken Robinson anauliza: "Je shule zinaua ubunifu? Nami naongeza swali hili: je, elimu yetu inatufanya tutambue uzito wa maneno ya mwanafalsafa Soren Kierkegaard wa Denmark aliyesema: "Kuna aina mbili za ujinga: kwanza kukubali uongo na upotoshaji, na pili kukataa kukubali ukweli."
Hebu tujiulize: ni kipengele kipi katika elimu tuliyoipata imetuonya kwamba kila mmoja wetu anaihitaji jamii, na kila jamii inahitaji vipaji vya kila mmoja?
Je, tumefundishwa na kujadili shuleni, msingi, sekondari na vyuoni, ukweli kwamba kutambua na kuheshimu utu wetu na wa wenzetu ni wa msingi katika kuishi hapa duniani?
Tujiulize
Tujiulize hoja ya Mwalimu Nyerere ya “Ujamaa na Kujitegemea” tumeizungumzia shuleni? Nchi yetu kweli inajitegemea?
Je, tumelizungumzia shuleni “Azimio la Arusha”? Kwa nini kipengele hiki kisiwe katika mfumo wetu wa elimu?
Kwa nini katika vyuo vyetu tusiwe na mijadala ya nguvu kuhusu nchi yetu kujitegemea?
Kwa nini elimu yetu isituamshe tukaachana na mawazo mgando ya kutegemea mataifa mengine tunaowaita wahisani na wadau wa maendeleo yetu? Kwa nini bajeti yetu inaingiza ndani ombaomba kutoka mataifa mengine?
Hatuoni kwamba tunaowaita wawekezaji wanachota hapa kwetu utajiri mkubwa ili hali sisi tunaendelea kuomba misaada na mikopo kutoka kwao?
Hili kweli linaingia akilini? Je, hili tumelizungumzia katika elimu tuliyopata wewe na mimi?
Je, sasa hivi watoto wetu shuleni wanalizungumzia hili? Wahitimu wangapi wa vyuo vikuu wamefanya utafiti katika hili? Wataalamu wetu wa uchumi watuambie tutaendelea kuwategemea wahisani hadi lini?
Tafakari yangu juu ya haya niliyoyataja hapo juu inanionyesha kwamba elimu tuliyopata na tunayoitoa sasa bado ina upungufu mkubwa unaotugharimu maisha yetu.
Ni elimu inayomuona mwalimu kwamba anaelewa kila kitu na mwanafunzi hajui chochote.
Wajibu wa mwanafunzi ni kukariri anachofundishwa na kukieleza kama kilivyo katika mitihani.
Katika mfumo huu wa elimu mwanafunzi anakuwa mtumwa, na uhuru wake wa kufikiri hufifishwa. Elimu haimweki huru.
Tunatamani mfumo wa elimu ambao unampa mhitimu unyenyekevu wa kutambua, kuheshimu na kuthamini mawazo mbadala, mawazo tofauti. Tunatamani kuona wahitimu wanaokumbatia mabadiliko ya mawazo kama ndiyo msingi wa hakika wa kupata maendeleo.
Hatuwezi kuleta maendeleo katika nchi yetu ikiwa tutaendelea kukumbatia mawazo yale yale yaliyotufikisha katika umaskini huu wa kutegemea wengine.