Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ongezeko vyuo vikuu lizingatie ubora

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, kwa mara nyingine ameweka bayana aina ya uendeshaji wa taasisi za elimu ya juu unaostahiki na anaoutarajia kwa mazingira ya dunia ya sasa, akiwa ndiye msimamizi mkuu wa sekta ya elimu nchini.

Akizungumza katika mkutano wa mtandao wa wathibiti ubora wa elimu ya juu barani Afrika (AfriQAN) uliolenga kujadili mchango wa wathibiti ubora wa elimu ya juu katika dunia ya kidijitali jijini Dar es Salaam, Profesa Mkenda alisema hatarajii kuona elimu ya juu ikiendeshwa kwa msukumo wa kibiashara zaidi.

Alisema haikubaliki kuona chuo kikishusha alama za ufaulu kwa sababu tu kinataka ada za wanafunzi au kuendelea na kuwa na wanafunzi hata kama hawana uwezo wa kumudu masomo ya elimu ya juu.

Hii si mara ya kwanza kwa Profesa Mkenda kuonyesha shaka juu ya mwenendo wa utoaji elimu katika vyuo vya elimu ya juu.

Kwa mfano, Desemba 12, 2022 alinukuliwa na vyombo vya habari akitaka GPA kubwa isiwe kigezo pekee cha mtu kuajiriwa kama mhadhiri chuoni. Alitaka wahusika wapimwe weledi na umahiri wao kwa kufanya usaili.

Kwa muda mrefu, utaratibu wa vyuo vingi nchini umekuwa ni ule wa kuwabakisha wanafunzi wanaopata alama kubwa, hasa GPA ya alama 4 kwenda juu, sifa nyingine za haiba na uwezo wa ufundishaji, mawasiliano na nyinginezo za kiukufunzi zilikuwa hazizingatiwi.

Tangu kuanza kwa ongezeko la vyuo vikuu vipya na hata wimbi la kubadili vyuo vya kada ya kati kuwa vyuo vikuu, tumeshuhudia maendeleo makubwa katika elimu ya juu, hasa upande wa idadi ya wanufaika. Hivi sasa Tanzania inajivunia kuwa na taasisi za elimu ya juu 47 zenye wanafunzi zaidi ya 206,000.

Hata hivyo, ubora wa wanufaika hao umekuwa suala linalozua mjadala mara kwa mara wadau wa elimu wanapokutana.

Uwezo wa wahitimu wengi katika vyuo umekuwa wa kutiliwa shaka, kiasi cha walio wengi kukosa sifa za kuajirika, huku wanaobahatika kupata fursa za ajira wakielezwa na waajiri kuwa hawakupikika ipasavyo vyuoni.

Pengine hiki ndicho kinachomsukuma mara kwa mara Waziri Mkenda kutaka mabadiliko katika taasisi hizi nyeti za elimu, ikiwamo ya kuhakikisha kuwa vyuo vinadahili wanafunzi kwa kuzingatia sifa ya ufaulu badala ya kila mwenye uwezo wa kifedha kuruhusiwa kusoma.

Matunda mabovu ya wahitimu si jambo la kushangaza ikiwa kuna vyuo vimelegeza mno masharti ya udahili. Lakini kama haitoshi, vipo vyuo hata mifumo yake ya utahini imekuwa ikitiliwa shaka.

Katika vyuo hivi ukianza masomo unajihakikishia kumaliza na kuhitimu hata kama mwanafunzi ana walakini mkubwa wa ujifunzaji na kukamilisha matakwa ya kitaaluma kama ufanyaji wa utafiti.

Tanzania haihitaji utitiri wa taasisi za elimu ya juu, kinachohitajika ni wahitimu hata kama ni wachache lakini wenye weledi na umahiri usiotiliwa shaka kwa vigezo vyovyote vile vya kitaaluma vya ndani na hata kimataifa.

Aina hii ya wahitimu ndio wanaotarajiwa kuivusha nchi yetu kutoka iliko sasa kuelekea katika nafasi bora zaidi ya maendeleo ya uchumi na ustawi wa wananchi wake.