Simbu aandika rekodi mpya Boston Marathon, ashika nafasi ya pili

Muktasari:
- Alphonce Simbu ameipa heshima kubwa Tanzania kwa kutwaa nafasi ya pili katika mashindano haya makubwa, akitanguliwa na Mkenya John Korir.
Dar es Salaam. Mwanariadha nyota wa Tanzania, Alphonce Simbu ameandika historia mpya katika mbio za kilomita 42 kwa kushika nafasi ya pili mbio za Boston Marathon zilizofanyika leo, Aprili 21, 2025, huko Massachusetts, Marekani.
Simbu, ambaye amekuwa akiiwakilisha Tanzania kwa mafanikio katika medani za kimataifa, alimaliza mbio hizo kwa muda wa saa 2:05:04, akitanguliwa kwa sekunde chache na Mkenya John Korir aliyeibuka kidedea kwa muda wa saa 2:04:45 ikiwa ni muda wa pili kwa kasi zaidi katika historia ya mbio hizo.

Mwanariadha John Korir
Katika mbio hizo, Simbu alionesha ushupavu wa hali ya juu, akiibuka kinara kutoka kwa kundi kubwa la wanariadha waliotabiriwa kufanya vizuri, akiwemo Cybrian Kotut wa Kenya aliyeshika nafasi ya tatu na Mmarekani Conner Mantz aliyemaliza wa nne.
Akizungumza baada ya mbio hizo, Simbu amesema kuwa alikuwa amejiandaa vizuri na anaamini bado ana nafasi ya kufanya makubwa zaidi katika mbio zijazo.
“Nashukuru Mungu kwa kunipa nguvu. Hii ni zawadi kwa Watanzania wote. Nilipambana hadi mwisho, na nafasi ya pili ni fahari kubwa kwangu na kwa taifa,” amesema Simbu.
Kwa muda sasa, Simbu amekuwa kwenye kasi ya juu, akitoka kuweka rekodi yake binafsi ya saa 2:04:38 katika Valencia Marathon mwaka jana, na sasa ameendelea kuthibitisha ubora wake katika medani ya riadha duniani.
Ushindi wa John Korir katika Boston Marathon 2025 umeendeleza utawala wa Wakenya katika mbio za masafa marefu duniani.
Mtanzania huyo amejinyakulia zawadi ya pesa taslimu kiasi cha Dola za Marekani 75,000 sawa na Sh201.4 milioni. Mshindi wa mbio hizo, John Korir, amepokea Dola za Marekani 150,000, ambazo ni sawa na takriban Sh403.2 milioni.

Mwanariadha Mkenya Sharon Loked
Katika upande wa wanawake, Mkenya Sharon Lokedi amevunja rekodi ya mbio hizo kwa kumaliza kwa muda wa saa 2:17:22, akimshinda mshindi wa mara mbili Hellen Obiri kwa sekunde 19. Lokedi alionyesha nguvu na kasi katika kilomita za mwisho, akijihakikishia ushindi wa kihistoria.
Boston Marathon ya mwaka huu ilikuwa ya 129 tangu kuanzishwa kwake, ikiwakutanisha wakimbiaji zaidi ya 32,000 kutoka nchi 118, na kuadhimisha miaka 250 ya Vita vya Mapinduzi ya Marekani.