Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanawake walia masharti magumu mikopo halmashauri

Katibu Tawala Wilaya ya Geita, Lucy Beda akizungumza kwenye kongamano la wanawake wafanyabishara wa mkoa wa Geita lililo andaliwa na TWCC likilenga kuwajengea uwezo wa kujitegemea kiuchumi.

Muktasari:

  • Wanawake wajasiriamali Geita wamelalamikia masharti magumu ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri, ikiwamo sharti la wanakikundi kutoka mtaa mmoja na muda mfupi wa mkopo. TWCC wameomba Serikali itazame upya masharti hayo.

Geita. Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Mkoa wa Geita (TWCC) wamelalamikia masharti magumu yaliyowekwa kwenye mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri na kudai hayatekelezeki kwa urahisi, hivyo kuiomba Serikali iyatazame upya.

Moja ya masharti hayo ni la kuwataka wanakikundi wanaoomba mkopo kutoka kwenye mtaa mmoja, jambo ambalo limekuwa gumu kwa wajasiriamali wanawake na vijana.

Katibu wa TWCC Mkoa wa Geita, Eveline Bwire amesema hayo leo Jumamosi, Aprili 26, wakati wa kongamano la wanawake na vijana wajasiriamali lililofanyika katika Manispaa ya Geita, likilenga kuwajengea uwezo wa kujitegemea kiuchumi.

"Licha ya Serikali kutenga asilimia 10 ya mapato kwa ajili ya wanawake, vijana na walemavu, masharti ya mikopo hiyo ni magumu kwa wajasiriamali wadogo.

“Hii inawafanya wengi washindwe kunufaika na fursa hiyo, huwezi kupata watu wenye malengo yanayofanana wanaoishi mtaa mmoja, na matokeo yake mtashindwa kufikia malengo," amesema Bwire.

Sharti jingine ambalo limekuwa kikwazo ni muda wa mkopo kuwa mwaka mmoja, jambo ambalo kwa wafanyabiashara wa kilimo inawawia vigumu kurejesha kulingana na msimu wa kilimo na kuomba sekta hiyo itazamwe kwa jicho la ziada.

Amesema changamoto nyingine inayowakwamisha ni kukosekana kwa maeneo rasmi ya biashara kwa wanawake na vijana wajasiriamali, hali inayowafanya kufanya biashara zao katika mazingira duni yasiyo rasmi.

TWCC imeiomba Serikali kuweka msukumo katika elimu ya urasimishaji biashara, hasa kwa wajasiriamali wadogo waliopo katika sekta isiyo rasmi, ili wapate faida kamili za mifumo rasmi ya kiuchumi.

Amesema sera za kitaifa za biashara bado hazijaweka utambuzi mahsusi kwa wajasiriamali wa chini, huku mfumo wa kodi, usambazaji wa bidhaa na uwepo wa mamlaka mbalimbali za kibiashara ukitajwa kama kikwazo kinachowadidimiza badala ya kuwainua.

Akizungumzia changamoto ya mikopo ya asilimia 10, Ofisa Maendeleo wa Manispaa ya Geita, Zengo Pole amesema yapo mambo ambayo yako kikanuni na kisheria, hivyo wanapaswa kuyatekeleza ili kila mmoja anufaike na fedha hizo.

"Mfano kuna jambo linalolalamikiwa sana ni hili sharti linalowataka wanaotaka mkopo wanakikundi watoke kwenye mtaa mmoja. Shida hapa ni wao kutoaminiana, lakini lengo la Serikali ni kuona fedha hizi zinawanufaisha wananchi wote, wakitoka mtaa mmoja ni rahisi hata kiongozi kuwafuatilia," amesema Pole.

Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Geita, Robert Gabriel amewataka wajasiriamali kujitambua kwa kuhakikisha wanatumia fursa za kiuchumi zilizopo, lakini akiwataka kuwa na nidhamu ya fedha za biashara na kuacha kuzitumia kwenye matumizi yasiyo sahihi.

Mwenyekiti wa TCCIA mkoani Geita, Robert Gabriel akizungumza kwenye kongamano la wanawake wafanyabishara lililoandaliwa na TWCC lwa lengo la kuwajengea uwezo wa kujitegemea kiuchumi

Amewataka wanawake kuacha kuzunguka kwenye kila kamati za harusi wakitaka kuonekana wanapesa wakati fedha hizo ni za mkopo na matokeo yake wanashindwa kurudisha na kuanza kulalamika.

"Tambueni mambo ya kupata sifa mtaani yamepitwa na wakati. Umechukua mkopo halafu kila kamati upo, harusi yenyewe haikuhusu uko bize kuchangia ili uonekane wakati hata mtaji ulionao ni wa mkopo. Acheni kutaka kuonekana, jifunze kuwekeza kwa malengo," amesema Gabriel.

Akizungumza kwenye kongamano hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Saphia Jongo amesema changamoto nyingi za ukatili wa kijinsia zinatokana na vita ya kiuchumi.

"Wanawake watavumilia kupigwa, kunyanyaswa kwa sababu huyo mwanaume ndiye tegemeo lao na mwisho wa siku mwanamke ndiye anaumizwa," amesema.

Amesema makongamano kama hayo yanayoandaliwa na TWCC ni muhimu kuwainua wanawake ili watambue wana uwezo na kuwatafutia fursa mbalimbali na kuwawezesha, ili wasimame kiuchumi kwa kuwa akisimama mwanamke kiuchumi ameinyanyua dunia.

"Kitu kinachowafanya wanawake washindwe ni kutojiamini na kujinyanyapaa. Kitu kinachotushinda ni sisi wenyewe kutojiamini. Jitambue, jikubali, amini inawezekana. Hii elimu mliyopata leo msiidharau, ichukue ifanyie kazi," amesema Jongo.

Katibu Tawala Wilaya ya Geita, Lucy Beda amewataka wanawake wajasiriamali kutumia fursa zilizopo kujikwamua kiuchumi, na kuahidi kuchukua changamoto zilizotajwa ili waweze kuzitatua kwa pamoja.