Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Biteko ataka mikopo umiza ikomeshwe

Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko akikabidhiwa zawadi na Rais wa Chama cha Wanawake katika Sekta ya Fedha (TAWI) Fikira Ntomola wakati wa mkutano wa chama hicho jijini Dodoma.

Muktasari:

  • Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko amekitaka Chama cha Wanawake wa Sekta ya Fedha (Tawifa) kutoa elimu ya matumizi sahihi ya fedha kwa wanawake ili kuepuka mikopo umiza.

Dodoma. Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko amewaagiza Chama cha Wanawake wa Sekta ya Fedha (Tawifa), kutoa elimu kwa wanawake juu ya matumizi ya fedha hasa za mikopo ili kuepusha kundi hilo kuingia katika mikopo hatarishi.

Mikopo hatarishi imepachikwa majina mengi ikiwemo kausha damu, komandoo, pasua moyo, kichefuchefu; imekuwa ikitajwa kuwa chanzo cha kufilisika, kujiua, kuvunjika kwa ndoa na kupata magonjwa ya akili baada ya wakopaji kushindwa kulipa kutokana na masharti magumu.

Changamoto ya mikopo umiza imekuwa ikiwakabili watu wengi, hali iliyofanya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuanzisha kampeni maalumu ya Zinduka, usiumizwe, kopa kwa maendeleo.

Akizungumza leo Jumatatu, Aprili 14, 2025, wakati akifungua mkutano wa chama hicho wa mwaka 2025, amesema bado elimu ya fedha haijawafikia wanawake wengi hasa walio vijijini.

“Utaona wanawake wengi wanakopa katika maeneo hatarishi na matokeo yake wanabaki kuwa watumwa wa wakopeshaji. Ni kawaida kuona wanawake mahali pengi wakifuatwa na watu wanaoitwa vicoba, wengine wanataka kuuza makochi yao, wengine masufuria yao,” amesema Dk Biteko.

Amesema kwa kuwa mwanamke anajishughulisha na furaha ya mtu mwingine, ukifuatilia unakuta kuwa mwanamke alipopata fedha hiyo alimpatia mwanaume akiamini kuwa atairejesha, lakini hafanyi hivyo.

“Tawifa mnawajibu wa kutoa elimu kwa wanawake juu ya matumizi ya fedha hasa zinazokopwa,” amesema.

Dk Biteko amesema kati ya asilimia 47 ya wafanyakazi katika sekta ya fedha ni wanawake, ni asilimia 10 pekee ndiyo waliopo kwenye nafasi za juu za uongozi.

Amesema hiyo inaonesha kuwa bado kuna changamoto nyingi zinazowakabili wanawake, mojawapo ikiwa ni ukosefu wa elimu ya fedha unaowapelekea kuchukua mikopo isiyofaa.

Dk Biteko amekiagiza chama hicho kuwekeza kwenye teknolojia itayowezesha kuwafikia wanawake wengi zaidi ili kuleta mabadiliko chanya katika maisha yao.

Pia, amekitaka chama hicho kutokata tamaa na kuhakikisha kinatekeleza malengo yake, licha ya kuwepo kwa watu au mazingira yanayoweza kujaribu kuvunja ari yao. Amesisitiza kuwa dhamira kuu ni kumkomboa mwanamke katika masuala ya kifedha na kiuchumi.

Naye Naibu Waziri wa Fedha, Chande amesema Serikali itaendelea kushirikiana na chama hicho na vyama vingine vya wanawake ili viendelee kuimarika kwa kasi kubwa.

Kwa upande wake, Rais wa Tawifa, Fikira Ntomola amesema mkakati wa chama ni kuhakikisha kuwa kufikia mwaka 2028, angalau asilimia 30 ya wanawake katika sekta ya fedha wanashikilia nafasi za juu za uongozi kupitia uwekezaji katika mafunzo mbalimbali ya uongozi na programu za ulezi.

Amesema kuwa lengo hilo linatarajiwa kuongezeka hadi asilimia 40 ifikapo mwaka 2033.

Kwa mujibu wake, ripoti ya utafiti uliofanywa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) uliohusisha nchi 70 duniani umeonesha kuwa endapo asilimia 30 ya nafasi za juu za uongozi zitashikiliwa na wanawake, mchango wake katika ukuaji wa uchumi huwa mkubwa.

Fikira amesema kuwa kutokana na matokeo hayo, chama hicho kimejizatiti kuwaunga mkono wanawake kupitia programu mbalimbali za maendeleo na uongozi.

“Ili kufanikisha lengo hili, chama kimetoa wito kwa Serikali kuendelea kuweka mazingira wezeshi yatakayowawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za kibiashara, hatimaye kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa Taifa,” amesema.

Aidha, Fikira ameomba benki na taasisi nyingine za kifedha kufanya utafiti wa kina kuhusu bidhaa zinazolengwa kwa wanawake kabla ya kuziwasilisha sokoni.

Amesema kwa kufanya hivyo, bidhaa hizo zitakuwa na ufanisi zaidi na kuwasaidia wanawake kuvitumia kuboresha kipato chao.

“Tumepokea maombi kutoka kwa vikundi mbalimbali vya wanawake wakihitaji mafunzo ya kifedha, na tuko tayari kuyatoa. Lengo letu ni kuwasaidia wanawake kupiga hatua kutoka ngazi moja hadi nyingine, hivyo tunaiomba Serikali kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya wanawake kuendesha biashara ndogondogo,” amesema.

Naye Naibu Kamishna Msaidizi wa Mamlaka ya Bima Tanzania (Tira), Khadija Said amesema wanasisitiza umuhimu wa ushiriki wa wanawake katika sekta ya fedha kwa sababu bima ni kinga dhidi ya majanga.

“Bima inamrudisha muhanga katika hali yake ya awali na kuleta utulivu wa kifedha. Bila usawa wa kijinsia na ushiriki wa wanawake kwa ufanisi hatuwezi kufanikisha maendeleo jumuishi,” amesema.