Prime
Wabunge walia na upungufu, ubora wa walimu

Muktasari:
- Kilio kikubwa cha wabunge kimekuwa ni upungufu wa walimu wakitaka kufanyika mageuzi makubwa katika kuajiri ili kupata wanaoendana na mitalaa mipya.
Dodoma. Uhaba wa walimu na upatikanaji wenye ubora watakaoendana na mtaala mpya wa mafunzo ya amali unaotumika sasa umekuwa ndiyo kilio cha wabunge wakiitaka Serikali itatue changamoto hiyo haraka.
Hayo yamejitokeza katika mjadala wa siku mbili jana na leo Jumanne, Mei 13, 2025, kuhusu bajeti ya Wizara ya Wizara ya Elimu kwa mwaka 2025/26, iliyowasilishwa na Waziri wa wizara hiyo, Profesa Adolf Mkenda. Waziri aliomba Sh2.43 trilioni, kati ya fedha hizo Sh1.74 trilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Katika michango yao, wabunge hao wametaka kufanyika mageuzi makubwa katika kuajiri walimu na kuwa bila kufanya hivyo, itachukua zaidi ya miaka 15 nchi ikiwa na upungufu watumishi hao.
Kilio cha wabunge kinashabihiana na kile kilichoelezwa na Taasisi ya HakiElimu Mei 12, 2025 kuelekea bajeti hiyo ikiwa sehemu ya mapendekezo yake matano ya kusaidia kuleta ufanisi katika utoaji wa elimu nchini.
HakiElimu ilishauri Serikali kuja na mkakati wa muda mfupi angalau miaka mitano kuajiri walimu wapya wasiopungua 40,000 kila mwaka.
Ilipendekeza pia kuongeza bajeti ya sekta ya elimu kufikia angalau asilimia 15, elimu iwe jumuishi na yenye mlengo wa kijinsia, kuandaa mkakati mahususi wa ajira na mafunzo kupunguza uhaba wa walimu pamoja na kutenga bajeti kwa ajili ya uchapaji na usambazaji wa vitabu vya mtaala mpya.
Jambo jingine walilogusia wabunge ni mikopo kwa ajili ya Watanzania wanaosoma elimu ya juu ili waweze kupatikana wataalamu wengi, kwa kuwa inashindikana kutokana na kukosa fedha za kujilipia.
Uwezo wa walimu
Katika mchango Mbunge wa kuteuliwa, Profesa Shukrani Manya licha ya kueleza kuhusu uhaba wa walimu, alienda mbele zaidi akihoji uwezo wa walimu wenyewe katika kufundisha mtalaa mpya wa elimu, akionya kwamba hakutakuwa na ubora unaotarajiwa, ikiwa waliopo wataanza kufundisha bila kuwa na mafunzo mahsusi.
“Walimu watakaofundisha mtalaa mpya wasiwe walimu ambao hawakufunzwa vizuri, wakiwa ni walimu ambao wametokana mtalaa wa zamani, ila wamepewa mafunzo kidogo tu watapeleka ujuzi wao wa zamani katika mtalaa mpya,” amesema.
Profesa Manya amependekeza walimu waliopo wapewe mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu kwa kuzingatia teknolojia ya sasa, wakishaiva watatoa wahitimu bora na zao ambalo Taifa lingetamani kulipata.
Amesema si sahihi kuwafundisha wanafunzi teknolojia za zamani kwamba ndiyo sababu ya kuwa na maabara za zamani katika vyuo vikuu, huku akishauri Serikali itoe mikopo kwa Watanzania wanaotaka kusoma shahada ya uzamili na uzamivu, kuliko kuendelea kutegemea wafadhili.

Msomi huyo amesema ni wakati sasa kwa Tanzania inapoingia katika utekeleza wa mitalaa mipya, isiache kuwatumia wataalamu kutoka nje ya nchi, ili wasaidie kuboresha uwezo wa walimu wa ndani.
Kwa upande wake Mbunge wa Singida Mjini (CCM), Mussa Sima amesema mdondoko wa wanafunzi ni mkubwa shuleni na kuwa kuna tatizo kubwa la uhaba wa walimu, hivyo akaitaka Serikali ije na mkakati wa kukabiliana na suala hilo.
Sima ameshauri walimu wanaojitolea wapewe kipaumbele zaidi kwa kuwa walishazoea mazingira na uwezo wa kufundisha kwa vitendo badala ya kuchukua watu ambao hawajazoea.
Akisisitiza umuhimu wa kada hiyo, Mbunge wa Muleba Kaskazini (CCM), Charles Mwijage ameitaka Serikali kuja na uamuzi mgumu wa kusitisha baadhi ya huduma ili ielekeze fedha kwenye ajira za walimu.
Mwijage amesema ziko nchi ambazo ziliamua kufanya hivyo hazijawahi kujutia na Tanzania ikifanya hivyo haitajutia, kwani litakuwa ni jambo jema lenye maana na tija kwa Taifa.
“Tusimamishe mambo mengine tukatoe ajira za walimu hawa walioko mtaani ambao wanafikia 265,000, tukiwachukua wote kwa wakati mmoja tutakuwa tumemaliza na kufuta kabisa kilio cha walimu, ndipo mambo mengine yatafuata,” amesema Mwijage.
Kuhusu hilo, Maimuma Mtanda, mbunge wa Newala vijijini (CCM) amesema uhaba wa walimu umekuwa ni mkubwa na ndicho chanzo cha mdondoko wa wanafunzi, akitolea mfano wilaya yake ambayo ina upungufu wa walimu 400.
Mtanda ameitaka Serikali kuacha kuzungumza kwa mdomo badala yake ije na vitendo kwa kutoa ajira ili walimu wengi wapatikane kwa wakati mmoja, ndipo wanaweza kuinua ubora wa elimu.
Wabunge wengine waliozungumzia uhaba wa walimu ni Aysharose Mattembe (Viti Maalumu) aliyesisitiza ajira mpya za walimu, Francis Ndulane (Kilwa Kaskazini) ambaye ameitaja wilaya ya Kilwa kuwa na upungufu wa zaidi ya walimu 500.
Mbuge wa Sengerema (CCM), Hamisi Tabasamu aliyesema kwa namna yoyote bila kuwatumia walimu wanaojitolea kuingia moja kwa moja kwenye ajira, upungufu wa walimu utazidi.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ng’wasi Kamani aliungana na Profesa Manya kuzungumzia uwezo wa walimu katika kufundisha mtaalamu mpya, aliosema bila kuwa na wataalamu mahiri, hakutakuwa na maana yoyote kwenye mafunzo ya amali.
Kamani amesema bado Watanzania wengi hawajajua kwa kina kuhusu maana halisi ya amali, hivyo angetamani wapewe elimu, hoja ambayo iliungwa mkono pia na Mbunge wa Tabora Kaskazini, Almas Maige.
Hata hivyo, Maige amesema ni muhimu zikateuliwa shule chache ambazo zitaanza kuanzia sasa, kufundisha kuliko kusubiri kukamilika kwa shule zote ambazo amesema mpango huo unaweza kuchelewa.
Mbali na hayo, Mbunge wa Viti Maalumu, Nusrat Hanje yeye amesisitiza suala tofauti la elimu ya lugha ya alama, kwamba itolewe kwa ulazima kwa watu wote, ili kuwaunganisha watu katika mawasiliano, kuliko ilivyo sasa ambapo kundi la wenye ulemavu linashindwa hata kufuatilia Bunge kwa kuwa ni kama limetengwa.
Waziri akubali
Akijibu hoja hizo, Profesa Mkenda amesema Serikali ipo tayari kuchukua wakufunzi kutoka nje ya nchi ili waje kutoa ujuzi kwa walimu wa amali nchini.
Profesa Mkenda amesema hakuna tatizo kwani ujuzi unahitajika na kwa namna yoyote kutakuwa na utaratibu wa kuhakikisha wanapatikana wataalamu wazuri wa kuwafundisha walimu nchini.
Kwenye hoja ya mkopo kwa wasomi, Waziri amesema mpango huo ulishaanza na hadi sasa kuna watu 80 ambao wamepewa mkopo kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili ambao wanasoma Chuo cha Nelson Mandela.

“Tunalenga kukifanya chuo hicho kuwa cha wasomi na watu maarufu katika tafiti mbalimbali, pale watasoma watu wa kuanzia Shahada ya Uzamili ili tuweze kuzalisha wataalamu wa kutosha na suala la mkopo litakuwa endelevu,” amesema.
Kwa hoja ya walimu wa kujitolea ili waweze kuajiriwa, amesema mpango huo umefanyiwa maboresha na hadi sasa wanayo ikama ya walimu wa kujitolea 23,465, ambao pia wanaonyesha uwezo na mchango mkubwa.
Akihitimisha Bunge mchana wa leo Jumanne, Naibu Spika, Mussa Zungu ameitaka Serikali kufanya kila liwezekanalo na kutoa kipaumbele kwa walimu wanaofundisha kwa kujitolea ili wawe wa kwanza kuingia kwenye ajira, kwani baadhi yao wamefanya kazi hiyo zaidi ya miaka saba lakini hawafikiriwi.