Waitara alia na walimu wa lugha

Mbunge wa Tarime Vijijini (CCM), Mwita Waitara, akichangia mkadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka 2025/26 bungeni leo Jumatatu Mei 12, 2025. Picha na Hamis Mniha
Muktasari:
- Changamoto ya walimu waliobobea katika lugha, imemuibua Mbunge wa Tarime Vijijini (CCM) Mwita Waitara akihimiza kuangaliwa suala hilo.
Dodoma. Mbunge wa Tarime Vijijini (CCM), Mwita Waitara amesema kuna changamoto ya walimu waliobobea kwenye ufundishaji wa mtalaa mpya kwa sababu wengi waliopo wanauelewa mdogo.
Waitara alikuwa akichangia mkadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka 2025/26 bungeni jijini Dodoma leo Jumatatu Mei 12, 2025.
Makadirio hayo yamewasilishwa na Waziri mwenye dhamana ya elimu, Profesa Adolf Mkenda ambaye ameliomba Bunge kumuidhinishia Sh2.4 trilioni kwa mwaka 2025/26 huku Sh1.74 trilioni zikienda katika miradi ya maendeleo.
Katika mwaka 2024/25, Bunge liliidhinishia wizara hiyo bajeti ya Sh1.97 trilioni huku miradi ya maendeleo ikitengewa Sh1.32 trilioni.
“Na kuna upungufu mkubwa sana wa vifaa, fanya tathimini kwanza kama unaweza kufanya kwa wakati mmoja kuanza mtalaa mpya tuendelee kama unadhani hatuwezi tungechagua baadhi ya shule,”amesema Waitara alipokuwa akichangia makadirio hayo.
Ameshauri Serikali kufundisha walimu wa sekondari zote kuhusu mtalaa huo ili waelewe jinsi ya kuufundisha.
Amesema walimu wa Kiingereza waliobobea katika ufundishaji wa lugha hiyo hawapo wa kutosha katika shule za sekondari nchini.
Waitara amesema wanafunzi katika shule za msingi wanasoma masomo yote kwa Kiswahili, lakini wanapofika katika shule za sekondari wanapambana kujua lugha ya Kiingereza kwa kuwa ndio inayotumika kufundisha.
Amesema ukienda katika jimbo lake, wanafunzi wa kidato cha pili waliopata daraja 0 mwaka jana, walikuwa ni 1,539 wakati waliopata daraja la nne walikuwa ni 3,710.
“Nenda miaka mitatu ya nyuma, kuna shida ya lugha ya kujifunzia, twendeni tuandae walimu wanaojua lugha vizuri, bora akose mwalimu wa hesabu kwa muda, atafundishwa mtaani lakini lugha kunafanya watoto wakimbie masomo na waache shule,”amesema.
Waitara ambaye kitaaluma ni mwalimu, amesema sababu za wanafunzi kuacha shule kuwa ni pamoja kushindwa kufahamu lugha.
“Mwalimu mwenyewe anafundisha Kiingereza hajui, inaitwa kiswa - kinge, mwanafunzi anashangaa mwanzo hadi mwisho wa kipindi. Hapo kuna mtihani ni muhimu Serikali ijipange kuandaa walimu wa Kiingereza na kama bajeti haitoshi, watoto kabla ya kuingia kidato cha kwanza wafanye kozi ya maandalizi,”amesema.
Naye Mbunge wa Vwawa (CCM), Japhet Hasunga amesema watoto wanaogopa masomo ya sayansi na hisabati.
Amesema inamaanisha kuwa nchi imara haiwezi kujengwa bila kuwa na watu waliosoma sayansi na teknolojia.
“Tuandae watoto wetu kupenda masomo ya sayansi na kama tunasema sayansi hatuitaki ina maana hatuwezi kwenda kokote kule, tuwaandae vijana wetu kupenda sayansi,”amesema.
Hasunga amesema tatizo la wanafunzi kuogopa masomo ya sayansi na hesabu yanatokana na kutishiwa kuwa ni magumu kabla hata ya kufika shuleni.
Amesema changamoto hiyo inasababishwa na saikolojia na hivyo kinachotakiwa kufanywa ni kujenga misingi ya vijana kupenda hesabu na sayansi.
Aidha, amesema maeneo mengi ya shule hayana walimu wa fizikia kwa sababu hawapo na kushauri kuandaliwa kwa walimu hao.
Naye Mbunge wa Geita Mjini (CCM), Constantine Kanyasu ameshauri Serikali kuangalia mitihani inayotungwa kwa ajili ya kudahili walimu wapya kama inaendana na masomo waliyosoma walimu wa zamani.
Amesema walimu waliokuwa wakijitolea katika shule mbili jimboni kwake, walikwenda kufanya mitihani ya ajira lakini walifeli ingawa shule hizo zinafanya vizuri kwa masomo yanayofundishwa na walimu hao.