Prime
Wadau waikaanga wizara mitihani kwa walimu

Ni mwendelezo wa kuvuruga na kudhalilisha taaluma ya walimu. Hivi ndivyo inavyotafsiriwa na baadhi ya wadau wa elimu, kufuatia utaratibu mpya uliotangazwa hivi karibuni utakaotumika kuajiri walimu ukihusisha ufanyaji wa mtihani.
Mjadala umeibuka tangu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda aeleleze utaratibu huo mpya, kuwa kuanzia sasa ajira katika kada hiyo zitatolewa kwa mwalimu aliyefanya mtihani na kufaulu.
Utaratibu uliokuwa ukitumika awali kwenye ajira za walimu ulihusisha kutuma maombi katika tovuti maalum ya maombi ya ajira. Anayepata nafasi kupangiwa eneo la kazi lakini sasa atapangiwa kituo cha kazi baada ya kufanya mtihani na kufaulu.
Profesa Mkenda alieleza kuhusu utaratibu huo Juni 16, 2023 wakati wa hafla ya utoaji tuzo kwa walimu walioshinda shindano la kwanza la stadi za kufundisha kuhesabu na hisabati, lililoandaliwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET).
“Wakati wa kutangaza nafasi mpya za ualimu, wakitaka kupata kazi, watafanya mtihani haijalishi tayari umesoma, kwanza itatuondolea matatizo. Kuajiriwa kuwa mwalimu utafanya mtihani, utaona matokeo, tutaangalia idadi inayohitajika tutachukua waliofaulu tutawaajiri,” alieleza.
Kwa mujibu wa Profesa Mkenda, utaratibu huo unalenga kurudisha hadhi ya taaluma ya ualimu, kwamba isitazamwe kuwa chaguo la mwisho baada ya wanafunzi kukosa kozi nyingine za kusoma vyuoni.
Licha ya kukubaliana na lengo la Serikali katika kuifanyia maboresho sekta ya elimu, wadau wameonyesha kutoridhishwa na utaratibu huo mpya wa kuajiri walimu wakieleza kuwa utadhalilisha taaluma hiyo na kuiondolea heshima.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) Dk Paul Loisulie anasema badala ya kutumia nguvu nyingi katika kuweka mitihani, ungefanyika mchakato wa kuanzisha bodi ya walimu ambayo ndiyo itachukua jukumu la kusimamia taaluma ya ualimu.
“Waziri anatakiwa kupambana na bodi ambayo itakuwa na jukumu la kusimamia taaluma ya ualimu na maadili yake lakini sio kuweka mitihani kwa walimu. Kauli za aina hii zinazidi kuwavuruga walimu na kuwaondolea ari ya kufanya kazi.
Kama lengo ni kurekebisha au kuongeza ufanisi kwa walimu, basi itengwe bajeti kwa ajili ya programu za mafunzo wakiwa kazini, siasa zisiwekwe kwenye taaluma. Kuliko kuwa na mitihani ni heri ukawepo utaratibu wa usaili kwa maana ya kwamba kila halmashauri ikawa na utaratibu wa kuwasaili walimu wapya,” anasema Dk Loisulie.
Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Leah Ulaya ni miongoni mwa waliopingana na utaratibu huo licha ya kukiri kuwa huenda uamuzi huo wa Serikali una nia njema ya kutengeneza walimu bora na wenye vigezo vya kufundisha.
Akizungumzia hilo, Leah anasema si sahihi kwa mwalimu kufanya mtihani ilhali alipita chuoni na kupewa mafunzo yaliyothibitishwa kupitia mitihani aliyofanya kabla ya kuhitimu.
Leah ambaye kitaaluma ni mwalimu, anasema kumfanyisha mtihani mwalimu inaweza kumletea athari ya kisaikolojia na inawezekana akawa mwalimu mzuri lakini asifanye vyema katika mtihani huo.
Leah amekwenda mbele zaidi na kueleza endapo utaratibu huo utafanyika, utawaumiza walimu hasa waliomaliza chuo kwa muda mrefu na kukaa mtaani kwa kukosa ajira.
“Tunashuhudia walimu wengi wanamaliza masomo yao na kusota mtaani kutokana na ukosefu wa ajira, sasa mwalimu huyu ambaye ameshakaa nyumbani kwa muda mrefu inatokea ajira leo unamwambia afanye mtihani humtendei haki, kwa sababu ili mtu umpe mtihani lazima umfundishe sasa huo mtihani atajibu kwa mafunzo gani?’’ anahoji na kuongeza:
‘’Kinachotakiwa hapa Serikali iwe inaajiri walimu wanapotoka vyuoni wasikae muda mrefu mtaani, pia urudishwe utaratibu wa mafunzo kazini. Kwa mfano, waajiriwa wapya waripoti kwenye vituo vyao halafu baada ya miezi mitatu wapewe mafunzo.
Kiongozi huyo wa CWT anasema bado kuna nafasi ya Serikali kukaa na wadau kujadili suala hilo, huku akibainisha kuwa chama chake kiko tayari kushauri namna bora ya kuwa na walimu bora kwa kuwa suala hilo ni muhimu kwa mustakabali wa Taifa.
Hoja hiyo imeelezwa pia na msemaji wa sekta ya elimu wa chama cha ACT- Wazalendo Riziki Mngwali aliyeeleza kutoridhishwa na mpango huo wa Serikali wa kuwafanyisha mitihani walimu.
Riziki anasema mwalimu anapatikana kutokana mifumo iliyowekwa inayoelekeza ili mtu awe mwalimu ni lazima apitie chuo kwa ajili ya mafunzo ya ualimu ambayo yatatolewa na mtu mwenye sifa za kufundisha.
“Huyu mwalimu akiwa chuoni atasoma, atafanya mitihani, majaribio, mafunzo kwa vitendo na mazoezi yanayomjenga na kumuimarisha katika taaluma hiyo. Sasa kama amepitia yote haya inakuwaje inapofika kwenye kumuajiri unataka afanye mtihani.
“Je hatuna imani na mifumo ambayo tumeiweka yenyewe, kwa sababu kama vyuo vina jukumu la kuandaa walimu halafu unataka mwalimu afanye mtihani ili aajiriwe ni wazi kwamba hatuna imani na njia aliyopitia kuandaliwa. Nini kinatupa wasiwasi halafu nani amethibitisha kwamba mtihani wa saa mbili unaweza kupima uwezo wa mtu ambaye huamini alichojifunza katika miaka mitatu?’’ anahoji.
Kukabiliana na wasiwasi huo, Riziki anaeleza ipo haja ya kurudi na kuangalia namna vyuo vinavyofundisha ili kuwapata wahitimu bora wa kada ya ualimu kulingana na vigezo vilivyowekwa na kuwekwa muda wa uangalizi kwa walimu wanapoajiriwa.
“Turudi tuangalie mfumo mzima, kuna changamoto gani hadi tunapata wasiwasi huu, kisha turekebishe. Mafunzo ya ualimu yatolewe na watu walioiva katika kada hiyo halafu pia kama kuna haja ya kuwachuja basi uwepo muda wa uangalizi ikionekana ndani ya miezi mitatu mwalimu hafanyi vizuri, basi atolewe lakini sio kufanya mtihani kuwa ndio kigezo cha ajira,”anaeleza.
Mtazamo tofauti
Wakati wadau hao wakipinga utaratibu huo, Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (Tenmet), Ochola Wayoga ana mtazamo tofauti, akieleza kuwa unaweza kupunguza kilio cha muda mrefu cha ubora wa walimu kutokana na kada hiyo kuingiliwa na watu wengi wasiokuwa na sifa.
Hata hivyo, anakiri kuwa utaratibu huo bado unaweza usiwe suluhu ya kukabiliana na changamoto hiyo kwa kuwa inawezekana wapo watakaofaulu mtihani na kuajiriwa lakini wasiwe walimu wazuri.
“Sioni kama utakuwa na manufaa makubwa ila hata kwa kuanzia nakubaliana na utaratibu huu, utasaidia kupunguza watu wasio na sifa za ualimu kuvamia taaluma hii ambayo kwa kiasi kikubwa inahitaji kuwa na watu wenye wito na mapenzi na kazi hii.
Kumekuwa na mjadala kwamba kutofanyika kwa tathmini yoyote katika kuwapata walimu ndiyo chanzo cha kuwa na walimu wasiofaa. Ni ukweli kwamba si kila mtu anaweza kuwa mwalimu, tumekuwa tukifanya ualimu ni kazi rahisi kuipata wakati ni kada ya jukumu kubwa katika kujenga Taifa,”anasema.
Ili utaratibu huo ulete matokeo chanya, Wayoga anashauri Serikali kutoa mwongozo utakaoonyesha namna itakavyofanyika mitihani hiyo ili kusiwe na uonevu wala upendeleo kuepusha malalamiko.
“Kama tayari Serikali imeliona hili basi iweke mfumo utakaowezesha upatikanaji walimu wenye vigezo na sifa stahiki, taaluma hii ina heshima sio chaguo la watu walioshindwa katika maeneo mengine,”anaongeza kusema Wayoga.
Wasemavyo walimu
Mwalimu mstaafu, Daniel Matembele anapingana na utaratibu huu akieleza kuwa utafifisha taaluma ya ualimu na kuzidi kuiondolea heshima kwenye jamii licha ya umuhimu wake.
“Sikubaliani kabisa na utaratibu huo, sasa kama ili mwalimu aajiriwe ni lazima afanye mtihani kulikuwa na umuhimu gani wa kusoma chuoni, kufanya mafunzo kwa vitendo na kufanya mtihani wa mwisho hadi akatunukiwa cheti kwamba amefaulu? Tatizo ninaloliona ni siasa kuingizwa kwenye mambo ya msingi,” anasema Matembele.
Naye mwalimu Debora Nyanja wa Shule ya Sekondari Kisauke, anasema utaratibu huo sio njia sahihi ya kupata walimu bora, kwani itafanya kada ya ualimu izidi kudhalilishwa.
“Mwalimu anasoma darasani, anafanya mazoezi kwa vitendo kisha anafanya mtihani wa kuhitimu, kumwambia ili aajiriwe ni lazima afanye mtihani ni kumdhalilisha mwalimu na kada nzima ya ualimu. Huyu mwalimu amefundishwa na walimu huko chini ina maana hatuwaamini?
Ninachoona hapa ili kuwa na elimu bora, walimu washirikishwe kwenye uandaaji wa mitalaa maana wao ndiyo wanatumia muda mwingi kuwa na wanafunz; wanajua kitu gani kinahitajika katika kuwaimarisha kitaaluma, kimaadili na kijamii,” anasema Debora.
Mawazo ya Debora hayatofautiani na yaliyotolewa na mwalimu mkuu wa shule ya awali na msingi Moga, mchungaji Leonard Ntimba, aliyeeleza kuwa hakuna sababu ya kumtahini mtu ambaye alishakaa chuoni na kufundishwa ualimu.
“Mimi ni mwalimu ninachofahamu ukisomea ualimu ndani ya miezi miwili ya mafunzo, tayari unaanza kuishi misingi ya ualimu. Kutaka mwalimu afanye mtihani naona imekaa kisiasa na inaweza kutengeneza mianya ya rushwa.
“Ninachoona kwa sababu nia ya waziri ni njema basi uwekezaji ukafanyike kwenye vyuo vya ualimu, kule iondolewe mianya yote inayoweza kumruhusu atoke akiwa hajaiva. Chuoni kuna muda wa kwenda kwenye mafunzo kwa vitendo, pale ndio panga lingenolewa ili kuhakikisha mwalimu anatoka akiwa ameiva sio kusubiri amalize chuo apewe cheti halafu kwenye kuajiriwa useme afanye mtihani,”anasema Ntimba.
Profesa Mkenda afunguka
Akitolea ufafanuzi suala hili hivi karibuni nje ya viwanja vya Bunge, Profesa Mkenda alisema walimu kufanya mitihani ni maoni ya wadau na yapo katika mapendekezo ya rasimu ya Sera ya Elimu.
Anasema tangu maoni haya yatolewe baada ya rasimu hiyo kusomwa, hajawahi kusikia watu wakipingana na utaratibu huu kwa kuwa lengo lake ni jema kupata walimu bora. “Ifahamike kwamba utaratibu huu hautawagusa walimu waliopo kazini, watakaofanya mitihani ni waajiriwa wapya kuanzia ajira mpya zitakazotolewa baada ya sera mpya kutumika.
“Walimu walipo kazini watapewa semina na mafunzo, hata kwenye bajeti ya mwaka huu tumetenga fedha kwa ajili ya mafunzo kwa walimu ambao wapo kazini. Hawana sababu ya kuhofia tutasawasaidia kujiendelea, hatutawaondoa kazini watabaki hapo hadi muda wao wa kustaafu utakavyofika,”
Kuhusu utaratibu wa mitihani hiyo, waziri alisema taarifa zote zitatolewa baada ya sera kupitishwa na kuanza kufanya kazi na kwamba utaratibu huo utashirikisha wadau.
“Tunataka hadhi ya ualimu irudi, tunataka mwalimu awe yule aliyeandaliwa na akaiva kuwa mwalimu. Kuna wanaosema labda hatuamini vyuo vyetu, hapana huu ni utaratibu wa kawaida kama unavyofanyika kwenye fani nyingine,” alisema.