Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali kupima vyuo vikuu kwa ubora wa tafiti, ufundishaji

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda pamoja na Mkuu wa chuo kikuu cha KCMC ambaye ni Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Alex Malasusa wakiteta jambo  wakati wa uzinduzi wa chuo hicho kilichopo Moshi, Mkoani Kilimanjaro. Picha na Janeth Joseph

Muktasari:

  • Profesa Adolf Mkenda amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha vyuo vikuu vinakuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya kitaaluma na kiteknolojia kwa kufanya tafiti zenye tija.

Moshi. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema Serikali imeanza mchakato wa kuvipima vyuo vikuu nchini kwa kuzingatia viwango vya ufundishaji wa wahadhiri, ubora wa tafiti na namna matokeo ya tafiti hizo yanavyotolewa na kutambulika kimataifa.

Profesa Mkenda amesema hayo leo Mei 10, 2025 alipozindua Chuo Kikuu cha KCMC kilichopo Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Chuo hicho kimepandishwa hadhi na Serikali kutoka kuwa Chuo Kikuu Kishiriki cha Tiba na Afya (KCMUCo) kuwa chuo kikuu kamili.

Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha vyuo vikuu vinakuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya kitaaluma na kiteknolojia kwa kufanya tafiti zenye tija na kuongeza ushindani wa kimataifa.

"Tunavyoendelea kuvipima vyuo vikuu nchini, tunavipima kwanza kwa uwezo wa wahadhiri wake, kufanya tafiti na kutoa matokeo ya utafiti wake duniani na katika ufundishaji," amesema.

Amesema kazi ya chuo kikuu si kufundisha pekee bali ni kufanya tafiti na kutoa gunduzi zenye kujibu changamoto za kijamii.

"Chuo kikuu kikawa kinafanya kazi ya kufundisha tu kinakuwa ni kama 'high school' si chuo kikuu," amesema.



Profesa Mkenda amekipongeza chuo hicho kwa kuendelea kufanya tafiti za kisayansi, akizungumzia utafiti ambao umechapishwa hivi karibuni na jarida la kimataifa la nje kuhusu mbege na vyakula vya asili vinavyoimarisha kinga ya mwili.

"Tunaendelea kuhimiza watafiti wetu kuchapisha katika majarida makubwa zaidi duniani na tunapokwenda huko majarida yetu yataendelea kukua kwa sababu baadhi ya tafiti zitachapishwa kwenye majarida yetu humu," amesema.

Mkuu wa chuo hicho, ambaye ni Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa ameishukuru Serikali kwa namna ambavyo imekuwa mstari wa mbele kwenye sekta ya elimu, afya na kuhakikisha vyuo vinaendelea kutoa elimu bora nchini.

Amesema chuo hicho kimejiwekea mikakati itakayofanikisha mipango mizuri ikiwa ni pamoja na kuanzisha mfuko maalumu (KCMC endowment fund) kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wenye uhitaji wanaojiunga na chuo hicho.

"Mfuko huu utasaidia vijana wengi kufikia ndoto zao kwa kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia, maana hapa tunapata vijana wengi wasiokuwa na uwezo wa kulipa ada lakini wana uwezo mzuri wa kujifunza na tunaona wanaweza wakawa msaada mkubwa kwa Taifa letu," amesema.

Askofu Malasusa amesema tangu kuanzishwa kwa chuo hicho mwaka 1997, kimezalisha maelfu ya wataalamu ambao hivi sasa wanalitumikia Taifa katika nyanja mbalimbali.

Katibu Mtendaji wa Shirika la Msamaria Mwema, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya KCMC, Profesa Gileard Masenga amesema chuo hicho kimekuwa kikizalisha madaktari 200 kila mwaka na madaktari bingwa 120 kila mwaka.