Prime
Huu ndio umuhimu wa elimuhisia kwenye mfumo wa elimu

Muktasari:
- Ukiangalia namna mwalimu anavyoandaliwa kwa ngazi mbalimbali, utaona wazi msisitizo mkubwa umewekwa kwenye uelewa wa masomo ya kufundishia, misingi ya ualimu na kwa kweli eneo la hisia ni kama halina msisitizo wa kutosha.
Dar es Salaam. Nimekuwa nikishirikiana na shule mbalimbali kuutazama mchakato wa ujifunzaji na mbinu wanazotumia, kumwezesha mwanafunzi kufikia malengo yanayobainishwa na mtalaa.
Katika kutekeleza majukumu yao, walimu wanakabiliana na changamoto mbalimbali.
Kwa mfano, masuala kama ukosefu wa mazingira wezeshi ya kufundishia, uhaba wa vifaa vya kufundishia, matatizo ya nidhamu kwa wanafunzi yanachangia, kwa kiasi kikubwa, kuzorotesha ari ya wanafunzi kujifunza.
Lakini pia, kiwango cha uelewa wa namna ya kushughulika na nidhamu ya wanafunzi kinatisha.
Walimu wengi, mathalani, wanaamini woga ndio msingi muhimu wa nidhamu ya mwanafunzi. Hii, pengine, ndio sababu kudhibiti mawazo ya wanafunzi darasani, inaonekana ndio kipaumbele kuliko kuchochea udadisi.
Sehemu ya tatizo, naamini, ni muundo wa mafunzo yenyewe ya ualimu. Ukiangalia namna mwalimu anavyoandaliwa kwa ngazi mbalimbali, utaona wazi msisitizo mkubwa umewekwa kwenye uelewa wa masomo ya kufundishia, misingi ya ualimu na kwa kweli eneo la hisia ni kama halina msisitizo wa kutosha.
Umuhimu wa hisia
Katika kuwezesha ujifunzaji, hisia zina nafasi ya pekee. Sayansi ya ujifunzaji inaonesha wazi kuwa uwezo wa mtu kufikiri na kujifunza unategemea Kwa kiasi kikubwa utulivu wa kihisia alionao mtoto.
Mtoto mwenye huzuni, majuto, upweke, maumivu ya kihisia, hawezi kujifunza kwa ufanisi. Kwa msingi huo, hatuwezi kutenganisha fikra angavu na namna mtoto anavyojisikia.
Aidha, watafiti wa eneo hili la hisia wanatuambia kuwa hisia, kama eneo muhimu katika makuzi, ni zao la uhusiano wa karibu baina ya mtoto na mzazi wake. Miaka ya mwanzo ya maisha ya mtu inajenga msingi muhimu wa hisia.
Je, ni kwa kiwango gani watoto wetu wanapata mahitaji yao ya kihisia katika ngazi ya familia? Je, wazazi wanaelewa wajibu wao katika kujenga hisia za watoto wao? Katika mazingira ambayo mzazi anaweza kukosa uelewa na hata utashi wa kumsaidia mtoto, mwalimu ana nafasi kubwa ya kumsaidia mtoto kujaza ombwe analokuja nalo shuleni.
Umahirihisia
Imethibitika kisayansi kuwa watu wenye kiwango cha juu cha umahirihisia wana nafasi kubwa ya kufanikiwa kwenye shughuli zao kuliko watu wenye akili nyingi lakini wasiozielewa na kurekebu hisia zao.
Umahirihisia ni uwezo wa kuelewa namna hisia zetu zinavyofanya kazi, kuzitambua kadri zinavyoitokeza, kuelewa nini kinazichochea, kuzirekebu (regulate), kuzimudu lakini pia kuelewa namna ya kuzitumia hisia hizi kuwasiliana na kuboresha mahusiano yetu na watu.
Umahirihisia una mawanda mengi. Hata hivyo, Daniel Goleman anayeaminika kuwa mtaalam wa kwanza kuitambulisha elimu hii kwa umma, anautazama katika nyanja kuu tano muhimu, ambazo zinaweza kuwa sehemu muhimu ya programu za kukuza umahiri hisia kwa walimu na wanafunzi wetu.
Kwanza, ni kuzitambua hisia zako mwenyewe ikiwa ni pamoja na matokeo yake kwa wengine; pili kurekebu na kumudu hisia; tatu kutambua na heshimu hisia za mwingine (ushirikieli), nne kujenga na kukuza motisha binafsi na tano kutumia hisia katika kuwasiliana na kuhusiana na watu.
Nchi mbalimbali zilizooendelea zimefanya jitihada za makusudi kutambua umuhimu wa kuwa na programu maalumu zinazolenga kukuza hisia za watoto.
Moja ya program zinazokuza umahiri hisia ni ile inayofahamika kama ujifunzaji wa hisia na uhusiano (social emotional learning) kwa kifupi SEL. Manufaa ya program kama hizi ni pamoja na kuongeza uwezo wa wanafunzi kujitambua, kuimarisha utengemavu wa afya ya akili kwa watoto, kukuza nidhamu ya wanafunzi, kuimarisha uhusiano baina ya walimu na walimu na kubwa kabisa ni kuinua kiwango cha kuongeza ufaulu.
Tuangalie maeneo manne makubwa yanayozingatiwa na program kama hizi zinazoweza kuufaa mfumo wetu wa elimu.
Kukuza msamiati wa hisia
Hatuwezi kuwa na mwanafunzi tunayesema ameelimika vyema ikiwa anapata shida kuzielewa hisia zake. Mwanafunzi wa namna hii, kwa hakika, ana uwezekano mkubwa wa kujikuta katika matatizo makubwa anapochangamana na watu wengine.
Uelewa wa hisia unakwenda sambamba na mtu kuwa na msamiati sahihi wa hisia. Katika kujenga msamiati wa hisia, mtoto anafundishwa kueleza vile anavyojisikia: hasira, furaha, upendo, woga, ujasiri, aibu, fadhaa, fahari, hatia, wivu, husda na kadhalika.
Sambamba na kuzielewa hisia zake, mtoto anajifunza ujumbe unaobebwa na hisia hizi. Hasira, kwa mfano, ni maandalizi ya ubongo kushambulia na kulinda usalama. Hatia, kwa mfano, ni ujumbe wa ksoa lililofanyika na kadhlika kadhalika.
Tunawezaje kuweka mazingira yanayomsaidia mtoto wa Kitanzania kufuatilia mihemuko yake? Tunawezaje kumsaidia mtoto kutofautisha na mihemko na hisia zake kama upendo, fahari, hatia, majuto, fedheha, chuki, husda na kadhalika?
Kujifunza msamiati wa hisia na kuuelewa ujumbe unaobebwa na hisia hizo ni msingi mkubwa wa maamuzi yake mengi katika maisha.
Kurekebu na kutawala hisia
Matukio ya walimu kuwavamia watoto na kuwaumiza kimwili na hisia yanaeleza tatizo la uwezo mdogo wa walimu kukosa mahiri za kutawala hisia zao. Ukitazama migogoro mingi katika mazingira ya ujifunzaji, hali kadhalika, unaona uwezo hafifu wa mwalimu au mwanafunzi kuelewa ni wakati upi hisia zinaweza kuletea hasara. Huu ndio msingi mkuu wa pili wa kumsaidia mwalimu na mwanafunzi kujifunza umahiri hisia.
Kimaumbile, tunaambiwa na wataalam, hisia hutuvaa kabla hatujafikiri na kuyachambua mazingira yaliyochokoza hisia zetu. Kimaumbile, tunahisi kisha tunafikiri.
Kabla mtu hajawaza kinachomkasirisha, mathalani, hatua ambayo inahitaji kushirikisha sehemu ya ubongo inayofikiri, tayari anakuwa ameshakuwa kwenye mazingira ya kuchukua hatua kama kushambulia, kujitetea, kusema maneno makali na kadhalika, hatua zinazoweza kuleta madhara makubwa ndani ya muda mfupi hata kabla hajaanza kutafakari.
Ingawa ni kweli hisia hutawala tabia zetu, bado tunaweza kujifunza kutumia vyema ufahamu wetu kuzielewa, kuelewa zinavyofanya kazi, mazingira yanayozichochea na matokeo ya hisia hizo kwa wengine.
Shule zetu na vyuo vyetu vinavyoandaa walimu vina uwezo wa kuwapa walimu na wanafunzi nyenzo hizi za kuwawezesha kumudu hisia zao. Mwalimu anapokuwa na nyenzo hii, inakuwa nadra kwake kupelekeshwa na hisia na hivyo kujua namna ya kukwepa mazingira yanayochochea hisia hizo.
Kujenga motisha na ari ya kazi
Motisha si kutambuliwa kwa kazi mtu anayofanya, kuonekana, kusifiwa, kupandishwa cheo wala kupewa kitu kama bakhshishi ya bidii ya kazi. Motisha ni ile sababu inayoamsha ari ya kujipata, kujua mtu anataka kufanya nini na maisha yake, kubaini na kupambania malengo aliyonayo. Motisha ni ule msukumo unaomnyima mtu usingizi ili atie bidii kwenye kile anachokifanya.
Motisha huleta nidhamu. Mtu mwenye motisha ana uwezo wa kusema hapana kwa chochote kinachoingilia malengo. Tukisema mwanafunzi ana nidhamu maana yake tumejiridhisha kuwa ana uwezo wa kusimamia malengo yake kwa kujijengea utaratibu wa maisha yanayotabirika kuwezesha kutekelezeka kwa malengo hayo.
Nidhamu hutegemea uwezo wa mwanafunzi kumudu hisia zake, namna anavyonyamazisha matamanio yake, na kuchochea ari ya kulipa gharama ya kesho iliyobora.
Je, tunaweza kuingiza umahiri wa motisha kwenye madarasa yetu? Ni kwa kiasi gani hatua hii inaweza kupunguza uvivu na ugoigoi kwa wanafunzi?
Uelewa wa hisia za wengine
Uso wa kila unayekutana naye hubeba mawimbi yenye ujumbe usiosemwa wazi. Ujumbe huu unaweza kuwa wa kupoteza, kufurahia, kutishwa, kuumizwa, kukerwa, kushangazwa, kufedheheshwa, kuhurumiwa, kuomba msaada na kadhalika.
Uwezo wa kuyasoma mawimbi haya, kuyaheshimu na kuchukua hatua stahiki kufanyia kazi ujumbe wake ndio unaoitwa ushirikieli.
Uwezo huu humaanisha uwezo wa kumheshimu mtu kwa kiwango kinachokufanya utake kuelewa anachopitia, anachofikiri, anavyotafsiri mambo, na kubwa zaidi anavyojisikia bila kujaribu kumpuuza, kumtafsiria hisia zake kwa namna unavyotaka ajisikie wala kujaribu kumbadilisha afikiri kama wewe, aone kama wewe, ajisikie kama wewe.
Ushirikieli ni ushahidi mzuri kuwa una afya njema ya akili, unampenda mtu, unamchukulia kama binadamu anayestahili heshima na staha hata katika mazingira ambayo anakuwa amekosea, amekuudhi au anafikiri tofauti na wewe.
Program ya umahiri hisia inalenga kukuza uwezo wa watoto kuelewa hisia za wengine na matokeo yake ni kupunguza ugomvi, migogoro na mitafaruku mingine inayotokana na uwezo mdogo wa kuelewa hisia.
Katika mazingira ambayo familia inaanza kushindwa kuwa eneo la kujenga umahirihisia, shule zina nafasi ya kuweka mfumo madhubuti wa kumsaidia mtoto kuelewa na kurekebu hisia, zake, kujenga motisha na kuelewa hsiia za wengine kama hatua muhimu ya kujenga kizazi cha watoto wenye utimamu wa afya ya akili.
Tusipochukua hatua, ipo hatari ya kuelimisha vichwa vya watoto wetu, ilhali tukisahau kuelimisha mioyo yao. Elimu isiyogusa mioyo ya watoto wetu, kwa hakika, haiwezi kuwa elimu bora.
Mwandishi ni mhadhiri wa saikolojia na mtafiti wa ukuzaji wa elimuhisia wa Chuo Kikuu cha Dodoma.