Faraja Kotta: Miss Tanzania aliyeleta mageuzi ya elimu, teknolojia kwa mtoto wa kike

Kupitia Teacher Kidevu App, mfumo wa akili bandia uliotengenezwa na Shule Direct ili kusaidia walimu na wanafunzi kupata maudhui ya elimu kwa njia rahisi na bunifu, Faraja Nyalandu Kotta ameweka historia ya mabadiliko ya kielimu nchini Tanzania.
Lakini nyuma ya mafanikio haya ya kiteknolojia, kuna safari ya kipekee ya mwanamke ambaye alianza kujulikana kupitia taji la Miss Tanzania mwaka 2004.
Faraja si jina geni katika tasnia ya urembo, lakini kwa sasa amegeuka kuwa mama, mjasiriamali na kiongozi wa mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu.
“Nilipopewa taji la Miss Tanzania nilianza kujiona mtu mwenye wajibu kwa jamii,” anasema Faraja kwa sauti ya utulivu lakini iliyojaa msisitizo wakati akihojiwa na Kituo cha luninga cha CNN akitambuliwa kama mmoja wa walioleta mabadiliko barani Afrika.
Katika mahojiano hayo yaliyorushwa na CCN na kuendeshwa na mtangazaji maarufu, Larry Madowo yamemtambulisha Faraja kama mwanamageuzi barani Afrika.
Kupitia nafasi yake hiyo, alisafiri sehemu mbalimbali, kushiriki katika shughuli za kijamii na kufanya kazi na taasisi tofauti na kupata uzoefu uliomfungua macho kuhusu changamoto zinazowakabili Watanzania, hasa katika elimu.
Baada ya ushindi wake kwenye Miss Tanzania, Faraja aliendelea na masomo ya shahada ya sheria nchini Uingereza. Akiwa mama wa watoto wawili na mke, changamoto zilikuwa nyingi.
“Ilikuwa kazi kubwa kusoma nikiwa na familia. Nilijifunza kufanya yote kwa kutumia teknolojia,” anakumbuka.
“Hapo ndipo alipoanza kutambua nguvu ya teknolojia katika kubadilisha maisha, hasa kwa wanawake na wazazi wanaotafuta elimu.”
Aliporejea Tanzania, alikuta hali ya elimu ikiwa tete ufaulu wa wanafunzi wa sekondari ulikuwa umeshuka kwa kiwango kikubwa.

“Niliamini kuna haja ya kusaidia wanafunzi na walimu kwa kuwapatia vifaa vya kujifunzia kwa njia ya teknolojia,” anasema.
Hapo ndipo wazo la Shule Direct lilipozaliwa mwaka 2013, jukwaa la kidijitali linalotoa maudhui ya elimu kwa wanafunzi na walimu kupitia mtandao.
“Shule Direct ni kama darasa mkononi unapata vitabu, maswali, na maelezo moja kwa moja, bila kulazimika kuwa darasani,” anaeleza.
Mwaka 2018, Shule Direct ilianzisha Teacher Kidevu, mfumo wa akili bandia (AI) unaowezesha usambazaji wa maudhui ya elimu kwa njia rahisi na inayofikika hata maeneo ya mbali. Mfumo huo sasa ni sehemu muhimu ya jukwaa hilo.
Mtandao wa Shule Direct mpaka sasa una watumiaji karibu milioni tano na imepakuliwa na watu zaidi ya 300,000.
Kuzaliwa kwa NdotoHub
Mbali na elimu, Faraja pia ni mwanzilishi wa NdotoHub, mradi unaolenga kuwawezesha wasichana na wanawake vijana katika ujasiriamali na ubunifu. NdotoHub hutoa mafunzo, mitaji na ushauri kwa wanawake wajasiriamali na wanaoanzisha mashirika au kampuni.
Kutambuliwa duniani
Juhudi zake hazikupita kimya. Mwaka 2020 World Economic Forum ilimtambua Faraja kama miongoni mwa wanawake wanaoongoza mabadiliko kupitia teknolojia. APP ya Shule Direct imepakuliwa zaidi ya mara 2,000, huku matumizi yake yakiongezeka kila siku.

“Naamini kila mtu ana uwezo wa kufanikiwa, tunahitaji maarifa na elimu bora ili kila mtu atimize ndoto zake” anasema Fraja.