Uchakavu wa miundombinu elimu wakithiri Morogoro

Muktasari:
- Juma la elimu lahitimishwa mkoani Morogoro, huku upungufu wa na uchakavu wa miundombinu ya shule ikiwa ni changamoto iliyoibuka katika shule za Morogoro vijijini zilizofikiwa wakati wa maadhimisho hayo.
Morogoro. Mtandao wa Elimu Tanzania (TENMET) umetoa wito kwa Serikali kwa kushirikiana na jamii pamoja na wadau katika ujenzi wa miundombinu ya elimu ili kuondoa adha ya upungufu wa vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, majengo ya utawala na matundu ya vyoo.
Wito huo umetolewa leo wakati wa kuhitimishwa kwa maadhisho ya juma la elimu yaliyokuwa yakifanyika katika kata ya Mvuha, mkoani Morogoro.
Mwenyekiti wa bodi wa TENMET, Faraja Nyalandu amesema baada ya kutembelea shule kadhaa zilizo ndani ya wilaya ya Morogoro vijijini imebainika kuwa elimu bado iko chini kutokana na changamoto lukuki ikiwemo upungufu wa miundombinu hiyo.
Amesema katika maadhimisho hayo walitembelea shule za msingi na sekondari ikiwemo Shule ya Msingi Njia nne, Duthumi, Bonye, na Magogoni, wa Bwakira Chini na Selembali ambako kote kulikuwa na upungufu na uchavu wa miundombinu.
“Tumekutana na changamoto za upungufu wa madarasa, matundu ya vyoo na shule nyingine majengo yake ni chakavu yanahatarisha usalama wa wanayoyatumia.
“Wanamtandao kupitia mashirika hayo wameangalia kwa namna gani kila moja itaweza kusaidia katika maeneo hayo ila kwa kuanzia tutasaidia ujenzi wa vyoo vya walimu shule ya Bonye, ujenzi wa sakafu shule ya njia nne na tutachangia madawati shule ya msingi Duthumi,” amesema Faraja.
Mbali na hilo Faraja kwa niaba ya mtandao huo ameshauri jamii iendelee kuhamasishwa kuchangia huduma ya chakula na lishe bora, maji safi na salama shuleni.

Juma la elimu mwaka 2023 limebebwa na kauli mbiu ni: ‘Tuboreshe Uwekezaji wa Rasilimali za ndani kwenye elimu kwa maendeleo endelevu’ ikilenga kuhamasisha uboreshaji elimu kwa kutumia rasilimali za ndani ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu.
Katika maadhimisho haya shughuli mbalimbali zilifanyika ikiwa ni pamoja kuandaa darasa la mfano la elimu jumuishi ya awali ambalo lipo katika shule ya msingi Mvuha.
Washiriki pia walipata fursa ya kushiriki kazi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa bweni la wasichana wenye ulemavu katika Shule ya Msingi Mvuha.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo mratibu wa miradi wa shirika la lisilo la kiserikali la kampeni ya elimu wa watoto wa kike (CAMFED) Wilaya ya Morogoro Stumai Kaguna amesema hamasa bado inahitajika katika kuwafanya wanafunzi ndani ya wilaya hiyo wabaki shuleni.
“Morogoro ni miongoni mwa mikoa ambayo CAMFED inatekeleza miradi mbalimbali ya kuwawezesha watoto kupata elimu, kupitia mradi wa stadi za maisha na dunia yangu bora tunawawezesha watoto kujitambua na kuona umuhimu wa elimu.
“Lengo letu ni kupunguza tatizo la utoro na kuwafanya watoto wakabiliane na changamoto wanazokutana nazo kwa kufanya hivi tutaweza kuongeza mahudhirio shuleni na hata kiwango cha ufaulu kitakuwa juu,” amesema Stumai.