Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bosi Ruwasa, wenzake walimwa faini, waamriwa kurejesha Sh53.9 milioni

Muktasari:

  • Meneja wa Ruwasa Kakonko na wenziye wawili wamehukumiwa kulipa faini ya Sh4 milioni na kurejesha zaidi ya Sh53.9 milioni zilizofanyiwa ubadhirifu.

Kigoma. Mahakama ya Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, imewahukumu watu watatu, akiwemo Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) wa wilaya hiyo, Benjamin Brighton kulipa faini ya Sh4 milioni na kurejesha zaidi ya Sh53.4 milioni baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya rushwa na uhujumu uchumi.

Wengine waliotiwa hatiani mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ambilike Kyamba katika shauri la uhujumu uchumi ni Fundi Sanifu wa Ruwasa wilayani humo, Faraja Kalokola na Mkurugenzi wa Kampuni ya Chiganda Construction Limited, Johansen Muganyizi.

Washtakiwa hao kwa pamoja walishitakiwa kwa makosa ya matumizi mabaya ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri ili kujipatia manufaa yao binafsi, ubadhirifu na ufujaji, matumizi mabaya ya mamlaka pamoja na ushawishi kinyume na vifungu vya 22, 23 (1), 28 (1), 31 na 33 vyote vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura namba 329 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Iliyosomwa pamoja na aya ya 21 kifungu cha 57(1) na kifungu 60 (2) vya Sheria ya Udhibiti wa Makosa ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa Sura namba 200, marejeo ya mwaka 2022.


Akitoa hukumu hiyo Aprili 8, 2025, Kyamba alisema washtakiwa hao wanatakiwa kulipa fedha hizo ndani ya miezi sita kwa kuwa waliisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh53.9 milioni, kwa ajili ya miradi ya maji kwenye Halmashauri  ya Wilaya ya Kakonko kupitia Ruwasa.

Awali, Mwendesha Mashitaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Kigoma, Jackson Lyimo aliiomba  Mahakama kutoa adhabu kali kwa watuhumiwa ili kudhibiti makosa kama hayo katika miradi ya Serikali inayotekelezwa katika jamii.

Hata hivyo, tayari wamelipa faini hiyo na kutanguliza Sh26 milioni ya fedha wanazotakiwa kuzirejesha huku kiasi kilichosalia kikitakiwa kulipwa ndani ya miezi sita.