Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ukiziona ishara hizi kapime, ni dalili za magonjwa ya ngono

Muktasari:

  • Baadhi ya magonjwa hayo ambayo mtu anaweza kuishi nayo mpaka miaka 20, huleta athari katika mirija ya uzazi na kusababisha PID, huku kwa mwanaume ikiathiri uzalishaji na ubora wa mbegu na njia ya kupitisha mbegu hizo.

Dar es Salaam. Wakati takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zikionyesha mamilioni ya watu wanaishi na magonjwa ya ngono (STDs) bila kujijua, wataalamu wa afya wametaja dalili za mtu mwenye magonjwa hayo.

Wametaja miongoni mwa magonjwa ambayo mtu anaweza kuishi nayo kwa muda mrefu ni pamoja na kaswende (mpaka miaka 20) kisonono na klamidia (jamii ya fangasi) ambayo husababisha ugonjwa wa PID na ugumba kwa wanawake.

Kisonono kimetajwa pia huathiri njia ya kupitisha mbegu kwa mwanaume lakini kuathiri uzalishaji na ubora wa mbegu.

Kauli ya wataalamu hao, ipo sambamba na ripoti ya utekelezaji wa mikakati ya sekta ya afya duniani juu ya maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU), homa ya ini na magonjwa ya ngono ya mwaka 2022–2030 ya WHO inayoonyesha ongezeko la magonjwa ya zinaa hususani nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Ripoti hiyo inaonyesha magonjwa manne ya zinaa yanayotibika yaani kaswende, kisonono, klamidia na trichomoniasis, husababisha zaidi ya maambukizi milioni moja kila siku duniani.


Dalili

Umewahi kupata kidonda usichokielewa sehemu za siri au mdomoni? Uchafu au fangasi wanaojirudia ukeni? Wataalamu wanashauri uhudhurie katika maabara zenye ubora ufanye vipimo vya magonjwa haya.

Mtaalamu wa Afya ya Jamii, Dk Ali Mzige anasema kuna dalili kadhaa zinazoashiria mtu amepata au anaishi na maambukizi ya ugonjwa mmojawapo wa ngono.

Amezitaja baadhi ya dalili kuwa ni pamoja na kupata kidonda kisichoeleweka na kisicho na maumivu sehemu za siri ambacho huja na kupotea na nyakati zingine hutokea mdomoni. Anasema wengine wanapata vipele kwenye ngozi (rushes).

“Pia, mgonjwa kama ana kisonono, hutoa uchafu njia ya haja ndogo na kwa mwanamke anatoa uchafu ukeni, kuna wengine wanaweza kupata maumivu wakati wa haja ndogo kutoa uchafu sehemu ambayo haikuwa na tatizo awali,” amesema Dk Mzige.

Amesema jinsi mgonjwa anavyokaa kwa muda mrefu anapata ugumba. Ametaja dalili nyingine ni wale ambao wamepata mtoto ana tatizo la kiafya, mimba kutoka na wengine hupata matatizo ya akili.

Dk Mzige amesema kaswende ni mbaya zaidi kwani husambaa mwili mzima na kufika mpaka kwenye ubongo na mara nyingi athari zake ni kumletea mgonjwa matatizo ya afya ya akili.

“Wengine wanaweza kupata magonjwa ya zinaa kama kisonono kwenye koo na kaswende kwenye ulimi, haya magonjwa mengine ya zinaa baadaye yanaleta saratani hasa ya njia ya haja kubwa au ya uke na nyakati zingine mtoto kuzaliwa na matatizo ya macho,” amesema na kuongeza:

“Kwa sasa magonjwa ya ngono yanaongezeka na wengi wanaishi nayo bila kujua, wengine wamejifungua watoto wadogo, mtoto anapata changamoto ya kutokwa na tongotongo, hiyo ni dalili mama na baba wakachukuliwe vipimo maabara.”

Amesema kaswende huharibu mimba mara kwa mara pindi zinapotungwa na watoto kufia tumboni, huku pia ikiathiri afya ya moyo.

Kwa mujibu wa Dk Mzige, ugonjwa wa kaswende ulikuwepo miaka mingi na baadaye walipogundua dawa walianza kutibu kwa penisilin.

Amesema mwanamke yupo kwenye hatari zaidi ya kupata magonjwa hayo kwa kuwa hupata kirahisi zaidi ikilinganishwa na mwanaume, akibainisha kuwa ugonjwa wa kisonono ni rahisi mwanaume kuona dalili mapema na kujitibu, ingawaje wapo ambao hawaoni mapema dalili.

“Wananchi wanahitaji uelewa, wengi sasa hivi wanatafuta dawa za kienyeji, wanatumia dawa zisizo sahihi za mitandaoni wanajitibu kesho ugonjwa umerudi tena. Tunashauri wafike vituo vya afya wapime katika maabara zenye weledi wao na wapenzi wao, asijitibu peke yake hatafanya kitu hapo,” amesema Dk Mzige.

Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake katika Hospitali ya Salaaman, Abdul Mkeyenge amesema wengi wamekuwa wakijifichia katika maambukizi ya njia ya mkojo kutibu magonjwa ya ngono.

“Wengi hasa wanawake hulalamika kutokwa na uchafu sehemu za siri au majimaji, akinywa antibayotiki siku tano zile dalili zinapotea, mdudu bado yupo anaendelea kuathiri baada ya miezi kadhaa anapata PID kwa kuwa magonjwa ya ngono yamekaa muda mrefu,” amesema.

Amesema kaswende ina hatua zisizopungua nne na mojawapo ni kupata vipele sehemu za siri na kupotea, kupata muwasho au kidonda kisichopona au majimaji sehemu za siri.

Mtaalamu wa mshauri wa masuala ya afya, Dk Elisha Osati amesema Serikali pamoja na wadau wanaohusika wamejisahau na kwamba wanapaswa kusisitiza masuala ya kupima na kujipima na kuchukua tahadhari.


Hali halisi nchini

Takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha idadi ya waliopimwa na kubainika kuwa na kaswende pekee ilipanda kutoka 16,015 mwaka 2017 hadi 26,592 mwaka 2019. Kaswende iligundulika zaidi kwa wajawazito waliopimwa na kupata matibabu na idadi yao iliongezeka kutoka 10,049 hadi 18,298 katika kipindi hicho.

Takwimu za matibabu ya kaswende miongoni mwa wanawake waliogunduliwa wanaohudhuria kliniki, ilikuwa asilimia 17.3, asilimia 22.4 na asilimia 25 katika mikoa ya Tanga, Dodoma na Dar es Salaam na asilimia 100 katika mikoa ya Kagera, Geita, Mara na Simiyu.


Ukweli kuhusu STD

Takwimu zinaonyesha kuwa maambukizi ya magonjwa ya zinaa yanaendelea kuongezeka katika maeneo mengi ya dunia. Mwaka 2022, nchi wanachama wa WHO waliweka lengo la kupunguza maambukizi mapya ya kaswende kwa watu wazima kutoka milioni 7.1 hadi 0.71 milioni ifikapo mwaka 2030.

Hata hivyo, mwaka huohuo, maambukizi mapya yaliongezeka na kufikia milioni 8 kwa watu wazima wenye umri wa miaka 15-49. Ongezeko kubwa lilishuhudiwa katika kanda ya Amerika na Afrika.


Dondoo

1.       Zaidi ya maambukizi milioni 1 ya magonjwa ya ngono yanayotibika hutokea kwa siku (saa 24) duniani kwa watu wenye umri wa miaka 15–49.

2.       Mwaka 2020, kulikuwa na makadirio ya maambukizi mapya milioni 374 ya aina nne za magonjwa ya ngono yanayotibika; klamidia jamii ya fangasi (milioni 129), kisonono (milioni 82), kaswende (milioni 7.1) na trikomonia (milioni 156).

3.       Mwaka 2022, watu wazima milioni 8 waliambukizwa kaswende.

4.       Zaidi ya watu milioni 500 wenye umri wa miaka 15–49 wanakadiriwa kuwa na maambukizi ya virusi vya herpes (HSV).

5.       Maambukizi ya virusi vya HPV yanahusiana na zaidi ya vifo 311,000 vya saratani ya mlango wa kizazi kila mwaka.

6.       Wanawake wajawazito milioni 1.1 walikadiriwa kuwa na maambukizi ya kaswende mwaka 2022, na kusababisha zaidi ya matokeo mabaya ya uzazi 390,000.

7.       Magonjwa ya ngono huathiri moja kwa moja afya ya uzazi na ya kijinsia kwa kusababisha unyanyapaa, ugumba, saratani, matatizo ya ujauzito na pia huongeza hatari ya kuambukizwa VVU.

8.       Ustahimilivu wa dawa ni tishio kubwa katika juhudi za kupunguza mzigo wa magonjwa ya ngono duniani.

9.       Maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yanaweza kusababisha kuharibika kwa mimba, vifo vya watoto wachanga, uzito mdogo wa kuzaliwa, uchungu wa mapema, ugonjwa wa macho kwa watoto wachanga na ulemavu wa kuzaliwa.

10.   Kisonono na klamidia husababisha ugonjwa wa PID na ugumba kwa wanawake.