Ongezeko magonjwa ya ngono, homa ini yaiamsha Serikali

Muktasari:
- Ongezeko la maambukizi ya magonjwa ya ngono na homa ya ini, yameifanya Wizara ya Afya wameboresha Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi na kuja na Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini (NASHCoP).
Dar es Salaam. Kutokana na ongezeko la magonjwa ya ngono na homa ya ini nchini, Wizara ya Afya nchini Tanzania, imezindua Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini (NASHCoP), ili kupambana na magonjwa hayo ya kuambukiza.
Kuanzishwa kwa mpango huo jumuishi, kumekuja miaka 35 tangu Tanzania ianzishe Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi Tanzania (NACP) mwaka 1988, ikiwa ni miaka mitano baada ya Ukimwi kuingia nchini mwaka 1983.
Akizungumza leo Ijumaa, Novemba 24, 2023 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema nguvu kubwa iliwekwa katika kupambana na Ukimwi na kuyapa msukumo mdogo magonjwa ya ngono.
"Nguvu kubwa tuliiweka katika mapambano ya Ukimwi, tumepata mafanikio makubwa eneo hilo na Desemba Mosi tutapata rasmi takwimu mpya, tumefanikiwa kupunguza vifo, maambukizi mapya na mafanikio yamechangiwa kutokana na jitihada za Serikali na wadau, kwa kuongeza vituo, tiba na kushirikisha jamii," amesema.
Hata hivyo, Waziri Ummy amesema bado kuna kazi ya kufanya kupunguza maambukizi mapya kwa vijana, pamoja na kutokomeza maambukizi mapya kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Waziri huyo mwenye dhamana ya afya nchini, ameweka wazi kuwa nchi ililegalega kushughulikia magonjwa ya ngono, hasa uhamasishaji wa ngono kwani takwimu za maambukizi ya magonjwa ya ngono na homa ya ini ni makubwa.
"Tuna tatizo la magonjwa ya ngono nchini ambayo yanachangia kudhorotesha afya za Watanzania na kurahisisha maambukizi ya VVU na homa ya ini. Nilipoingia Wizara ya Afya miaka saba iliyopita, niliwaambia tusisubiri siku ya homa ya ini kutoa tamko, bali lazima tupambane na huu ugonjwa,” amesema
"Leo nafarijika angalau zile ndoto zimefikia, tunazindua mpango huu utakaoshughulikia homa ya ini, ukimwi na magonjwa ya ngono. Nilisema lazima tuanze na watoa huduma za afya mpaka sasa tumeweza kuwafikia watumishi wa afya 23,000 waliopata chanjo kati ya 110, 000," amesema
Amesema baada ya kuanzishwa kwa mpango huu, watawafikia walio katika mazingira hatarishi wote wapate chanjo na homa ya ini.
Akizungumzia magonjwa ya ngono amesema takwimu zinapanda mwaka hadi mwaka.
"Kati ya magonjwa yanayoongoza watu kujinunulia dawa za antibiotiki ni magonjwa ya ngono kwa sababu ya unyanyapaa, Watanzania nendeni kwa wataalamu mpime epukeni kutumia dawa kiholela bila kupimwa hususani antibiotiki," amesema.
Amesema kuna dawa zinauzwa kuliholela zikiwemo zinazodawa za maambukizi ya via vya uzazi PID na kuonya kwamba uchafu utokao ukeni waweza kuwa ugonjwa wa ngono, saratani ya shingo ya kizazi.
Amesema ongezeko la watu kutoshika mimba pia linachangiwa na magonjwa ya ngono, na kuwaagiza wataalamu kulifanyia kazi eneo hilo.
"Matarajio mpango huu utakwenda kuongeza hamasa, asilimia kubwa ya wanaogundulika na vvu na ambao hawajaanza dawa wana magonjwa ya ngono na ukiangalia wenye magonjwa ya ngono wengi wana maambukizi ya vvu, na takwimu zilituonyesha waliotokwa uchafu na vidonda sehemu za siri walikuwa na vvu," amesema.
Amesema matumaini ya mpango jumuishi ni kupunguza gharama, kuwafikia wananchi wengi na kutaleta ufanisi zaidi.
Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya afya na ukimwi, Stanslaus Nyongo amesema program hiyo jumuishi inakwenda kurahisisha utoaji wa huduma za afya katika janga hilo kubwa.
"Suala hili wabunge tumelitaka miaka mingi, wananchi wapate huduma kwa urahisi, hii inakwenda kuokoa muda na kupunguza gharama, tutaendelea kushiriki kupitisha mipango mbalimbali makini kama hii pamoja na kupitisha bajeti lakini kuzisimamia hizi programu," amesema Nyongo
Naye Mkurugenzi wa huduma za afya Ofisi ya Rais-Tamisemi, Rasheed Mfaume amesema mpango huo lazima Serikali ishirikiane na wadau wengine wakiwemo wanasiasa.
"Kila mmoja ngazi zote tungependa afua hizi ziwafikie wananchi wa ngazi za chini katika vijiji, kata kule walipo kwa kutumia huduma mkoba. Tuna vituo, watumishi na uwepo wa miundombinu," amesema Dk Mfaume.
Akielezea jinsi mpango huo utakavyofanya kazi, Mratibu wa huduma za Ukimwi Idara ya Afya, ustawi wa jamii na lishe Tamisemi, Dk Neema Mlole amesema:"Tunaongeza huduma ya magonjwa ya ngono na homa ya ini,
tutaendelea kutoa huduma kwa kuzingatia miongozo na sera kwa kupambana na magonjwa matatu kwa wakati mmoja."
Amesema mkakati huo unawapa utekelezaji ambao utakua mzuri zaidi hasa kwa vituo vya afya.