Prime
Mwanamke aliyemuua mfanyakazi wake wa ndani ahukumiwa kifo

Muktasari:
- Licha ya kujitetea kuwa marehemu alijinyonga, ushahidi wa madaktari na mpelelezi ulithibitisha aliuawa kwa kupigwa na kunyongwa. Jaji asema mshtakiwa alitoa taarifa za uongo na alionekana kuwa na dhamira ovu.
Dar es Salaam. Licha ya Diana Joseph Sabhai kudanganya jina lake halisi, mwanamke huyo hakuweza kukwepa mkono wa sheria, baada ya kuhukumiwa adhabu ya kifo kwa kumuua mfanyakazi wake wa kazi za ndani, Aneth Kassim.
Mauaji hayo yalitokea Februari 9, 2023 eneo la Tabata Kimanga, jijini Dar es Salaam, na baada ya kubaini ‘House Girl’ amekata kauli, alimkimbiza Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, ili kuokoa maisha yake.
Hata hivyo, Diana hakuweza kupangua ushahidi wa Jamhuri uliomwelemea, na ni kutokana na uzito wa ushahidi huo, Jaji Awamu Mbagwa wa Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Dar es Salaam, amemtia hatiani na kumhukumu adhabu ya kifo.
Hukumu hiyo iliyotolewa Aprili 4, 2025 na kupakiwa katika mtandao wa mahakama jana Jumanne, Aprili 8, 2025, iliegemea ushahidi wa mashahidi watano wa Jamhuri na kielelezo kimoja ambacho ni ripoti ya daktari ya uchunguzi wa kifo cha marehemu.
Katika hukumu yake, Jaji Mbagwa alisema baada ya kupitia ushahidi wa Jamhuri na utetezi wa mshtakiwa, ameridhika kuwa Jamhuri ilithibitisha shtaka hilo pasipo kuacha shaka kuwa mshtakiwa ndiye mhusika wa mauaji hayo.
“Ni matokeo yangu yasiyo na unafiki kuwa upande wa Jamhuri ulithibitisha shtaka hili pasipo kuacha shaka. Utetezi wa mtuhumiwa ulikuwa wa ushabiki tu ambao haukuleta shaka kwenye ushahidi wa Jamhuri,” alisema.
Tukio lilivyotokea
Kulingana na ushahidi wa upande wa mashtaka, ni kuwa Februari 9, 2023 akiwa eneo la Tabata Bima akisubiri wateja, dereva teksi, Daniel Sanga alipokea ombi la online la mshtakiwa akihitaji huduma.
Mshtakiwa alimtaka dereva huyo afanye haraka kumfuata kwa kuwa ana mgonjwa aliyetaka kumwahisha Hospitali ya Muhimbili, na alipofika, mshtakiwa alisema ana mgonjwa aliyekuwa ameanguka katika moja ya vyoo vya ndani.
Hivyo, alimuomba dereva teksi amsaidie kumbeba, ambapo alifanya hivyo, lakini wakati anambeba alikuwa amepoteza fahamu. Mshtakiwa alimwambia waende moja kwa moja Muhimbi kwa kuwa ana daktari wao wa familia.
Walienda moja kwa moja Kitengo cha Dharura (emergency) ambapo mshtakiwa alijiandikisha kuwa anaitwa Grace Joseph badala ya jina lake halisi la Diana Joseph na akaomba watumishi wa Muhimbili wamsaidie mgonjwa wake.
Hata hivyo, wafanyakazi wa hospitali walipofika kwenye gari kwa ajili ya kumchukua mgonjwa, walibaini alikuwa tayari ni marehemu, na hivyo mmoja wao, Prosper Ndahiyize akaenda kumwita daktari wa zamu.
Dk Hebert Mshana, aliyekuwa shahidi wa tano, alienda kwenye gari ile, na alipomchunguza mgonjwa aliyeitwa, alibaini alikuwa ameshafariki dunia.
Shahidi huyo alieleza kuwa mshtakiwa alijitambulisha kwake kama Grace Joseph na kudai ni mama wa kambo wa marehemu, na kwamba marehemu alianguka kwenye choo—maelezo ambayo daktari huyo aliyatilia mashaka.
Alitoa taarifa polisi ambao walifika Muhimbili muda mfupi baadaye na kukuta mwili wa marehemu ukiwa bado kwenye gari, ambapo mshtakiwa akajitambulisha kwa Koplo John mwenye namba H87 kuwa anaitwa Grace Joseph.
Lakini ilibainika jina lake halisi si Grace bali ni Diana, baada ya askari kumtaka ampe kitambulisho chake, na ni kutokana na kujikanganya huko na uchunguzi wa awali, ofisa huyo wa polisi alibaini michubuko kwenye shingoni ya marehemu.
Uchunguzi wa mwili wa marehemu uliofanywa na Dk Eda Vuhahula ulibaini kuwa kucha za marehemu zilikuwa na rangi ya bluu, ambayo ni dalili kuwa kifo cha marehemu kilisababishwa na kupata shida ya kupumua (respiratory distress).
Pia katika uchunguzi wake, shahidi huyo alibaini kuwepo kwa majeraha mabichi ya michubuko katika mikono na mapaja, inayothibitisha yalitokana na kuhangaika au kupigana, na kufuta kabisa uwezekano kuwa marehemu alijinyonga.
Mpelelezi alimaliza kila kitu
Katika ushahidi wake, shahidi wa tatu wa Jamhuri, E3411 Stesheni Sajini Lwanga aliyekuwa mpelelezi, alieleza kuwa katika upelelezi wake aliridhika marehemu hakujinyonga kama ambavyo mshtakiwa alidai.
Shahidi alitoa sababu tatu kufikia hitimisho hilo, kuwa ni pamoja na kitendo cha kujitambulisha kwa jina la uongo hospitalini na mshtakiwa kutoa hadithi mbili tofauti kuhusu nini kinaweza kuwa kiini cha kifo cha marehemu.
Hakukuwa na mbubujiko wa damu kwenye vein, na siku ya tukio walikuwa wawili tu ndani ya nyumba—mshitakiwa na marehemu.
Kulingana na shahidi huyo, awali mshtakiwa alimweleza dereva teksi, aliyekuwa shahidi wa kwanza, na Dk Mshana, aliyekuwa shahidi wa tano, kuwa marehemu alikuwa amedondoka chooni, lakini akabadili na kusema alimkuta amejinyonga.
Sababu ya tatu ni kuwa kulikuwa hakuna mbubujiko wa damu kwenye vein, na kwamba kwa kuwa siku ya tukio walikuwa watu wawili tu ndani ya nyumba, hakuna mtu mwingine aliyesababisha kifo hicho zaidi ya mshtakiwa.
Alivyojitetea kortini
Katika utetezi wake, mshtakiwa alikana kusababisha kifo cha marehemu na kufafanua kuwa siku ya tukio alikuwa na miadi katika Hospitali ya CCBRT, hivyo aliamka na kwenda hadi kituo cha mabasi, ambapo alichukua teksi.
Alieleza kuwa wakati anaondoka, alimuacha marehemu nyumbani akiwa bukheri wa afya, lakini akiwa njiani kwenda CCBRT, alipokea simu ya mtoto wake akimkumbusha kuhusu fedha ya ada wanayodaiwa.
Fedha hizo alikuwa ameziacha nyumbani, hivyo alishuka kwenye teksi na kuchukua bodaboda iliyomwahisha nyumbani, lakini alipofika, alimwita marehemu lakini hakuitikia, hivyo akaamua kufungua geti kwa kutumia ufunguo wa akiba.
Alienda moja kwa moja kwenye chumba chake cha kulala na kuchukua fedha hizo, na kabla ya kuondoka akapita kwenye chumba cha house girl wake, lakini hakumuona. Akaendelea kumwita kwa sauti, lakini kulikuwa hakuna majibu.
Mwisho, akaamua kwenda choo cha nje na kumkuta mfanyakazi wake huyo amejitundika (amejinyonga), kwa kutumia ndoo mbili za maji alimshusha na kutafuta usafiri na kumwahisha Hospitali ya Muhimbili.
Kwanini Diana ana hatia
Katika hukumu yake, Jaji Mbagwa alirejea ushahidi wa daktari akisema kuwa pamoja na kuwa ni wa kitaalamu, ushahidi wa mpelelezi unathibitisha dhamira ovu ya mshtakiwa.
Jaji akarejea hitimisho la mpelelezi aliyetoa sababu tatu za kwanini mshtakiwa ndiye aliyehusika na mauaji hayo, ikiwamo kutaja jina la uongo na kuwa na simulizi mbili tofauti kuhusiana na tukio moja: kuanguka chooni na kujinyonga.
“Katika kesi hii, tuna ushahidi wa daktari ambaye anasema kiini cha kifo cha marehemu hakikusababishwa na kunyongwa. Ninafahamu kanuni inaeleza kuwa mahakama haibanwi na maoni ya kitaalamu kufikia hitimisho,” alisema Jaji.
Hata hivyo, Jaji alisema lazima kuwe na sababu nzuri za kukataa ushahidi wa aina hiyo, lakini kwa jinsi alivyofuatilia wakati akitoa ushahidi wake kortini, ameridhika kuwa ni mtaalamu aliyebobea katika fani yake, hivyo anashawishika kumwamini.
Jaji alisema, pamoja na kuzingatia kuwa ushahidi wote uliotolewa ni wa mazingira, kuna haja ya kuangalia matendo ya mshtakiwa mwenyewe na kujiuliza: je, yale aliyokuwa akiyafanya yanamfanya aonekane hana hatia ya mauaji?
Kulingana na Jaji, ushahidi wa Daniel Sanga na Dk Hebert Mshana unaeleza kuwa mshtakiwa aliwaambia kuwa marehemu alikuwa ameanguka chooni, lakini baadaye alibadili hadithi hiyo na kudai alimkuta chooni akiwa amejinyonga.
Hoja ya pili ni kuwa mshtakiwa alimweleza shahidi wa kwanza kuwa alimpeleka marehemu Hospitali ya Muhimbili kwa kuwa ana daktari wa familia, lakini kwenye utetezi alisema alimpeleka huko kutokana na hali yake mbaya.
Lakini Jaji alisema pia mshtakiwa hakutaka kumshirikisha suala hilo kwa jirani yake yeyote yule au kiongozi wa mtaa anaoishi, licha ya tukio hilo kuwa la kuogofya, lakini ni mshtakiwa peke yake ndiye alikuwa akiishi na marehemu ndani.
Ni kutokana na sababu hizo na kwa kuzingatia utetezi wa mshitakiwa, Jaji alisema upande wa mashtaka ulikuwa umethibitisha shtaka hilo bila kuacha mashaka, hivyo anamhukumu adhabu pekee, nayo ni kunyongwa hadi kufa.