Jaji Mtungi aichambua No reforms, no election

Muktasari:
- Msajili wa vyama vya siasa nchini Tanzania, Jaji Francis Mutungi amezungumzia operesheni ya No reforms, no election akisema hakuna mtu anayeweza kuuzuia uchaguzi mkuu usifanyike.
Dodoma. Msajili wa vyama vya Siasa nchini Tanzania, Jaji Francis Mutungi ameichambua operesheni ya No reforms, no election (bila mabadiliko hakuna uchaguzi) akisema bado haijavunja sheria ya vyama vya siasa huku akasisitiza uchaguzi 2025 upo palepale.
Jaji Mutungi ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Aprili 10, 2025 alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma baada ya kushiriki warsha ya wadau inayojadili namna ya kuzuia na kupambana na rushwa katika uchaguzi mkuu 2025.
Warsha hiyo imeandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru). Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Crispin Chalamila amefungua kongamano hilo ambalo vyombo vya ulinzi na usalama vimeshiriki ikiwemo taasisi za Serikali zinazohusiana moja kwa moja kwenye mambo ya uchaguzi.
Chadema inatekeleza azimio lililopitishwa na mkutano mkuu wa Januari 21, 2025 la No reforms, No election ambapo viongozi wa kitaifa akiwemo Tundu Lissu wamekuwa wakifanya mikutano ya kuelimisha wananchi.
Mikutano hiyo imefanyika Kanda ya Nyasa na Kusini yenye mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma. Viongozi wa chama hicho wamesema bila mabadiliko katika mifumo ya uchaguzi hawatasusia uchaguzi lakini watauzuia usifanyike.
Jaji Mutungi amesema hakuna anayeweza kuzuia uchaguzi wa mwaka huu kwa kuwa kinachosemwa ni matamshi ya wanasiasa majukwaani ambayo kila chama kinaweza kuwa na maana yake.
“Hakuna awezaye kuzuia uchaguzi kwa kutamka tu kwenye majukwaa, Chadema hawajavunja sheria na hata nilipokutana nao hivi karibuni walisema hawatakuwa tayari kuvunja sheria za uchaguzi,” amesema Jaji Mutungi.
Ametaja chombo kinachoweza kuzuia uchaguzi ni mahakamani, jambo alilosema hakuna aliyekwenda huko isipokuwa kinachoendelea ni matamshi ya midomoni mwa wanasiasa.
Kwa mujibu wa Jaji Mutungu hajasikia kwamba Chadema wamekwenda mahakamani kupinga uchaguzi licha ya kuwa wanao wanasheria wanaojua utaratibu mzima wa nini kifanyike, hivyo kinachoonekana ni kama wanafanya propaganda za kisiasa ambazo haziwezi kuwatia hatiani isipokuwa kama kutakuwa na maneno mengine ndani ya kauli zao.
“Mimi nitatafuta muda wa kuwaiteni kuzungumza kirefu zaidi kuhusu mambo haya, lakini kama ulivyosema mimi ndiye baba wa vyama vya siasa ni kweli, na kila chama kina haki ya kusikilizwa lakini siyo kuvunja sheria, sisi hatutegemei kama wanaweza kuvunja sheria,” amesema.
Aprili 8, 2025, Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu alitaja mambo sita ambayo yakifanyiwa kazi chama hicho kitashiriki uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu.
Lissu alitaja mambo hayo Jumanne ya Aprili 8, 2025 wilayani Namtumbo, mkoani Ruvuma kwenye mwendelezo wa ziara ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu ‘No Reforms, No Election.
“Tunahitaji kubadilisha mfumo wa uchaguzi kusiwe na mgombea anayepita bila kupingwa, pili hatutaki taratibu za uchaguzi zinazoruhusu wagombea wengine kuenguliwa, tatu hatutaki kuandikishwa watoto wadogo kwenye daftari la kudumu la mpigakura.
“Nne hatutaki kufanyiwa fujo tena kwenye kampeni zetu tunazofanya, tano mawakala wa vyama vyote wawe huru kufanya shughuli zao, ikiwemo kujua kura zao na kama hakuna mawakala uchaguzi usifanyike, sita hatutaki kuona uchaguzi unaotoa kafara za watu ili wapate uongozi,” alisema Lissu.
Ilichokisema Takukuru
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Crispin Chalamila amesema huu ni mwaka wa uchaguzi ambao huenda yakaibuka mambo mengi ikiwemo rushwa, hivyo kila mmoja anatakiwa kuwajibika kuzuia ili Watanzania wapate viongozi wenye sifa.
Chalamila amesema Takukuru peke yake haiwezi kushinda vita ya uchaguzi, lakini kupitia wadau na wananchi wenyewe vita hiyo itakuwa ni rahisi na ushindi utapatikana.
Amesema Takukuru inaingia maeneo mengi, hivyo kwa kutumia maofisa wake itahakikisha mchakato wa uchaguzi kuanzia uteuzi wa wagombea ndani ya vyama vya siasa unakuwa huru pasipokutumia rushwa.
“Sisi tunayo macho marefu, tunaweza kufika hata maeneo ambayo wengi hawategemei kuwa tungeingia lakini tupo, tutahakikisha kila hatua kwenye uchaguzi inakwenda vizuri,” amesema Chalamila.
Amewataka Watanzania kuwa makini na watu wanaotumia rushwa, kwani kufanya hivyo kutasababisha kuwepo kwa viongozi ambao hawatakuwa na mapenzi kwa wananchi wao na wala nguvu ya kuongoza.