Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mpasuko Chadema, G55 waliamsha

Muktasari:

  • Wanamtandao wa G55 waweka hadharani machungu wanayopitia Chadema. Waonya makada kukimbilia vyama vingine, ‘No reforms, no election’ kaa la moto.

Dar es Salaam. Kile kinachoonekana kuwa mpasuko ndani ya Chadema kimeendelea kukita kambi, huku muungano wa watia nia wa ubunge wanaounda umoja wa G55 ndani ya chama hicho, ukionya hatari ya makada kukimbilia vyama vingine kutafuta jukwaa la kugombea.

Sambamba na hilo, umebainisha vitisho vinavyowakabili kutokana na msimamo wao, ukidai watatu kati yao wameandikiwa barua na uongozi ngazi ya matawi wakitakiwa kujieleza kwa nini wasifukuzwe Chadema.

Mpasuko uliopo ni kati ya G55 unaounga mkono kufanyika mabadiliko lakini si kuzuia uchaguzi, dhidi ya uongozi na wanachama wengine wenye msimamo kuwa, pasipo mabadiliko hakuna uchaguzi.

Hayo yameibuliwa leo Jumapili, Aprili 6, 2025 na Mkurugenzi wa zamani wa Itifaki na Mambo ya Nje wa Chadema ambaye ni mmoja wa wanaounda G55, John Mrema alipozungumza na wanahabari akiwawakilisha wenzake zaidi ya 55.

Kwa kuwa dhamira ya kila mwanasiasa ni kuwania uongozi, amesema kuna hatari ya kukimbiwa iwapo hautampa nafasi ya kushiriki uchaguzi kutimiza lengo lake la kuwawakilisha wananchi.

“Chama kinaweza kuondokewa au kupoteza viongozi na wanachama wenye nia ya kuwania urais, ubunge na udiwani, pamoja na nafasi za viti maalumu. Kuna watu wapo kwenye vyama vya siasa kwa sababu wanataka kuwa viongozi ndiyo maana mtu akifungiwa mlango na chama hiki anakwenda chama hiki,” amesema.

Hata hivyo, Mrema alipoulizwa iwapo wanafikiria kuachana na nia za kugombea iwapo viongozi hawatakubali kubadili msimamo kuhusu ‘No reforms, no election’ amesema hawana mpango huo kama ilivyo kwa Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu.

“Kuna wakati mwenyekiti wetu alisikika hapa ametia nia ya nafasi fulani na chama kinasimamia ‘No reforms, no election’ mbona hajatangaza kuachana na nia yake, hakuna atakayeacha nia yake hapa,” amesema.


Wanatishwa

Mrema amesema kutokana na hatua yao ya kuwashauri viongozi kuhusu ‘No refoms, no election’ wameanza kutishwa na baadhi yao wameandikiwa barua wakitakiwa kujieleza.

Amekitafsiri kitendo hicho kuwa dalili ya uongozi kuminya uhuru wa maoni wa wanachama wake, jambo alilodai ni hatari ndani ya chama hicho na litakikosesha uhalali wa kuikosoa Serikali iwapo itafanya hivyo.

Wakati Mrema akisema hayo, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Samwel Welwel ametangaza kuwachukulia hatua viongozi wake waliosaini waraka wa G55 uliotolewa Aprili 3, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Welwel, viongozi hao wataitwa kuthibitisha iwapo saini hizo ni zao, kufafanua dhamira zao kama kweli wamependekeza mwelekeo tofauti na msimamo wa chama, kisha hatua zitachukuliwa baada ya kupitiwa maelezo yao.

“Tukijiridhisha kuwepo kwa usaliti na njama za kukisaliti chama, hatutasita kuchukua hatua kali za kikatiba na kikanuni dhidi ya wote watakaobainika kuhusika,” amesema mwenyekiti huyo katika taarifa aliyoitoa leo, Aprili 6, 2025.


Upotoshaji

Katika hatua nyingine, Mrema amesema ajenda ya ‘No reforms, no election’ ilianza mwaka 2020 ikilenga kuhamasisha makundi ya kijamii kushinikiza mageuzi ya kisheria na si kuzuia uchaguzi.

Amesema yeye na ofisa mmoja wa chama hicho ndio walioachwa nchini Kenya kukamilisha andiko la nyaraka za ajenda hiyo wakati huo, lakini haikulenga kuzuia uchaguzi.

Amesema suala la kuzuia uchaguzi ni hatari kwa chama hicho, kwa kuwa hata sasa kimeanza kupoteza asasi za kiraia zilizokuwa zinakiunga mkono katika harakati zake za kudai mageuzi.

“Zinashindwa kuja mstari wa mbele kwa sababu tumeongeza kuzuia uchaguzi, angalieni asasi za kiraia zilizokuwa zinapiga kelele kuhusu mabadiliko, baada ya kusema tutazuia uchaguzi ni kama wamepoa kwa sababu wanaona sasa hapa Chadema inavuka mstari,” amesema.

Hata hivyo, amesema umoja wa G55 hauhusishi wanachama 55 pekee, wapo wengi isipokuwa idadi hiyo ni uwakilishi.

"Kundi hili siyo la watu 55, tupo wengi ambao tunakishauri chama, baada ya kuanzishwa kwa kundi hili hata wagombea wa udiwani, wameomba kujiunga na wengine wengi wanaomba," amesema.

Amesema hatua ya kuzuia uchaguzi inahatarisha ari na hamasa ya wanachama na wananchi na hata ya kukichangia chama hicho itapungua.

“Ndiyo maana hii kampeni yetu ya Tone Tone inakwama kwa sababu watu wanajiuliza hivi nawachangia Chadema ili iweje wakati hata uchaguzi hawashiriki,” amesema.

Katika hatua nyingine, amewataka viongozi wa chama hicho kwenda kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi Aprili 12, mwaka huu ili kukipa uhalali wa kushiriki uchaguzi mkuu.

"Wasije wakatumia mwanya huu wakakimbia kwenda kusaini kanuni ili baadaye waje watugeuzie tena, siyo kwamba ‘No election’ hatuzuii uchaguzi bali kanuni zimeshatutoa nje ya uchaguzi," amesema.

Wakati hayo yakiendelea, Baraza la Wazee la Chadema (Bazecha) kupitia chombo maalumu (caucus) kilichoundwa kutatua migogoro limeanza mchakato wa maridhiano kutibu majeraha yaliyotokana na uchaguzi ndani ya chama hicho.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo Mwananchi inazo, chombo hicho Aprili 4, 2025 kilikutana na Mwenyekiti mstaafu, Freeman Mbowe, nyumbani kwake Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia mchakato wa safari ya maridhiano Aprili 4, 2025, Mwenyekiti wa Bazecha, Suzan Lyimo alilieleza Mwananchi kwa kutambua hali inayoendelea ndani ya chama, baraza limeunda chombo maalumu kwa ajili ya kutatua na kusuluhisha migogoro.

“Kimeanza (caucus) kazi rasmi jana (Alhamisi Aprili 3), kinaongea na viongozi wakubwa wawili kwa kuanzia, kwa maana ya Mbowe na Lissu (Tundu- Mwenyekiti wa sasa), kwa sababu tatizo la kutoelewana limetokana na uchaguzi. Kwa hiyo kuna kundi linaloona ajenda ya kuzuia uchaguzi haiwezekani na wanasema kwa nini haiwezekani sasa wakati ilianzishwa wakati wa Mbowe, katika hali ya kawaida unaona inawezekana walio upande wa Mbowe wanataka mabadiliko na uchaguzi uwepo,” alisema.