Utunzaji mazingira ulinionyesha fursa kwenye matairi

Muktasari:
Matairi chakavu ya magari yanatumika kutengeneza masofa, makochi na viti vinavyoipamba nyumba n akumfanya mwenye nayo kuonekana anayekwenda na wakati.
Achana na mikokoteni kuna matumizi mengine ya matairi ya gari yaliyotumika. Watu wanatengeneza samani za maana tu na kujiingizia kipato cha uhakika.
Matairi chakavu ya magari yanatumika kutengeneza masofa, makochi na viti vinavyoipamba nyumba n akumfanya mwenye nayo kuonekana anayekwenda na wakati.
Najua ni ngumu kuamini kwa sababu wengi wamezoea kuona matairi hayo yakitumika kutengeneza viatu vya Kimasai au bidhaa nyinginezo.
Lakini Aisha Daudi (25), mhitimu wa astashahada ya ualimu ameamua kutumia matairi hayo yanayoonekana kama taka mtaani kutokana na kukosa matumizi mengine ya maana na kuchukua muda mrefu bila kuoza kutengeneza kitu kipya cheny emanufaa kwake na jamii inayomzunguka.
Kutokana na shughuli za utunzaji wa mazingira anasema aliiona fursa ya kutumia malighafi hiyo kutokana na ugumu wake katika uteketezaji na kukosa sehemu ya kuyatupa.
“Hata magari ya taka huwa hayabebi matairi haya hivyo kuyaacha yakihifadhi mbu na kuchafua mazingira jambo ambalo linaweza kuleta madhara,” anasema Aisha.
Anasema alianza urejelezaji wa matairi hayo na kupata kitu kipya kwa kuyapaka rangi, kuyawekea sponji na kutengeneza viti vinavyofaa kwa matumizi ya nyumbani.
Kupitia mitandao ya kijamii anasema aliweza kujifunza na kuongeza ujuzi wa utengenezaji wa viti kama inavyofanywa kwenye nchi nyingine.
Kwa mtaji wa Sh50,000 alinunua malighafi na kuanza utengenezaji huo Septemba 2017 na mpaka sasa mtaji wake umeongezeka na kuzidi Sh1 milioni.
“Kuna aina mbalimbali za viti ninavyotengeneza vingine muundo wake ni kama sofa kabisa na bei zake zinaanzia Sh35,000 hadi Sh150,000,” anasema Aisha.
Kwa siku anaweza kutengeneza viti sita hadi 10 na kwa wiki ana uwezo wa kutengeneza viti 49.
Wakati anaanza utengenezaji wa bidhaa hiyo watu wengi walikuwa hawaelewi anachofanya na kudhani ni mtu aliyechanganyikiwa kwa sababu alilazimika kuokota matairi sehemu mbalimbali kabla ya kuanza utengenezaji.
“Nilipotengeneza kila mtu alishangaa. Kwa sasa soko kubwa nalipata kupitia mitandao ya kijamii,” anasema Aisha.
Anasema haikuwa kazi ngumu kumudu biashara hiyo baada ya kukosa ajira alipomaliza chuo mwaka 2015 kwa sababu alikuwa akifanya biashara ndogondogo tangu akiwa anasoma.
“Tangu nipo chuo nilikiwa nauza nguo za kike, mikoba pamoja na kutengeneza na kuuza urembo wa asili,” anasema Aisha.
Kwa uzoefu alionao kwenye biashara hiyo Aisha anatamani kumiliki kiwanda cha kusaga matairi yaliyotumika kutengeneza bidhaa tofauti.
“Kuna rami, nyaya, mafuta lakini lazima uwe na mashine maalumu za kufanya hayo yote na endapo nitafanikiwa nitaweza kudhibiti matairi yote yanayosababisha uchafu mtaani na kuajiri vijana wengi zaidi,” anasema Aisha.
Anasema pia anatamani kupata eneo maalumu la kufanyia kazi yake ili awe huru kukusanya matairi mengi kadri awezavyo tofauti na sasa.
Anasem ahuwa anapigiwa simu na watu ili akachukue matairi lakini hana sehemu maalumu ya kuyaweka yakisubiri kuchakatwa.