Miundombinu ya viwanja vya ndege ilivyoporomosha Usafirishaji mizigo

Muktasari:
Ripoti hiyo inaonyesha kuwapo kwa upungufu wa tani 5,990 katika mwaka 2016 kutokana na usafirishwaji wa tani 24,030 za mizigo uliofanyika katika kipindi hicho ikilinganishwa na tani 30,021 zilizopatikana mwaka 2015.
Licha ya kuwapo kwa ongezeko la asilimia 2.3 la usafirishaji abiria kwa njia ya anga mwaka 2016, usafirishaji wa mizigo uliweza kupungua kwa asilimia 20, ripoti ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) inaonyesha.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwapo kwa upungufu wa tani 5,990 katika mwaka 2016 kutokana na usafirishwaji wa tani 24,030 za mizigo uliofanyika katika kipindi hicho ikilinganishwa na tani 30,021 zilizopatikana mwaka 2015.
Mbali na upungufu huo wa mizigo katika mwaka 2016, usafirishaji wa mizigo kimataifa nao ulipungua kwa asilimia 20.3 kutoka tani 27,600 mwaka 2015 hadi tani 21,988 mwaka 2016.
Miongoni mwa sababu kubwa zilizotajwa kuchangia kupungua kwa mizigo katika usafiri wa anga ni kupungua kwa usafirishaji wa chakula kutoka Tanzania kwenda Commoro.
Mbali na hiyo pia wajasiriamali wanaofanya biashara zao kati ya Tanzania, Afrika ya kati na Bara la Asia, walianza kutumia njia ya maji kusafirishia mizigo yao badala ya anga ili waweze kupunguza gharama.
Kukosekana kwa mvuto wa kibiashara na vifaa katika viwanja vya kimataifa vya Julius Nyerere, uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Abeid Amani Karume na Uwanja wa Ndege wa Mwanza, kumechangia pia kushuka kwa takwimu za usafirishaji wa mizigo.
Imeelezwa upungufu huo umesababisha baadhi ya wajasiriamali kuhama na kuamua kutumia viwanja vya ndege vya kimataifa vya nchi nyingine vikiwamo vya Jomo Kenyata nchini Kenya na Entebe cha Uganda kusafirisha bidhaa hususan samaki, nyama, maua, mboga za majani na matunda kwenda nje ya nchi.
Ndani ya nchi pia usafirishaji mizigo ulipungua kwa tani 380 kutoka tani 2,422 mwaka 2015 hadi kufikia tani 2,042 mwaka 2016 ambayo ni sawa na asilimia 15.7 huku sababu kubwa ikiwa ni kupungua kwa kasi ya shughuli za kibiashara zinazofanyika ndani ya nchi.
Uwapo wa baadhi ya changamoto hizo uliweza kuathiri kasi ya usafirishaji wa mizigo katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere (JNIA) ambao ndiyo nguzo kuu ya usafirishaji katika sekta ya anga hususani kimataifa.
Usafirishaji wa mizigo katika uwanja huo uliweza kupungua hadi kufikia tani 17,398 mwaka 2016 ikilinganishwa na tani 22,014 zilizokuwapo mwaka 2015 ambayo ni sawa na pungufu ya mizigo kwa asilimia 21.
Usafirishaji wa mizigo kimataifa kupitia uwanja huo pia uliweza kupungua hadi kufikia tani 16,716.3 mwaka 2016 kutoka tani 21,142.9 za mwaka 2015 ambayo ni sawa na asilimia 20.9.
Jumla ya asilimia 73 ya mizigo yote iliyosafirishwa ndani na nje ya nchi mwaka 2016 ilipitia JNIA ambayo ni ongezeko la asilimia moja ya mizigo iliyosarifishwa kupitia uwanja huo mwaka 2015
Hata hivyo, kuporomoka kwa shehena ilikuwa ni miongoni mwa agenda zilizojadiliwa katika mkutano wa kwanza wa wadau wa sekta ya usafiri wa anga nchini, uliofanyika hivi karibuni Jijini Dar es Salaam.
Katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TCAA, Hamza Johari alisema ongezeko la abiria lilipaswa kwenda sambamba na mizigo.
“Wafanyabiashara wa samaki wanatoka Mwanza, wanapeleka mizigo yao Uwanja wa Entebe kwenda nje wakati Mwanza nako kuna uwanja. Au mfanyabiashara wa maua anayasafirisha kutoka Kilimanjaro hadi Nairobi wakati kuna uwanja wa Kilimanjaro. Kuna tatizo mahali,” anasema Johari.
Wadau katika mkutano huo walipendekeza namna nzuri ya kuiinua sekta hiyo ni kuuboresha JNIA.
Wanasema uwanja huo ni njia panda ya kwenda nchi nyingine duniani.
Akizungumza kwenye warsha hiyo iliyowakutanisha wadau wa usafirishaji wa anga, Kaimu Mkurugenzi uchumi na Mamlaka ya Anga Tanzania (TCAA), Daniel Malanga aliwahi kunukuliwa akisema kumalizwa kwa changamoto miundombinu katika sekta ya usafiri wa anga ni kitu muhimu katika uchumi na maendeleo enedelevu na biashara mizigo.
“Asilimia 40 ya matunda na mboga za majani huharibika kila mwaka kabla ya kusafirishwa, kuinuliwa kwa miundombinu kutasaidia katika kuondoa hali hii,” anasema Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Wakulima wa Maua na Mbogamboga Tanzania (Taha), Aman Temu.
Anasema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2016/2017, uzalishaji wa mazao hayo ulikuwa tani 6.2 milioni za ujazo na kati ya hizo asilimia 50 zilisafirishwa kwa ndege kwenda masoko ya nje ya nchi.
Anasema, asilimia 20 ya mzigo huo ulisafirishwa kupitia Kenya na asilimia 30 Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
“Kampuni za ndani zinapaswa kujipambanua na kwenda nje. Ni muhimu kuimarisha miundombinu ya viwanja na uhifadhi wa mizigo,” anasema Temu.
Ofisa Uhusiano wa Kampuni ya Precision Air, Hillary Mremi anasema shehena ni chanzo muhimu cha mapato kwenye biashara ya usafiri wa anga, lakini hayavunwi vizuri kutokana na kukosekana kwa ndege za moja kwa moja zinazoenda kwenye mataifa ya mbali.
“Ukiacha abiria, mzigo huongeza mapato ya kampuni nyingi lakini katika viwanja vyetu huwezi kupata ndege ya moja kwa moja kwenda mataifa ya mbali.
“Vilevile aina ya ndege tunazo tumia si rafiki kwa usafirishaji wa mizigo,” anasema Mremi.
Mshauri wa masuala ya usafiri wa anga na mfanyabiashara ya kusafirisha mizigo, Jimray Nangawe anasema miundombinu ya viwanja vya ndege inahusika kwa kiasi kikubwa kustawisha bishara hiyo.
“Kuna vitu wateja wanavizingatia ili kuweza kutumia uwanja wa ndege fulani kama huduma na mifumo ya kuwahisha shughuli na usalama wa eneo hilo, lakini sisi viwanja vyetu vingi vipo katika hatua ya kuendelezwa bado havijafikia huko,” anasema Nangawe.
Anasema ni muhimu kuwa na uwanja ambao ni njia panda ya wasafiri wengi pamoja na kuzingatia mambo mengine muhimu kama mazingira ya biashara na kuondoa vikwazo visivyo vya lazima ili kuongeza kasi ya uwekezaji.
“Usafiri wa anga ulipitia wakati mgumu mwaka 2016, kupunguzwa kwa matumizi ya serikali hayajaathiri usafiri wa anga tu bali sekta ya usafirishaji wa anga kwa ujumla,” alisema Mremi.
Aliongeza; “Serikali ndiyo watumiaji wakubwa na wamepunguza miamala hata kwa sekta binafsi na haiepukiki kwetu sisi kuona ni jinsi gani imefinywa hasa katika kupiga marufuku safari za nje ya nchi kwa watumishi wa umma.” Meneja wa Operesheni wa Kampuni ya Swissport, Noel Kasako anasema hali hiyo nchini inachangiwa na kupungua kwa shughuli za utafiti wa mafuta na gesi kwenye ekina bahari.
“Mzigo unaoingia ndiyo umeshuka zaidi kuliko usafirishaji na hakuna sababu za hivi karibuni za kimazingira zilizosababisha hilo.
“Wakati wa utafiti wa mafuta na gesi tulikuwa na uwezo wa kusafirisha wastani wa tani 700 kwa wiki,” anasema Kasako.
Anasema mitambo iliyokuwa ikiletwa kwa ajili ya kufanyia utafiti ilikuwa na uzito mkubwa na ilikuwa inakodiwa kwa saa, hivyo lazima isafirishwe kwa ndege ili ifanye kazi haraka na kurudishwa kwa muda.
Kadhalika anasema kutoongezeka kwa mizigo kwenye viwanja vya nchini halikusababishwa na miundombinu ya uhifadhi wa mizigo tu, bali uwapo wa ndege zenye uwezo wa kubeba mizigo mikubwa kuelekea nchi ambazo wafanyabiashara wengi wanauza na kununua bidhaa.
Mpaka sasa, kuna maboresho kadhaa yamefanyika katika sekta ya anga nchini, kama upanuzi wa viwanja vya ndege na ununuzi wa rada mpya nne ambazo zimegharimu Sh63.1 bilioni kwa lengo la kuimarisha ukusanyaji wa mapato na usalama.