Bendi imara zinawezekana kwa kufanya haya-Zahoro

Kiongozi wa bendi, Salum Zahor
Muktasari:
Hata hivyo, kiongozi wa Bendi ya Shikamoo Jazz, Salim Zahoro anaeleza nini kifanyike kwa wanamuziki ili walete mafanikio katika bendi zao akikemea tabia ya kuhama bendi bila sababu ya msingi na kuonya kwamba inaharibu kipaji cha mwanamuziki na bendi kwa jumla.
Wanamuziki wengi wa muziki wa dansi wana sifa kubwa ya kuhama bendi moja kwenda nyingine na kuwa kama sehemu ya maisha au utamaduni wao hivyo kusababisha bendi nyingi kukosa uimara.
Hata hivyo, kiongozi wa Bendi ya Shikamoo Jazz, Salim Zahoro anaeleza nini kifanyike kwa wanamuziki ili walete mafanikio katika bendi zao akikemea tabia ya kuhama bendi bila sababu ya msingi na kuonya kwamba inaharibu kipaji cha mwanamuziki na bendi kwa jumla.
Anasema kuwa kinachoharibu mustakabali wa bendi nyingi nchini na vipaji vya mwanamuziki ni tabia ya kuhama hama bila sababu ya msingi.
Anasema kwamba licha ya kuwapo wanamuziki wachache waliofanikiwa kwa kuhama bendi moja kwenda nyingine, wengi wao huishia kupotea katika fani ya muziki.
Mkongwe huyo anaeleza kuwa wanaostahili kuitwa wanamuziki ni wale wanaofahamu kupiga vyombo na kuimba, akimtaja Ally Adinani kuwa ni mfano kwani alikuwa akipiga vyombo, akajifunza sasa anaimba na kwa umahiri.
Zahoro anasema kuwa wanamuziki wengi wanaohama bendi moja kwenda kutafuta maslahi na kusahau kwamba wanatakiwa kuweka kipaumbele mafanikio ya bendi waliopo wakizingatia kuwa bila wao hakuna atakayefanya hivyo.
Anasisitiza kuwa mwanamuziki aliyeko katika bendi ni muhimu afahamu kuwa lengo kuu la uwapo wake ni maendeleo ya bendi anayoitumikia.
“Nakumbuka wakati sisi tunaimba, tulikuwa tukifanya hivyo kwa mapenzi, hatukutaka jina la bendi liwe baya, ingawa wapo aliohama lakini waliona fahari kusikia mafanikio ya bendi yao, ”anasema Zahoro.
Zahoro anafafanua kuwa kitu muhimu wanachotakiwa kufanya ni kuhakikisha wanakuwa na heshima kati yao na mashabiki wao, huku wakiweka mbali urafiki usiokuwa na tija.
Anaeleza kuwa mbali na hilo wanamuziki inawapasa kujithamini wao kwa wao wanapofanya kazi kwa kujipanga huku kila mmoja akiona umuhimu wa mwenzake.
Alieleza kuwa, ujuaji, maringo, kujisikia, hakuna nafasi katika bendi, “Nimekuwa kiongozi miaka mingi na nimekuwa nikilikemea hili na kwa kiasi fulani limeleta umoja katika bendi nilizowahi kuongoza ikiwamo hii ya sasa Shikamoo Jazz, ”alisema Zahoro.
Alisema ili kuimarisha bedni wanamuziki waliopo wanatakiwa wafahamu kuwa siyo kila mwanamuziki katika bendi anaweza kuwa kiongozi bali kuna ambao wana hekima na wanaweza kuwa katika nfsi hiyo.
Alifafanua kuwa bendi haiwezi kufanya vizuri kama ina wanamuziki wenye tamaa na kufikiria kuwa viongozi kila siku.
Anabainisha kuwa madhara ya kuwa na moyo huo ni kutengeneza migogoro kwa kuwapinga waliopo madarakani.
“Mikishakuwa makundi, kila mmoja akafanya lake, hakuna kitakachofanyika, kazi zitakuwa hazina ubora huku wanamuziki wenye hekima wakitaka kuondoka na kutafuta mahali penye utulivu.
Hivyo ni bora kuwa na umoja na kufanya uchaguzi wa viongozi wa haki na kuwaunga mkono kwa moyo wote na safi, ”anasema Zahoro.