Marais wampongeza Papa mpya

Washington. Marais Donald Trump wa Marekani na Volodymyr Zelensky wa Ukraine wamempongeza Papa mpya, Leo wa XIV, kwa kuchaguliwa kwake kuwa Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani.
Rais wa Marekani, Donald Trump, alieleza furaha yake kubwa kupitia mtandao wa Truth Social, akimpongeza Kardinali Robert Francis Prevost kwa kuchaguliwa kuwa Papa. Trump alisema:
“Hongera kwa Kardinali Robert Francis Prevost, ambaye sasa ni Papa Leo wa XIV. Ni heshima kubwa kutambua kwamba yeye ndiye Papa wa kwanza kutoka Marekani. Ni jambo la kusisimua sana, na ni heshima kuu kwa taifa letu. Natarajia kwa hamu kukutana na Papa Leo wa XIV. Itakuwa wakati wa maana sana”
Kwa upande wake, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, ametuma salamu zake za pongezi kupitia mtandao wa X (zamani Twitter), akieleza matumaini yake ya kuendelezwa kwa usaidizi wa kiroho na kimaadili kutoka kwa Vatican katika kipindi kigumu kinachoendelea kutokana na vita nchini Ukraine.
Zelensky aliandika:
“Hongera kwa Mtakatifu Baba, Papa Leo wa XIV, kwa kuchaguliwa kwake kushika Kiti Kitakatifu cha Mtakatifu Petro na kwa kuanza kwa kipindi chake cha upapa.
“Ukraine inathamini sana msimamo thabiti wa Vatican katika kulinda sheria za kimataifa, kulaani uvamizi wa kijeshi wa Urusi dhidi ya Ukraine, na kutetea haki za raia wasio na hatia. Katika wakati huu wa hatima kwa taifa letu, tunatumaini kuendelea kupata msaada wa kiroho na wa maadili kutoka kwa Kiti Kitakatifu katika juhudi za kurejesha haki na kufikia amani ya kudumu.”
Alimalizia kwa kumtakia Papa mpya hekima, uvumilivu na nguvu za kiroho na kimwili katika kutekeleza jukumu lake takatifu, akisema:
“Ad multos annos!” (Maana yake: “Kwa miaka mingi ijayo!” tamko la baraka kwa maisha marefu).