Zambia yaonesha mfano, watoto wapatiwa kinga dhidi ya malaria

Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Kushoto) akisaini mkataba wa uenyeji wa Taasisi ya Umoja wa wakuu wa nchi za Afrika dhidi ya mapambano ya Malaria (ALMA) na Katibu mkuu wa Taasisi hiyo, Joy Phumaphi Jijini Dodoma leo Juni 28, 2025. Picha na Rachel Chibwete
Muktasari:
- Serikali imesaini mkataba wa miaka mitatu wa kuwa mwenyeji wa taasisi ya Umoja wa Wakuu wa Nchi za Afrika katika Mapambano dhidi ya malaria (ALMA), unaolenga kuimarisha juhudi za kutokomeza ugonjwa huo barani Afrika.
Dodoma. Katibu Mkuu wa Taasisi ya Umoja wa Wakuu wa Nchi za Afrika katika Mapambano dhidi ya Malaria (ALMA), Joy Phumaphi, amesema taasisi hiyo imepiga hatua kubwa katika kusaidia nchi mbalimbali barani Afrika kupambana na malaria.
Amesema baadhi ya nchi, ikiwemo Zambia, tayari zimeanza kutoa huduma za kinga kwa watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano ili kuwalinda dhidi ya maambukizi ya ugonjwa huo hatari.
Kwa mujibu wa Phumaphi, ALMA inaendelea kushirikiana na serikali za Afrika kuimarisha mikakati ya kutokomeza malaria kupitia matumizi ya rasilimali za ndani.
Phumaphi ametoa kauli hiyo leo, Jumamosi Juni 28, 2025, wakati wa hafla ya kusaini mkataba wa miaka mitatu kati ya taasisi hiyo na Serikali, ambao unaiweka rasmi Dodoma kuwa makao makuu ya ALMA, taasisi ya Umoja wa Wakuu wa Nchi za Afrika inayoshughulika na mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria.
Aidha, amesema kuwa hadi sasa, hakuna mradi wowote wa kutokomeza malaria uliowasilishwa na nchi za Afrika ambao umekataliwa na taasisi hiyo, jambo linalodhihirisha dhamira ya ALMA katika kuunga mkono juhudi za mataifa ya Afrika dhidi ya ugonjwa huo.
“Tangu kuanzishwa kwa taasisi hii miaka 16 iliyopita hali ya ugonjwa wa malaria imepungua tofauti na ilivyokuwa awali, tumekuwa tukitekeleza miradi mbalimbali ya nchi za Afrika ya kupambana na ugonjwa huo na hakuna mradi wowote ambao umewahi kukataliwa wa kupambana na malaria,” amesema Phumaphi.
Amesisitiza kuwa ALMA imekuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono juhudi za mataifa ya Afrika katika vita dhidi ya malaria, kwa kuhakikisha miradi inayolenga kutokomeza ugonjwa huo inapata uungwaji mkono wa kisera na kiufadhili.
Amesema kuwa lengo kuu la taasisi hiyo ni kuhakikisha Bara la Afrika linajitegemea katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria, kwa kutumia rasilimali zake za ndani badala ya kutegemea msaada kutoka mataifa ya nje.
Kwa mujibu wa Phumaphi, ALMA imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kusaidia nchi mbalimbali barani Afrika katika kupambana na malaria, ambapo baadhi ya nchi ikiwemo Zambia, tayari zimeanza kutoa kinga kwa watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano, ili kuwakinga dhidi ya maambukizi ya ugonjwa huo.
Amesema kuwa taasisi hiyo inashirikiana na wizara mbalimbali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria, hasa zile ambazo kwa namna moja au nyingine zinahusiana moja kwa moja na mazingira yanayochochea mazalia ya mbu wanaoeneza malaria.
Wizara hizo ni pamoja na Wizara ya Mazingira, Ujenzi, Madini na Fedha, kwa lengo la kuhakikisha kuwa juhudi za kutokomeza ugonjwa huo haziathiriwi na changamoto za kimfumo wala kiutendaji.
“Pia, tuna mpango wa kuanzisha ndege nyuki zitakazokuwa zinatumika kumwagilia mashamba, lakini zitakuwa na dawa ya kuua mazalia ya mbu ambayo ndiyo sababu ya kuenea kwa ugonjwa huu, teknolojia hii ipo mbioni na ikiishakamilika tutaisambaza kwa nchi zote za Bara la Afrika,” amesema Phumaphi.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amesema kuwa Taasisi ya ALMA imekuwa na mchango mkubwa katika kusaidia Tanzania kupunguza kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa malaria, ambao hapo awali ulikuwa ni tishio kubwa kwa afya ya umma.
Amesema hali ya sasa imeboreshwa kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma, ambapo malaria ilisababisha vifo vingi na kuathiri maisha ya watu wengi.
“Kwa sasa, maambukizi ya malaria yamepungua kwa kiasi kikubwa. Mimi binafsi nilikuwa naugua mara nne kwa mwezi, lakini sasa ni takriban miaka mitano sijapata tena ugonjwa huo. Hii inaonyesha wazi kwamba juhudi za ALMA zimeleta matokeo chanya,” alisema Balozi Kombo.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Seif Shekilaghe amesema ALMA imesaidia kwa kiwango kikubwa mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria kwa sababu imekuwa ikitekeleza afua mbalimbali za kukabiliana na ugonjwa huo kama vile kutokomeza mazalia ya mbu kwa kupuliza dawa maalum, kumhifadhi mwananchi kwa kumpatia chandarua na tiba pale mwananchi anapougua malaria..
“Moja ya malengo yaliyowekwa kwenye mkataba huu ni ifikapo mwaka 2030 tuwe tumeutokomeza ugonjwa wa malaria,” amesema Dk Shekilaghe.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Malaria Duniani yaliyofanyika Aprili 25, 2025, Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, alisema kuwa kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa malaria nchini kimepungua kwa asilimia 45, kutoka asilimia 14.5 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 8.1 mwaka 2024.
Mhagama alisema mafanikio hayo yametokana na juhudi madhubuti zilizowekwa na Serikali katika kudhibiti na kutibu ugonjwa huo, ikiwemo upuliziaji wa dawa kwenye mazalia ya mbu na kuimarisha huduma za kinga na tiba kwa wananchi.