Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali kuongeza nguvu mapambano ya dengue, chikungunya

Muktasari:

  • Serikali kwa kushirikiana na wadau wa afya kutoka Korea imeamua kuja na mradi wa miaka mitano wa ufuatiliaji wa magonjwa ya dengue na chikungunya sambamba na ugonjwa wa matatizo ya upumuaji.

Dar es Salaam. Serikali kupitia Wizara ya Afya imetangaza kuongeza nguvu katika ufuatiliaji wa magonjwa ya dengue na chikungunya kupitia mradi wa miaka mitano wa uwezeshaji wa wataalamu wa maabara na vituo vilivyopo halmashauri za mikoa, ili kugundua virusi wanaosababisha maradhi hayo.

Dengue ni maambukizi ya virusi yanayoenezwa na mbu aina ya Aedes ukiwa na dalili za maumivu ya viungo na misuli, homa kali na upele.

Kadhalika chikungunya kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ni ugonjwa unaoenezwa na mbu jike aliyebeba virusi vya chikungunya ukiwa na dalili za homa ya ghafla ikiambatana na maumivu ya misuli.

Serikali kwa kushirikiana na wadau wa afya kutoka Korea imeamua kuja na mradi wa miaka mitano uliozinduliwa leo Alhamisi Juni 19, 2025 kwenye mkutano uliofanyika katika ofisi za Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ukihudhuriwa pia na watendaji wa Wizara ya Afya.

Mkurugenzi wa Huduma za Dharura na Majanga Wizara ya Afya, Dk Erasto Sylvanus amesema mradi huo unahusisha ufuatiliaji wa magonjwa hayo ya virusi ambayo kwa kiasi kikubwa yanapatikana ukanda wa joto.

Pia, amesema mradi utahusisha ufuatiliaji wa maradhi ya virusi wanaosababisha matatizo ya upumuaji ikiwemo influenza, Uviko19.

“Mradi huu unafanywa na Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii utahusisha kuwezesha wataalamu wa maabara kuu na vituo vilivyopo halmashauri na mikoa watakaopima maradhi hayo.

“Mradi utasaidia ugunduaji wa mapema wa virusi hivyo vilivyopo ukanda wa joto na mvua nyingi ambao upo Afrika Mashariki. Ufuatiliaji utasaidia watu wenye homa na maumivu ya mwili hali isiyo ya malaria au magonjwa ya kuambukiza waweze kuchunguzwa ni wadudu gani ndipo tuangalie dengue na chipungunya,” amesema Dk huyo.

 “Magonjwa haya yapo miaka mingi mfano dengue umegundulika miaka ya 1700, chikungunya upo muda mrefu na kwa hapa Tanzania uligundulika ukanda wa Kusini. Maeneo yenye mbu hawa maalumu wanang’ata mchana badala ya usiku,” amesema.

Amesema magonjwa hayo yapo kwenye mazingira tunayoishi huku akitahadharisha watu waishio maeneo hayo kuchukua tahadhari ikiwemo kuvaa nguo ndefu na kutotembea maeneo yenye mbu na kupaka dawa za mbu.

Akifafanua zaidi amesema mradi utaanza ukanda wa bahari ya Hindi na maeneo yenye mvua nyingi na joto ambapo kuna hatari ya mbu hao kuzaliana.

“Hatujaona tatizo limeibuka hapana bali tunaongeza nguvu ya upimaji ili watu wajue watibiwe. Tumeongeza vipimo ili watu wajue njia bora za kutibiwa kuliko kusema wamerogwa,” amesema.

Ameongeza kwamba kwa kipindi cha mvua kama hiki na joto kali linapokuja wanategemea kuwepo kwa hali ya mbu hao kuwang’ata watu.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii, Ambele Mwafulango amesema maabara hiyo imejipanga na ina uwezo wa kupima virusi hivyo sambamba na kuangalia ni vya aina gani.

Naye, Hansol Park kutoka taasisi ya KOFIH Korea, amesema mradi huo ni muhimu kwa kuwa unaijengea uwezo maabara hiyo wa kukabiliana na magonjwa nchini Tanzania. 

“Kwa sasa tunakabiliwa na magonjwa mengi tofauti.  Kwa hivyo, lazima tujilinde, na tunapaswa kujiandaa jinsi tunavyoweza kukabiliana nayo,” amesema Park.