Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

WHO yaonya homa ya ini bado tishio kubwa Afrika

Muktasari:

  • Takwimu mpya za Serikali zinaonesha maambukizi ya homa ya ini aina B yameendelea kubaki asilimia 3.5 ya Watanzania, sawa na watu milioni 2.4, huku aina ya C yakipungua kutoka asilimia 0.2 hadi 0.1.



Dar/Mikoani. Wakati Shirika la Afya Duniani (WHO) likisema homa ya ini bado ni moja ya magonjwa yanayosababisha vifo vingi barani Afrika na kuitaka dunia kuongeza kasi ya mapambano ya kutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030, Serikali imesema Tanzania imepunguza maambukizi ya homa ya ini aina C kutoka asilimia 0.2 mwaka 2022 hadi asilimia 0.1 mwaka 2025.

Mwakilishi wa WHO nchini, Dk Johnson Lyimo, amesema mafanikio hayo ni hatua muhimu, lakini bado yanahitaji kuambatana na ongezeko la huduma za uchunguzi, chanjo, matibabu na elimu kwa umma ili kufikia lengo la kutokomeza homa ya ini kama tishio la afya ya umma.

Akizungumza leo Jumanne, Julai 28, 2026, katika maadhimisho ya Siku ya Homa ya Ini Duniani yaliyofanyika mkoani Dodoma, Dk Lyimo amesema watu wengi bado hugundulika wakiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa kutokana na mwitikio mdogo wa kupima afya zao.

“Kikubwa tunachokiona ni mwamko mdogo wa wananchi kupima afya zao. Wengi wanaendelea kuishi bila kujua hali zao na hufika hospitalini baada ya kupata madhara makubwa yanayoweza kuzuilika kwa uchunguzi wa mapema,” amesema.

Amesema makundi yaliyo katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ni pamoja na watu wanaotumia dawa za kulevya kwa njia ya kujidunga sindano, watu wenye maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), pamoja na watoto wanaozaliwa na mama wenye ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa Dk Lyimo, changamoto nyingine zinazokwamisha mapambano dhidi ya ugonjwa huo ni upatikanaji usioridhisha wa huduma za uchunguzi na matibabu katika baadhi ya maeneo, pamoja na mwamko mdogo wa wananchi kujitokeza kupima.

Tamko lililotolewa na Serikali na kutiwa saini na Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Eliudi Eliakimu, limeeleza kuwa maambukizi ya homa ya ini aina C yameshuka kutoka asilimia 0.2 mwaka 2024 hadi kufikia asilimia 0.1 mwaka 2025, huku homa ya ini aina B ikiendelea kubaki asilimia 3.5 ya Watanzania wana maambukizi.

“Katika kukabiliana na tatizo hili, Serikali imeendelea kuchukua hatua muhimu za kudhibiti na kujikinga na maambukizi, ikiwa ni pamoja na kuhimiza wananchi kuzingatia upataji wa chanjo ya homa ya ini aina ya B na kutoa elimu kwa umma,” amesema.

Dk Eliakimu amesema Serikali imepanua huduma za uchunguzi na matibabu katika hospitali za wilaya, mikoa, kanda na hospitali za Taifa, kuimarisha uchunguzi kwa wajawazito na matibabu ili kuzuia maambukizi kwenda kwa mtoto, pamoja na kuhakikisha damu inayokusanywa inapimwa.

“Tunawasisitiza wananchi kuhakikisha wanajilinda na kujikinga kwa kupata vipimo na chanjo, hasa kwa homa ya ini aina ya B ambayo inaweza kukingwa mapema,” amesisitiza.

Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma (NTLP), Dk Kisonga Riziki, amesema kupungua kwa maambukizi ya homa ya ini aina C kunaonesha hatua zinazochukuliwa zinaanza kuzaa matunda, lakini bado kuna kazi kubwa ya kufikia malengo ya mwaka 2030.

Amesema Serikali inaendelea kuhimiza wananchi, hususan waliozaliwa kabla ya mwaka 2000, kujitokeza kupima ili kubaini hali zao mapema na kupata chanjo au matibabu kulingana na matokeo.

“Mapambano dhidi ya homa ya ini yanahitaji ushiriki wa kila mmoja. Tunataka kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 ugonjwa huu hauwi tena tishio la afya ya umma nchini,” amesema.

Dk Kisonga amesema katika maonyesho ya maadhimisho yaliyofanyika Dodoma, zaidi ya wananchi 1,500 walipatiwa huduma za uchunguzi ndani ya siku mbili, jambo alilosema linaonesha mahitaji makubwa ya huduma hizo.

Mmoja wa watu waliofika katika mabanda ya maonyesho ya kilele yaliyofanyika katika viwanja vya Nyerere Square, Hapygod Makundi, amesema watu wengi wamekosa fursa ya kupata huduma hizo kutokana na matangazo kutofika kwa kiwango kilichotarajiwa.

Makundi amesema homa ya ini ni tatizo kubwa kuliko Serikali inavyoliona kwa wananchi, hivyo akaomba mkazo zaidi uelekezwe katika kutoa elimu kwa umma ili wananchi waache kupuuza ugonjwa huo, kwani elimu ndiyo itakayosaidia kuwafikia watu wenye changamoto na kuwakinga wale ambao hawajakutana na maambukizi.


Kambi maalumu Dar

Wakati huo huo, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kwa kushirikiana na kampuni ya Mega We Care, imeendesha kambi maalumu ya siku mbili ya uchunguzi, upimaji na chanjo za homa ya ini bila malipo katika Kituo cha Muhimbili Sokoine Drive, jijini Dar es Salaam.

Mkazi wa Magomeni, Shaibu Musa, amewahimiza wananchi kujitokeza kupima homa ya ini na kupata chanjo, akisema huduma za bure zinazotolewa zinatoa fursa muhimu ya kujua hali ya afya mapema.

Shaibu amesema alifika kwenye kambi ya uchunguzi baada ya kupata taarifa kupitia vyombo vya habari, akisisitiza kuwa kufuatilia elimu za afya kumemhamasisha kuchukua hatua ya kupima.

Amesema wananchi wengi bado hawapati taarifa za kutosha kuhusu homa ya ini, licha ya ugonjwa huo kuwa tishio kubwa kwa afya.

Ameiomba Serikali kuongeza kampeni za uhamasishaji na kusogeza huduma karibu na wananchi, akieleza kuwa wengi hawawezi kumudu gharama za vipimo.

Pia amewataka wananchi kutumia fursa za huduma za bure ili kujua afya zao na kupata kinga au matibabu mapema.


Sababu saratani ya ini

Mkuu wa kitengo cha magonjwa ya mfumo wa chakula na ini wa hospitali hiyo, Dk Swalehe Pazi, amesema homa ya ini bado ni miongoni mwa sababu kuu za saratani ya ini, lakini ugonjwa huo unaweza kuzuilika na kutibika ukigundulika mapema.

Amesema MNH kwa sasa inahudumia takribani wagonjwa 5,000 katika kliniki ya magonjwa ya ini, huku idadi hiyo ikiendelea kuongezeka kutokana na kuimarika kwa huduma za rufaa na kuongezeka kwa uelewa wa wananchi.

“Changamoto kubwa ni wagonjwa wengi kufika hospitalini wakiwa wamepata madhara makubwa kama kutapika damu, kujaa maji tumboni au macho kuwa ya njano. Hali hiyo hufanya matibabu kuwa magumu zaidi,” amesema.

Naye Dk Penina Sikira wa Hospitali ya Siha Polyclinic mkoani Tanga, amesema watu wengi wanaweza kuishi na maambukizi ya homa ya ini kwa zaidi ya miezi sita bila kuonesha dalili, jambo linalofanya uchunguzi wa mapema kuwa silaha muhimu ya kuzuia madhara.

Amesema hospitali hiyo imeanza kutoa huduma za vipimo na chanjo bila malipo kwa wiki moja ili kuwahamasisha wananchi kujua hali zao za afya.

Imeandikwa na Herieth Makwetta (Dar), Habel Chidawali (Dodoma) na Mbonea Herman (Tanga).