Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Macho, masikio NEC ya CCM ikikutana Zanzibar

Muktasari:

  • Kikao hicho kinachotarajiwa kufanyika wakati wowote kuanzia sasa visiwani Zanzibar, chini ya uenyekiti wa Rais Samia Suluhu Hassan.



Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) kinatarajia kufanya kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), huku kukiwa na mambo kadhaa yanayohitaji mwafaka au kauli kutoka katika chama hicho tawala.

Miongoni mwa mambo hayo ni hatima ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), mchakato wa Katiba mpya, kujengwa kwa mwafaka wa kitaifa na kuanza kwa maridhiano baina ya chama hicho, Serikali na vyama vya upinzani.

Kikao hicho, kinachotarajiwa kufanyika hivi karibuni visiwani Zanzibar, pia kinatarajiwa kufanya mabadiliko madogo katika Sekretarieti ya chama hicho.

Chanzo kutoka ndani ya CCM kilichozungumza na Mwananchi kimesema kikao hicho pia kitahusisha tathmini ya baadhi ya dharura zilizotokea katika siku za karibuni, hasa kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.


NEC katikati ya mambo haya...

Julai 25, mwaka huu, Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi, aliwaambia Watanzania wapambane kupata Katiba mpya, jambo lililofufua upya mjadala wa kupatikana kwa Katiba hiyo.

Akiwa katika mkutano mkuu wa watetezi wa haki za binadamu, Dk Nchimbi alisema: "Pambaneni mpate Katiba mpya. Pambaneni mpate Katiba ambayo ina makubaliano ya wadau wote."

Alisisitiza wapambanie Katiba itakayoleta mwafaka katika Taifa, itakayoipeleka mbele nchi kwa miaka 50 ijayo, ambayo kila Mtanzania atajisikia fahari kujitambulisha kuwa anatoka katika nchi yenye Katiba inayojali maisha ya mtu na kuheshimu haki za raia wake.

"Ili uwe na hakika ya kupata Katiba mpya, moja ya mambo muhimu sana ni utashi wa kupata Katiba wa Rais aliyepo madarakani. Nataka niwaambie bila kuwadanganya, kwa mujibu wa Katiba yetu, Rais anapokaa kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri, Baraza la Mawaziri haliamui, linashauri," amesema.

Mara ya mwisho Rais Samia Suluhu Hassan alizungumzia suala la Katiba mpya ilikuwa wakati wa hotuba yake ya kulifungua Bunge la 13, Novemba 14, mwaka jana.

Katika hotuba hiyo alisema Serikali yake italifanyia kazi suala la mabadiliko ya Katiba kwa kuanza na Tume ya Usuluhishi na Maelewano.

"Kama tulivyoagizwa na Ilani ya CCM ya mwaka 2025 hadi 2030, moja ya hatua itakayotufikisha kwenye maelewano hayo ni marekebisho ya Katiba yetu," alisema.

Kikao hicho cha NEC ndicho kinachotarajiwa kutoka na kauli kuhusu suala hilo, hasa baada ya kauli ya Dk Nchimbi kuibua mijadala nje na ndani ya chama hicho, ikiwahusisha hadi wajumbe wa Kamati Kuu.

Kuhusu SUK, CCM na ACT-Wazalendo zilisaini tamko la pamoja la kuweka msingi wa kuanza safari ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Kilichobaki ni upande wa CCM kukubali kutekeleza baadhi ya mambo waliyokubaliana ili SUK iundwe na ianze rasmi.

Hivyo, huenda kikao hicho kikajadili suala hilo na kutoka na mwafaka utakaohitimisha na kuanza utekelezaji wa makubaliano hayo.


Mabadiliko ya Sekretarieti

Taarifa kutoka viunga vya CCM zinaeleza huenda kikao hicho kikafanya mabadiliko madogo katika Sekretarieti ya chama hicho, inayoongozwa na Katibu Mkuu wake, Dk Asha-Rose Migiro.

Nafasi inayotajwa kuguswa na mabadiliko hayo ni ya Naibu Katibu Mkuu Bara, inayoshikiliwa na John Mongella.

Mmoja wa viongozi waandamizi wa chama hicho amesema: "Kuna uwezekano Sekretarieti ikaguswa kidogo. Kuna mambo hayako sawa na katika kuiboresha, huenda Naibu Katibu Mkuu Bara akawekwa kando.

"Lakini mwenyekiti amekuwa na 'surprise' za hapa na pale, sasa kuna uwezekano akaja na jina la Katibu Mkuu mwingine. Kwa hiyo, ngoja tusubiri, lakini maboresho yanaweza kufanyika pia kwa nafasi nyingine za wajumbe.”

Suala lingine ni mchakato wa maridhiano na maelewano kati ya CCM, vyama vya upinzani na Serikali.

Suala la maelewano limekuwa ajenda ya muda mrefu ya Serikali baada ya kutokea maandamano yaliyoibua vurugu na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 500 Oktoba 29, jana, hivyo kikao hicho kinatarajiwa kujadili namna ya kuyaendea maridhiano hayo.

Akizungumza na Mwananchi, mmoja wa wajumbe wa Sekretarieti ya CCM amesema anachojua ni kwamba kutafanyika tathmini ya dharura ndogondogo zilizojitokeza siku za karibuni.

Ametaja kuwa miongoni mwa tathmini hizo ni masuala yanayohusu Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, lakini hakufafanua kwa kina kiini cha yatakayojadiliwa.

"Ninachojua ni kwamba kutakuwa na tathmini ndogondogo za dharura zilizotokea siku za karibuni," amesema mjumbe huyo aliyeomba hifadhi ya jina lake.

Amesisitiza hafahamu iwapo kutafanyika uamuzi mgumu wowote kupitia kikao hicho kwa kuwa mambo kama hayo mara nyingi hutokana na ajenda ya mengineyo, ambayo mwenyekiti (Rais Samia Suluhu Hassan) ndiye mwenye mamlaka nayo.

"Kwenye mengineyo ndipo, kama mwenyekiti ana jambo lake mfukoni, analitoa, sasa mnaanza kulijadili," amesema mjumbe huyo.


Mtazamo wa wadau

Akizungumzia hilo, mchambuzi wa siasa, Profesa Baraka Mfinanga, amesema CCM inahitaji kuangalia manufaa na changamoto za SUK kwa mustakabali wa utulivu wa kisiasa.

"CCM ni chama tawala, hivyo uamuzi wowote kuhusu SUK hauwezi kuachwa kwa Serikali peke yake. NEC inaweza kutaka kupata tathmini ya kina kuhusu namna mfumo huo utakavyoathiri ushiriki wa kisiasa, mshikamano wa wananchi na maandalizi ya uchaguzi ujao Zanzibar," amesema.

Kuhusu Katiba mpya, amesema NEC inaweza kujadili suala hilo kwa kuwa limeendelea kuwa ajenda inayotajwa na wadau mbalimbali.

"Chama kinaweza kutafakari kama mazingira ya sasa yanahitaji kuhuishwa kwa mjadala huo au kuweka mkakati wa namna ya kuendelea nao bila kuathiri vipaumbele vingine vya maendeleo," ameeleza Profesa Mfinanga.

Kwa upande wake, mchambuzi wa siasa, Said Majjid, amesema NEC inaweza kujadili maridhiano kwa sababu siasa za Tanzania zinaingia katika kipindi kinachohitaji utulivu.

Pia amesema Katiba mpya inaweza kujadiliwa kwa sababu imekuwa moja ya hoja zinazotajwa mara kwa mara na wadau wa siasa, hasa ukizingatia kuwa siku chache zilizopita Dk Nchimbi alifufua mjadala huo.

"Kauli ya Nchimbi, asasi za kiraia na baadhi ya viongozi wa vyama wamekuwa wakishinikiza kupatikana kwa Katiba mpya. NEC inaweza kutaka kuwa na msimamo wa pamoja kuhusu mwelekeo wa mjadala huo na matarajio ya wananchi," amesema.

Kwa mtazamo wake, SUK, Katiba mpya na maridhiano ni hoja zenye uhusiano, akisisitiza kuwa mwafaka wa kisiasa unafungua mlango wa majadiliano ya kikatiba.

"Ukipata Katiba inayokubalika, unaimarisha maridhiano ya kudumu. Ndiyo maana si ajabu kuona masuala hayo yakipewa uzito katika kikao kijacho cha NEC," amesema.

Mchambuzi mwingine wa siasa, Mwalimu Dennis Kiondo, amesema kikao hicho kinaweza kuwa miongoni mwa vikao muhimu vya NEC katika kipindi hiki.

Hoja yake hiyo inatokana na kile alichofafanua kuwa kikao hicho kinakuja wakati CCM ikikabiliwa na masuala yanayogusa mustakabali wa siasa za Tanzania.

"Katiba mpya, Serikali ya Umoja wa Kitaifa na maridhiano si ajenda za kawaida. Haya ni masuala yanayogusa namna nchi itakavyojengwa kisiasa kwa miaka ijayo. Ndiyo maana NEC inaweza kutaka kuyatolea mwelekeo wa kisera na kisiasa kabla ya hatua nyingine kuchukuliwa," amesema.

Amesema kauli ya Dk Nchimbi kuhusu Katiba mpya imeongeza uzito wa mjadala huo kwa kuwa imetolewa na mmoja wa viongozi wakuu wa nchi na chama.

Kwa mtazamo wake, wananchi wengi wanasubiri kuona kama kauli hiyo itaungwa mkono na chama au itabaki kuwa msimamo wa mtu binafsi.

"Katika mfumo wa Tanzania, CCM imekuwa na ushawishi katika maamuzi makubwa ya kisiasa. Msimamo wowote utakaochukuliwa na NEC kuhusu Katiba Mpya unaweza kutoa picha ya mwelekeo wa Taifa katika miaka ijayo," amesema.

Kuhusu maridhiano na SUK, Mwalimu Kiondo amesema masuala hayo yanahusiana moja kwa moja na utulivu wa kisiasa.

"Vyama vya siasa vikipata mwafaka, migogoro itapungua na imani ya wananchi kwa taasisi za dola itaongezeka. NEC inaweza kuona huu ni wakati sahihi wa kujenga daraja jipya la maelewano," amesema.