Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hatari homa ya ini inavyoua kimyakimya

Muktasari:

  • Takribani asilimia 80 ya watu wazima wanaopata maambukizi mapya ya virusi vya homa ya ini B huweza kuviondoa wenyewe ndani ya miezi sita kutokana na kinga ya mwili, na hivyo hupona bila kuingia katika hatua ya ugonjwa sugu.



Dar es Salaam. Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Homa ya Ini leo Jumanne, Julai 28, wataalamu wa afya wameonya kuwa ugonjwa huo unaweza kuingia mwilini bila kuonesha dalili zozote na kuendelea kwa miaka 10 hadi 20, ukiendelea kuharibu ini taratibu hadi kulisababisha kusinyaa na baadaye saratani.

Wataalamu hao wanasema wagonjwa wengi wanaofika hospitalini huchelewa kutambua maambukizi hayo, hali inayopunguza nafasi ya matibabu yenye mafanikio na kuongeza hatari ya vifo vinavyoweza kuzuilika.

Virusi vya homa ya ini B huambukizwa kupitia damu na majimaji ya mwili yenye maambukizi, ikiwemo kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa ujauzito au kujifungua, kujamiiana bila kinga na mtu mwenye maambukizi, pamoja na kuongezewa damu isiyopimwa ipasavyo.

Pia, maambukizi yanaweza kutokea kwa kutumia vifaa vyenye ncha kali, kama sindano, wembe, mashine za kunyoa, vifaa vya kutoboa masikio au kuchora mwilini ambavyo havijatakaswa.

Kwa homa ya ini C, maambukizi hutokea zaidi kupitia damu, hususan kwa watu wanaotumia sindano zinazoshirikishwa au vifaa vya tiba visivyo salama.

Hata hivyo, katika michezo inayoweza kusababisha majeraha na kutoka damu, kama mpira wa miguu, ndondi au mieleka, tahadhari zinapaswa kuchukuliwa ili kuzuia damu ya mchezaji mwenye maambukizi kugusana na jeraha wazi la mwingine.

Kwa mujibu wa Serikali, kupitia Taarifa ya Hali ya Sekta ya Afya ya mwaka 2025, maambukizi ya virusi vya homa ya ini B (HBV) nchini yanakadiriwa kufikia asilimia 3.5, sawa na Watanzania milioni 2.4, huku homa ya ini C (HCV) ikiwa na maambukizi ya asilimia 0.2, sawa na watu 138,000.

Makundi yaliyo katika hatari zaidi ni wanaotumia dawa za kulevya kwa njia ya kujidunga, wahudumu wa afya na wafungwa.

Katika mikakati ya Serikali, uchunguzi wa mapema kwa wajawazito hufanyika ili kubaini maambukizi na kuwezesha hatua za kumkinga mtoto. Aidha, chanjo ya homa ya ini B inapatikana katika hospitali na vituo vingi vya afya vya Serikali na binafsi nchini.

Watoto huipata kupitia ratiba ya taifa ya chanjo, huku watu wazima ambao hawajawahi kuchanjwa wakishauriwa kupima kwanza ili kufahamu hali yao kabla ya kuanza dozi za chanjo.

Katika mahojiano maalumu jana, Jumatatu, Julai 27, 2026, Mtaalamu wa Magonjwa ya Mfumo wa Chakula na Ini kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk Swalehe Pazi, anasema tofauti kubwa kati ya virusi hivyo ni kwamba homa ya ini B haina tiba ya kuondoa virusi kabisa, lakini ipo chanjo inayokinga maisha yote, huku homa ya ini C ikiwa na dawa zinazoweza kuponya, lakini haina chanjo.

"Kinga ndiyo silaha kubwa. Ukipata chanjo ya homa ya ini B mapema, unajikinga maisha yote dhidi ya maambukizi mapya," anasema.

Dk Pazi anasema Serikali imeboresha upatikanaji wa vipimo na chanjo katika hospitali nyingi za umma, hatua iliyosaidia kuongezeka kwa idadi ya watu wanaogundulika mapema na kuanza matibabu.

"Chanjo kwa hapa Muhimbili haizidi Sh10,000 na kipimo ni kati ya Sh9,000 hadi Sh10,000. Ninaamini pia hospitali zote za rufaa zinatoa chanjo hizi."

Anasema katika Hospitali ya Taifa Muhimbili pekee, kliniki ya magonjwa ya ini sasa inahudumia takribani wagonjwa 5,000 kwa mwaka, idadi iliyoongezeka kutokana na kuimarika kwa huduma za uchunguzi, matibabu na uelewa wa wananchi.

"Watu wasisubiri mpaka macho yawe ya njano au tumbo lijae maji. Hizo ni dalili za hatua za mwisho. Kupima mapema kunaokoa maisha na hupunguza hatari ya kufikia saratani ya ini," anasisitiza.


Hatua za ugonjwa

Akielezea hatua za ugonjwa, Dk Pazi anasema wagonjwa wengi wanaobainika katika hatua za mwisho wangekuwa na nafasi kubwa ya kupona au kudhibiti ugonjwa kama wangepimwa mapema.

Anasema homa ya ini husababishwa zaidi na virusi, huku aina B na C zikiwa hatari zaidi kwa sababu zinaweza kusababisha saratani ya ini.

"Virusi vya homa ya ini havianzi na dalili za moja kwa moja. Mtu anaweza kupata homa ndogo, uchovu au kujisikia kama ana malaria, lakini asiwe na dalili zinazomfanya afikirie ana ugonjwa wa ini," anasema.

Kwa mujibu wa Dk Pazi, hatua ya kwanza ya ugonjwa hujulikana kitaalamu kama acute hepatitis, na maambukizi huwa ndani ya kipindi cha chini ya miezi sita.

Anasema katika hatua hiyo, zaidi ya asilimia 80 ya watu wazima wenye kinga nzuri huweza kuviondoa virusi bila matibabu maalumu.

"Hata hivyo, kama virusi vitabaki mwilini kwa zaidi ya miezi sita, ugonjwa huingia katika hatua ya pili ya chronic hepatitis, yaani homa ya ini sugu. Hapo ndipo hatari ya kupata madhara makubwa huanza kuongezeka," anasema.

Dk Pazi anafafanua kuwa katika hatua hiyo ini huanza kupata makovu na kuwa gumu, hali inayojulikana kama fibrosis.

Anasema wagonjwa wengi katika hatua hiyo hawaoneshi dalili zozote na huendelea na shughuli zao za kila siku bila kujua kuwa ini limeanza kuharibika.

"Unaweza kwenda kazini, kufanya biashara au shughuli zako zote, lakini ndani ya mwili ini linaendelea kupata makovu. Ndiyo maana uchunguzi wa mapema ni muhimu," anasema.

Anasema ugonjwa unapoendelea zaidi, ini huanza kusinyaa, hatua inayojulikana kama cirrhosis.

Katika hatua hiyo, mgonjwa huanza kuonesha dalili kama uchovu wa mara kwa mara, kupungua uzito, macho kuwa ya njano, ngozi kubadilika rangi na, wakati mwingine, tumbo kujaa maji.

"Wapo wagonjwa wanaokuja hospitalini wakiwa na tumbo kubwa lisiloendana na mwili wao. Wengine wanatapika damu au kupata choo cheusi kutokana na ini kushindwa kufanya kazi zake vizuri na kuathiri mzunguko wa damu," anasema.

Anasema wagonjwa wengine hufikia hatua ya kupoteza fahamu kutokana na ini kushindwa kuondoa sumu mwilini.

Kwa mujibu wa Dk Pazi, hatua ya mwisho ni pale ambapo ndani ya ini huanza kutokea vinundu vinavyoweza kubadilika na kuwa saratani ya ini.

Anasema mchakato huo unaweza kuchukua miaka 10 hadi 20 kwa watu wazima walioambukizwa baadaye maishani, lakini kwa watoto walioambukizwa kutoka kwa mama wakati wa kuzaliwa, madhara yanaweza kutokea mapema zaidi.

"Mtoto aliyezaliwa na virusi vya homa ya ini B anaweza kupata madhara makubwa hata akiwa na umri wa miaka mitano hadi 10 kwa sababu mwili wake bado hauna uwezo mkubwa wa kupambana na virusi hivyo," anasema.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dk Diwani Msemo, anasema chanjo ya homa ya ini aina ya B ni moja ya silaha muhimu katika kupunguza wagonjwa wa saratani ya ini nchini, akisisitiza wananchi kujenga utamaduni wa kupima afya zao na kuchanja mapema.

Anasema kwa sasa udhibiti wa virusi vya hepatitis B na C umepewa kipaumbele katika mkakati wa kudhibiti saratani, kwa kuwa maambukizi hayo ndiyo chanzo kikuu cha saratani ya ini.

"Ukichanja watu dhidi ya homa ya ini, unakuwa pia umewazuia kupata sehemu kubwa ya saratani ya ini inayosababishwa na virusi. Wataobaki ni wachache wanaopata saratani kutokana na sababu nyingine, kama matumizi makubwa ya pombe," anasema.