Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanasayansi wabaini mbu hatari, wataja mbinu za kumuangamiza

Muktasari:

  • Ni aina mpya ya mbu hatari 'Pwani molecular form' wanaopatikana katika ukanda pwani ya Tanzania na Kenya, wanaostahimili sumu zote za mbu.

Dar es Salaam. Wanasayansi wamegundua aina mpya ya mbu katika pwani ya Kenya na Tanzania, yenye uwezo mkubwa wa kustahimili dawa za kuua wadudu, huku wataalamu wakishauri mbinu za kumuangamiza.

Aina hiyo mpya ya mbu iliyopewa jina la muda la ‘Pwani molecular form’, imegunduliwa na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Glasgow, Taasisi ya Wellcome Sanger na Taasisi ya Afya ya Ifakara iliyopo Jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Kiongozi Mkuu wa utafiti huo, Sophia Mwinyi kutoka Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI) na Chuo Kikuu cha Glasgow, matokeo mapya yanaonyesha kuwepo kwa mbu mwenye utofauti mkubwa wa kijeni,  ambaye anaweza kuwa na athari katika ufuatiliaji wa mbu waenezao malaria.

Kiongozi Mkuu wa utafiti huo kutoka Taasisi ya Afya Ifakara, IHI na Chuo Kikuu cha Glasgow, Sophia Mwinyi

Utafiti wao ulichapishwa wiki iliyopita katika jarida maarufu la kisayansi duniani la Molecular Ecology, unawaamsha baadhi ya Watanzania waliotoa shuhuda namna ambavyo dawa za mbu hazisaidii kuwaangamiza hasa kipindi hiki cha masika.

Mkazi wa Michenzani, Unguja visiwani Zanzibar Ilham Ijumaa, amesema wanapambana na mbu wang'atao ambao wanaangamia kwa shida licha ya kubadili dawa za mbu.

"Hizi mvua za sasa hivi, unapuliza dawa mbu hawasikii. Nimebadilisha aina tatu za dawa wanapotea baada ya muda wanarudi wanang'ata," amesema Ilham.

"Nimekuwa nikipuliza dawa za mbu ndani, mbu anapotea baada ya dawa kuisha unashangaa wanarudi na wakikung'ata wanauma haswa, wanakuwa wakali kuliko mwanzo," amesema mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam, Amina Ally.

Hata hivyo, wanasayansi hao wanasema kuwa aina hiyo mpya ya mbu inaonekana kuwa sugu kwa dawa kwa njia ya kipekee ambayo haijawahi kutambuliwa hapo awali katika pwani ya Kenya na Tanzania.

Inahusishwa na kundi la Anopheles gambiae, ambalo lina baadhi ya mbu hatari zaidi wanaoeneza malaria duniani.

Wanasema aina hii ya mbu  inaleta changamoto mpya hasa ikizingatiwa kuwa dawa za kuua wadudu ndizo msingi wa kudhibiti mbu waenezao magonjwa kama malaria.

Wanaongeza kuwa aina hii mpya ya mbu inaonekana kuwepo tu katika maeneo ya pwani ya nchi hizo mbili jirani, na ina uwezo wa kuongeza maambukizi ya malaria, hivyo kuongeza mzigo wa ugonjwa huo katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa utafiti huo, aina ya ‘Pwani molecular form’ ina sifa za kipekee za kustahimili dawa na tofauti na mbu wengine wa malaria wa ukanda huo, haina alama za kawaida za vinasaba vinavyohusiana na usugu.


Walivyogundulika

Kwa mujibu wa Mwinyi, walitumia teknolojia ya kisasa ya upangaji wa vinasaba vya malaria.

Upangaji wa vinasaba (genetic sequencing), hasa wa aina ya whole-genome sequencing (WGS), ni mchakato wa kubaini mpangilio kamili wa DNA ya vimelea vya malaria au mbu wanaobeba vimelea hivyo.

Teknolojia hii huwasaidia watafiti kuelewa maumbile ya kijeni ya vimelea, ikiwemo mabadiliko ya vinasaba, jambo linalosaidia katika utafiti wa mbinu za kuambukiza, usugu wa dawa, pamoja na kutengeneza tiba na chanjo mpya.

Mtafiti aliyeshiriki kutoka IHI, Dk Frederick Okumu

WGS huwapa watafiti taswira kamili ya jenomu ya vimelea, hivyo kutambua vinasaba vinavyohusika katika hatua mbalimbali za maisha ya vimelea, kama vile uwezo wake wa kuambukiza binadamu na kustahimili dawa za malaria.

WGS pia husaidia kufuatilia jinsi vimelea vya malaria vinavyobadilika na kujibadilisha kutokana na mabadiliko ya mazingira kama vile ya tabianchi na matumizi ya dawa.

Utafiti pia umeonyesha tofauti za kijiografia katika makundi ya Anopheles gambiae s.s. mbu kutoka Muleba, kaskazini-magharibi, walionyesha usugu zaidi dhidi ya pyrethroid kuliko wa kutoka Muheza, Kaskazini-Mashariki, ikionyesha kuwepo kwa makundi ya mbu yaliyotengwa kijiografia.

Kwa upande mwingine, Anopheles arabiensis hakuonyesha tofauti za kikanda, ikimaanisha kuwa kuna mtiririko mkubwa wa jeni kati ya maeneo.


Hatua za kuchukua

Kwa mujibu wa Mwinyi ugunduzi huu unaonyesha umuhimu wa takwimu za kijeni katika kudhibiti malaria. Kuelewa tofauti hizi kunaweza kusaidia kuandaa mikakati mahususi, hivyo kuboresha juhudi za kupambana na malaria Afrika Mashariki.

“Ugunduzi wa aina ya kijeni ya pwani umeonyesha mapungufu katika uelewa wetu wa utofauti wa mbu katika maeneo yenye malaria. Tabia yake ya kipekee dhidi ya viuatilifu na usambazaji wa kijiografia uliodhibitiwa, unaonyesha kuwa mbu huyu huenda anachangia katika kuendeleza maambukizi ya malaria wakati wa msimu wa kiangazi.

"Wakati aina nyingine za mbu huwa hazipo sana. Hii pia inaweza kueleza ni kwa nini kunaendelea kuwepo kwa wagonjwa wa malaria licha ya matumizi ya neti za mbu kwa wingi katika maeneo haya,” anasema Mwinyi.

Anasema ingawa athari za ugunduzi huu bado hazijaeleweka kikamilifu, matokeo haya yanaonyesha kuwa mikakati ya sasa ya kudhibiti mbu huenda haitafanikiwa kwa ufanisi dhidi ya aina hii mpya ya mbu wa Pwani.

Mtafiti mwenza kutoka IHI, Dk Fredros Okumu anasema; "Kwa kutumia maarifa ya kijeni, tunaweza kuwahi hatua mbele katika vita dhidi ya malaria. Kuelewa DNA ya makundi ya mbu kunawasaidia wanasayansi na maofisa wa afya ya umma, kuandaa mikakati bora ya kuzuia ueneaji wa ugonjwa.”

Mtafiti mwingine Alistair Miles anasema; “Uchambuzi wa kijeni umebaini kundi jipya fiche la mbu wa malaria lenye tabia tofauti ya usugu dhidi ya viuatilifu katika pwani ya Afrika Mashariki.

"Ugunduzi huu unahitaji uchunguzi wa haraka wa kientomolojia na wa ki-epidemiolojia ili kubaini tabia, ikolojia, na uwezo wa kueneza ugonjwa wa aina hii ya pwani.”

Jitihada za kuangamiza mbu nchini

Mtafiti Kiongozi kutoka Taasisi ya Utafiti wa magonjwa ya binadamu - NIMR, Kituo cha Amani, Muheza Tanga, Dk William Kisinza anasema hatua iliyopo ni kuhakikisha nchi zinazuia maambukizi ya malaria kwa ujumla na kuzuia hao mbu kueneza ugonjwa huo.

Anasema aina za kuzuia mbu zinajulikana, kama zilivyoainishwa na wataalamu wa afya na miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) inazojulikana ikiwemo kutumia kwa usahihi vyandarua vilivyowekwa dawa hasa nyakati za usiku.

Dk Kisinza anasema kuna matumizi ya kupulizia ukoko ndani ya nyumba ambayo pia ni njia sahihi ya kujikinga na malaria.

"Njia nyingine ambayo hasa Serikali ya Tanzania na nchi zingine, kuna tafiti zimeonyesha viuadudu ni mbinu sahihi zaidi. Viuatilifu sisi tuna kiwanda Kibaha, haijalishi ni mbu wa aina gani inapuliziwa kwenye madimbwi inaua aina yoyote ya mbu.

"Viuadudu vinaua kabla mbu hawajawa pevu hiyo maana yake wanaua lavi, hayo ndiyo matumizi sahihi."

Dk Kisinza anasema zaidi ni ufuatiliaji wa mabadiliko ya mbu hii ni ya muhimu sana, "Kwa bahati nzuri kwa Tanzania tuna mpango huu ambao unaongozwa na Wizara ya Afya pia kuna taasisi nyingi ikiwemo NIMR na zingine za utafiti ikiwemo Ifakara na KCMC."