Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vitanda vitano vyatolewa kusaidia tiba ya saratani Bugando

Mkuu wa taasisi za Serikali na binafsi benki ya NMB, William Makoresho (kulia) akimkabidhi kitanda maalum kwa ajili ya wagonjwa wa Saratani, Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Hospitali ya Bugando, Padre George Nzungu (kushoto). Picha na Damian Masyenene

Muktasari:

  • Takwimu zinaonyesha tangu kuanzishwa kwa matibabu ya saratani Bugando mwaka 2009, wagonjwa 140,000 wamebainika na kutibiwa, huku wagonjwa 70,000 wakiendelea kufuatiliwa kwa matibabu zaidi katika klinini zao.

Mwanza. Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando imepatiwa msaada wa vitanda vitano maalumu kwa ajili ya matibabu ya wagonjwa wa saratani.

Vitanda hivyo vyenye thamani ya Sh64 milioni vimetolewa siku chache tangu Hospitali ya Bugando itoe taarifa ya kuwepo ongezeko la wagonjwa wa saratani katika kanda hiyo.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa vitanda hivyo leo Jumanne, Juni 24, 2025 Kaimu Mkuu wa Idara ya Saratani Bugando, Dk Heronima Kashaigili amesema kwa mwaka Bugando inaona wastani wa wagonjwa wapya 2,000 (watu wazima) na watoto 350 baada ya huduma kuimarika.

Ambapo, kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya matibabu kwa siku wanaona wagonjwa 350, huku kwa mwezi wakiona wagonjwa 1,500 kwenye kliniki ya hospitali hiyo.

Takwimu hizo zinaonyesha tangu kuanzishwa kwa matibabu ya saratani Bugando mwaka 2009, wagonjwa 140,000 wamebainika na kutibiwa, huku wagonjwa 70,000 wakiendelea kufuatiliwa kwa matibabu zaidi katika klinini zao.

“Tulianza na watu wachache chini ya 900 (watu wazima) na watoto 350 kwa mwaka, lakini kwa sasa huduma zimekua hususan matibabu ya mionzi tiba na watoto. Mpango mkakati wa idara ni kuwa na wodi ya kutibu wagonjwa wa saratani ya damu na tumeshapeleka wataalamu watatu shuleni,” amesema Dk Kashaigili.

Kutokana na idadi hiyo ya uwepo wa wahitaji wa matibabu ya saratani, Dk Kashaigili amesema idara ina upungufu wa wataalam mbalimbali 50, huku akiwaomba wadau wengine kuendelea kusaidia kuboresha miundombinu ikiwemo vifaa tiba, rasilimali fedha na kuongeza uelewa kwa wananchi.

Akizungumza baada ya kukabidhi vifaa hivyo, Mkuu wa Taasisi za Serikali na Binafsi Benki ya NMB, William Makoresho amesema kilichowasukuma kufanya hivyo ni baada ya kuguswa na matatizo yaliyopo kwenye jamii kwani wanaamini jamii yenye afya ndiyo hutoa wateja wa uhakika.

‎”Tunatumia zaidi ya asilimia moja ya mapato yetu kurudisha kwa jamii hususan sekta ya afya ambapo tunatoa mashuka, vitanda, kujenga majengo ikiwemo wodi na kutoa vifaa tiba, tunaamini msaada huu itakuwa na mchango mkubwa katika kusaidia wagonjwa wenye uhitaji hapa Bugando,” amesema Makoresho.

Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Dk Alicia Masenga amesema pamoja na misaada wanayopata kwa wadau na Serikali kupitia Wizara ya Afya kuwezesha matibabu lakini uongozi unafanya juhudi binafsi kuhakikisha wagonjwa wanapata matibabu stahiki.

‎”Tuna wagonjwa wengi ambao wana changamoto za saratani na gharama za matibabu yake ni kubwa na moja ya juhudi tunazofanya ni kuanzisha mbio za hisani kukusanya Sh1 bilioni kusaidia matibabu haya, tukipata hizi fedha zitarejesha tabasamu kwa wagonjwa wetu ambao wanakuwa wamekata tamaa,” amesema Dk Masenga.

Mwakilishi wa Bodi ya Wadhamini Hospitali ya Bugando, Padre George Nzungu amesema hospitali hiyo inahudumia Kanda ya Ziwa yenye wakazi milioni 22 ambapo msaada uliotolewa na NMB utasaidia Watanzania wengi ambao kwa kiasi kikubwa wanapata changamoto, huku akiomba wadau wengine kujitokeza kusaidia kutatua changamoto zilizopo.

Mkazi wa jijini Mwanza anayeuguza mgonjwa mwenye saratani ya koo hospitalini hapo, Annastazia Alfred  amesema; “Changamoto tunazokutana nazo vifaa ni vichache foleni inakuwa kubwa tunatoka usiku, tunawashukuru NMB kwa msaada huu wa vitanda itasaidia kupunguza baadhi ya changamoto kwa wagonjwa,” amesema.