Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

1,000 wafanyiwa upasuaji wa mdomo sungura na makovu

Daktari wa upasuaji wa kurekebisha sura, Dk Dane Barrett (mwenye mavazi meupe) kutoka Chuo Kikuu cha Duke cha Marekani akiongoza jopo la madaktari wa upasuaji sanifu na rekebishi wakijiandaa kufanya upasuaji kwa mmoja wa wagonjwa wenye changamoto za sura na kichwa, katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando. Upasuaji huo umefanyika Juni 5, 2025 hospitali hapo ikiwa ni sehemu ya wagonjwa 20 waliofanyiwa upasuaji huo ndani ya wiki moja. Picha na Damian Masyenene

Muktasari:

  • Mbali na upasuaji huo, hospitali hiyo kupitia kambi ya matibabu ya siku tano iliyoanza Juni 2 - 6, 2025.

Mwanza. Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando imefanya upasuaji wa kurekebisha hitilafu za kimaumbile ikiwemo mdomo wazi, mdomo sungura na makovu unoni kwa wagonjwa takriban 1,000 katika kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2021.

Mbali na upasuaji huo, hospitali hiyo kupitia kambi ya matibabu ya siku tano iliyoanza Juni 2-6, 2025 imefanya upasuaji kwa wagonjwa 20 kati ya 30 wenye changamoto za majeraha ya kuungua, ajali na asili (kuzaliwa).

Wagonjwa hao ni wale waliopatikana katika kliniki ya matibabu iliyofanyika hospitalini hapo kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Duke na Shirika la Healing Children kutoka Marekani.

Kaimu Mkuu wa Idara ya upasuaji sanifu na upasuaji rekebishi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Dk Biswalo Yango amesema ingawa tafiti za mdomo sungura bado zinaendelea, lakini hadi sasa inaonyesha ugonjwa huo husababishwa kwa njia ya kurithi kutoka kwa wazazi (vinasaba), na mazingira mfano matumizi ya dawa zinazomuathiri mama.

“Watu tunaowafanyia upasuaji kuna wanaopata majeraha ya kuungua na ajali na kuleta hitilafu kwenye mwili unakuta sehemu moja haifanani na kama ilivyokuwa awali, kwa hiyo tunamrudisha katika hali  aliyokuwa nayo kabla,” amesema Dk Yango

Ameongeza kuwa, “wengine wanakutwa na majeraha ya kuungua hawawezi kufunga macho vizuri ama mdomo haufungi vizuri au kuna sehemu viungo vimeharibika baada ya kuungua au kupata ajali pia tunatibu.”

Yango ambaye ni daktari bingwa bobezi wa upasuaji sanifu na rekebishi, amesema kupitia kliniki tatu zinazofanywa kila wiki kwenye idara yake hupokea wagonjwa 100 wenye changamoto zinazohitaji upasuaji rekebishi,

Idadi hiyo ni sawa na  wagonjwa 350 hadi 400 kila mwezi, huku akiwahakikishia wananchi kuwa huduma za upasuaji ni endelevu na zinafanyika kila siku hospitalini hapo.

“Tunatarajia wageni wetu watarudi tena Julai, 2025 kama kuna wagonjwa ambao walikosa huduma kwa awamu hii wanaweza wakaja hospitali na tutawaelekeza utaratibu ili mwezi wa saba wapate huduma hii,” amesema Dk Yango

Mkufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Duke cha Marekani, Profesa Dane Barrett amesema wamekuwa wakishirikiana na Hospitali ya Bugando kwa miaka mitatu katika kuwajengea uwezo wataalamu wake kufanya upasuaji huo na kusaidia vifaa na dawa.

“Changamoto tunayoiona kwa wagonjwa hapa tofauti na Marekani ni kwamba wengi wanafika hospitalini tatizo likiwa limeshakuwa kubwa na kufanya matibabu yake kuwa na usumbufu, hivyo tunaamini ushirikiano huu utaendelea ili kuwaongezea nguvu Bugando kupitia elimu, mafunzo na kujengeana uwezo,” amesema DK Barrett

Naye, Grace Julius mama wa mtoto wa miaka minne aliyefanyiwa upasuaji wa mdomo sungura, amesema mwanzo haikuwa rahisi kukubali tatizo la mwanaye baada ya kuzaliwa akiwa amechanika mdomo wa chini na ndani, hadi pale alipoanza matibabu Bugando.
Grace amewashauri wazazi wenye watoto walio na changamoto hiyo kutowaficha au kuwatenga, bali wawapeleke kwenye vituo vya afya au Bugando wapate matibabu yanayohitajika mapema.