Vikombe vya hedhi njia mbadala ya kumstiri mwanamke

Dar es Salaam. “Nilikuwa nikitumia vikombe vya hedhi ninapokuwa katika siku zangu, lakini ilinilizimu kuacha baada ya kuwa napata muwasho mara kwa mara, nilishauriwa na daktari kubadili njia ninayotumia kujisitiri katika siku zangu.”

Ndivyo alivyosimulia mwanamke huyu uzoefu wake katika matumizi ya vikombe hivyo ambavyo kitaalamu huitwa ‘menstrual cup’, vinavyotajwa kuwepo tangu miaka ya 1930.

Vikiwa katika muundo wa plastiki laini, inakuwa kama mbadala wa sodo kwa mwanamke, badala ya kutumia sodo katika siku zake za hedhi, huweza kupachika kikombe hicho ili kukinga damu anayoipata.

Kwa mujibu wa jarida la Healthline, vikombe hivyo vipo vya aina mbili na kwa mwanamke aliye chini ya miaka 30 hushauriwa kutumia size ndogo na walio na umri zaidi ya hapo hushauriwa kutumia ‘size’ kubwa.

Tofauti na sodo za kawaida zinazotumiwa na wanawake, kikombe hiki huwa na uwezo wa kukaa kati ya saa nane hadi 12, huku ikitajwa kuwa na faida kiuchumi kwa sababu mtu huweza kuirudia katika matumizi.

Lakini kabla ya kutumia, inashauriwa mhusika kuwasiliana na daktari ili waweze kushauriana baadhi ya vitu, ikiwemo ni kikombe cha ukubwa gani anaweza kutumia ili kufanikisha azma yake. Hiyo itatokana na vipimo ambavyo atafanyiwa na daktari kujua ukubwa wa maumbile yake.

Tovuti ya WebMd nayo inaeleza kuwa kikombe cha kwanza cha hedhi nchini Marekani kilitengenezwa mwaka 1987 na tangu hapo kumekuwapo na bidhaa tofauti zinazotengenezwa.


Namna ya kutumia

Tofauti na sodo nyingine ambazo huwekwa au kushikiliwa na nguo za ndani, kwa kikombe hiki cha hedhi hushikiliwa na maungo ya binadamu. Lakini ili mtu aweze kukitumia lazima awe katika mkao anaoweza kukipachika na kuhakikisha kimekaa vizuri, ili kuweza kumfanya awe huru.

Ili kufanikisha hilo, mtumiaji anatakiwa kukaa katika mfumo wa kuchuchumaa, ili kuruhusu kikombe hicho kilicho na uwezo wa kukunjika kirahisi kuingia na aweze kukiweka vizuri. Pia wakati wa kutoa, mtumiaji atatakiwa kuwa katika mtindo wa kuchuchumaa (squat), ili kukisukuma kwa nguvu au kutumia vidole vyake kukivuta.

Angalizo linatolewa kwa watumiaji wa vikombe hovyo kuwa ni vema kuviosha vizuri kabla ya kuvitumia tena, kuvifuta na kuacha vikauke huku wakiona kuwa kwa vile ambavyo vinapaswa kutupwa baada ya kutumika basi visirudiwe, kwani kukiuka inaweza kumuweka mtu katika hatari ya kupata maambukizi mbalimbali, ikiwemo miwasho kwa mujibu wa tovuti ya health online.

Katika matumizi ya vikombe hivi kama chanzo chetu cha habari kilivyoeleza ni pamoja na miwasho sehemu za siri ambayo huwakosesha watumiaji raha.

Healthline inaeleza miwasho hiyo huweza kusababishwa ikiwa kikombe hakikuoshwa au kutunzwa vizuri baada ya matumizi.

Tovuti hiyo pia inaeleza kuwa miwasho kwa baadhi ya watu huweza kusababishwa na mzio kutokana na malighafi zilizotumika katika utengenezaji.


Vinapatikana nchini

Vikombe hivi kwa sasa upatikanaji wake umekuwa si wa kutafuta na tochi, kwani mitandaoni vinauzwa na mteja huweza kuelekezwa namna ya kuvitumia.

Mmoja wa wauzaji wa vikombe hivyo aliliambia Mwananchi kuwa kikombe kimoja huuzwa kwa Sh10,000 na ili mtu awe huru anatakiwa kuwa na walau vikombe vitatu.

“Tukikuuzia tunakuuzia na sterilizer yake kwa ajili ya kusafishia, ni nzuri na kama unasumbuliwa na miwasho ukitumia sodo za kawaida hii itakufanya uwe huru,” anasema. Lakini si wote wanaotumia vikombe hovyo hupata madhara, kwani Luciana James anaelezea kuwa hiyo imekuwa njia yake ya muda mrefu.

“Naogopa sana sodo za kawaida, njia hii ya vikombe nilijifunza kama mwaka mmoja sasa, niko huru, gharama unaipata wakati wa kuvinunua lakini baada ya hapo utasahau kila kitu.

“Kama ni mtunzaji mzuri unaweza kukaa na vikombe hivi hata mwaka mmoja, ila ukizingatia usafi wake,” anasema.

Anasema mbali na watu wanavyofikiri, mtu akipachika kikombe hicho huweza kufanya shughuli zote, ikiwemo kurukaruka, kukimbia, push ups na hata kutembea kwa muda mrefu. “Haina tofauti na sodo, ni mawazo tu ya watu,” anasema muuzaji huyo.

Wakati njia hii ikiwa inaonekana kama ngeni masikioni kwa watu, Dk Ramadhani Senga anaeleza anafahamu uwepo wa vikombe hivyo, huku akieleza kuwa ni vema kabla ya mtu kutumia aonane na daktari.

“Kwa sababu vikombe hivi vina ukubwa tofauti ni azima mtu apate kile kinachoendana na ukubwa wa sehemu zake, ili awe huru,” anasema Dk Senga.

Anasema mara nyingi mtu anapotumia kitu kipya kwa mara ya kwanza huweza kumpa shida, lakini kadiri anavyozoea hali hiyo huimarika.

Kauli yake inaungwa mkono na Dk Samwel Shita, anayesema bado hajapata kesi yoyote kuhusu vikombe hivyo, huku akieleza miwasho huwa ni kawaida kwa baadhi ya taulo za kike na kwamba kitu cha muhimu ambacho watumiaji wa vikombe hivyo wanapaswa kuzingatia ni kutoa taarifa kwa wataalamu wa afya, ili kujua kuna visa vingapi vimetokea.