Utafiti: Wanawake walio kwenye ndoa waongoza kwa utoaji mimba

Muktasari:
- Kwa mujibu wa utafiti unaojulikana kama “Incidence of Induced Abortions and the Severity of Abortion-related Complications in Kenya”, takribani wanawake 792,694 walitoa mimba mwaka 2023.
Kenya. Kumekuwa na dhana miongoni mwa wanajamii kuwa mabinti wadogo au ambao hawajaingia kwenye ndoa hujihusisha na matukio ya utoaji wa mimba zaidi kuliko wale walioko kwenye ndoa.
Hata hivyo, hiyo imekuwa tofauti baada ya utafiti mpya uliofanyika nchini Kenya na Taasisi ya APHRC, NADC na Guttmacher kuonyesha kuwa wanawake walioko kwenye ndoa, wenye elimu na ambao wamewahi kupata watoto, wanaongoza kwa kutoa mimba kwa hiari.
Kwa mujibu wa utafiti huo uliopewa jina la “Incidence of Induced Abortions and the Severity of Abortion-related Complications in Kenya”, umeonyesha kuwa takribani wanawake 792,694 walitoa mimba mwaka 2023.
Idadi hiyo inawakilisha kiwango cha utoaji mimba wa hiari cha asilimia 57.3 kwa kila wanawake 1,000 wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 49.
Katika utafiti huo wanawake takribani 2022 walihojiwa na kati yao asilimia 58 wameolewa huku asilimia 32 wakiwa tayari na watoto kati ya wawili hadi watatu.
Utafiti huo ulibaini wanawake waliopokea huduma za baada ya utoaji mimba walikuwa kati ya umri wa miaka 25-34 asilimia 78.6 wameolewa au wanaishi na wapenzi wao.
“Wanawake waliofiwa na waume au walioachika walikuwa asilimia 22 ya waliotoa mimba, huku wale ambao hawajawahi kuwa katika uhusiano wowote wakiwa asilimia 19,” amesema.
“Wanawake wasiokuwa na watoto waliotoa mimba walikuwa 597, huku 562 wakiwa na mtoto mmoja,”unaeleza utafiti huo.
Kwa mujibu wa uchambuzi wa utafiti huo uliochapishwa katika tovuti ya Daily Nation, matukio hayo yalijitokeza zaidi katika maeneo ya Nairobi na Kanda ya Kati kwa 78.3 ikifuatiwa na Nyanza na Magharibi (69.4) na Mashariki (55.6).
Pwani na Kaskazini Mashariki zilikuwa na kiwango cha chini zaidi cha utoaji mimba cha 38.7 kwa kila wanawake 1,000 wenye umri wa kuzaa.
Kwa mujibu wa tovuti ya Taifa Leo, takriban asilimia 89.4 walitumia mbinu moja tu huku dawa zikiongoza kwa asilimia 61.8. Mbinu za jadi zilitumiwa na asilimia 27 huku asilimia 12.2 wakitumia mbinu nyinginezo.
Utafiti unaeleza kuwa ongezeko hilo linasababishwa hasa na ongezeko la mimba zisizotarajiwa ambazo zilifikia jumla ya milioni 1.4 mwaka 2023.
Utafiti unaonyesha kuwa zaidi ya nusu ya mimba zote zisizotarajiwa huishia kutolewa kwa hiari.
Utafiti pia umeonyesha kuwa idadi ya utoaji mimba kwa kila vizazi hai 100 ilipanda kutoka 30 hadi 48 kati ya mwaka 2012 na 2023. Kupanda huko kunahusishwa na upatikanaji wa dawa za kutoa mimba kwa urahisi zaidi katika miaka 15 iliyopita.
Hali ilivyo Tanzania
Licha ya kukosekana kwa takwimu za hivi karibuni, takwimu za zamani zinazotokana na utafiti uliofanywa na Guttmacher zinaonyesha kwamba utoaji mimba pia unafanyika Tanzania kwa kiwango kikubwa.
Kwa mujibu wa Guttmacher, inakadiriwa kuwa mimba 405,000 zilitolewa ndani ya mwaka 2013 nchini Tanzania.
Idadi hiyo ni kiwango cha utoaji wa mimba 36 kwa kila wanawake 1,000 wenye umri kati ya miaka 15-49 na uwiano wa utoaji mimba 21 kwa kila watoto 100 wanaozaliwa wakiwa hai.
Januari 31, 2025, Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel, akijibu swali la mbunge wa viti maalumu, Fatma Tawfiq aliuliza swali akitaka kujua idadi ya watoto wa kike na wanawake walioathirika na utoaji mimba usio salama nchini, alisema kwa mwaka 2024 idadi ya wanawake na wasichana waliopata changamoto za kuharibikiwa na mimba na kupata huduma katika vituo vya afya na kuruhusiwa kurudi nyumbani walikuwa 181,071.
Dk Mollel alitaja wanawake na wasichana 32,512 ni ambao walipatiwa huduma wakiwa wamelazwa wodini kwa mwaka 2024. Lakini katika kipindi cha mwaka 2022 hadi 2024 wanawake 92 walipoteza maisha kutokana na changamoto mbalimbali zinasababishwa na kuharibika kwa mimba.
Wakati huohuo, takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha wanawake 181,071 walipata huduma ya kusafishwa na wengine 32,512 walilazwa baada ya mimba kuharibika mwaka 2024.
Hata hivyo, Ripoti ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria (TDHS) iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu NBS mwaka 2023 ilionesha Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa asilimia 23 ya mimba kuharibika.
Imeandikwa na Mariam Mbwana kwa msaada wa mashirika ya habari.