Unajua kwa nini unaweza kuugua maradhi ya moyo?

Muktasari:
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), maradhi yasiyoambukiza kama yalivyo maradhi ya moyo, kila mwaka huua watu milioni 38 duniani na vifo vingi kati ya hivyo, hutokana na maradhi ya moyo.
Ugonjwa wa moyo unajumuisha matatizo ambayo yanaathiri muundo na kazi za moyo na ni moja ya maradhi yasiyoambukiza.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), maradhi yasiyoambukiza kama yalivyo maradhi ya moyo, kila mwaka huua watu milioni 38 duniani na vifo vingi kati ya hivyo, hutokana na maradhi ya moyo.
Ugonjwa huu mara nyingi huhusishwa na kujibana au kukazika kwa mishipa ya damu au mkusanyiko wa taka katika kuta za mishipa ya damu ambayo husababisha kupungua kipenyo cha mishipa ya damu na hivyo kuzuia mzunguko ulio huru wa damu na hatimaye kukupa hatari ya kupata shambulio la moyo, kupooza kwa maana ya kiharusi.
Ugonjwa wa moyo ni moja ya maradhi makuu manne yaliyopata kujadiliwa katika mjadala wa kwanza wa ‘Mwananchi Jukwaa la Fikra’ kuhusu maradhi yasiyoambukiza.
Wadau walielezea nini suluhisho la kupambana na ugonjwa huo.
Mjadala huo uliandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communication (MCL) kwa kushirikiana na kituo cha Televisheni cha ITV na Radio One.
Mwananchi limezungumza na wadau mbalimbali ambao wametoa mapendekezo yao ya nini kifanyike ili kupambana na maradhi haya.
Mkurugenzi wa Kliniki ya maradhi ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Adelila Kimambo anasema, changamoto kubwa ni upatikanaji wa afya bora kwa wote. “Hakuna uwiano sawa wa tiba kwenye vipengere hivi vyote ambavyo ni muhimu vya huduma hizi ambazo ni elimu ya afya na upatikanaji wa huduma ya matokeo ya matibabu. Katika utafiti tunapata changamoto kwa kuwa pamoja na kwamba, tunapata wagonjwa wengi wanaofika kutibiwa JKCI hatujaweza kuwafikia wote,” anasema.
Anasema inakadiriwa ulimwenguni kote kati ya watoto watakaozaliwa 1,000, wanane watakuwa na matundu kwenye moyo na matatizo mengine yafananayo na hayo.
“Watoto hawa bado wanaleta mzigo mkubwa kwa sababu wote watahitaji upasuaji wa moyo na ukija kwenye hii afya bora kwa wote, bado tunapata changamoto kwa kuwa wengi hawajafikiwa hata na ile huduma ya toto ‘Afya Card’.”
Dk Kimambo anasema licha ya kwamba inaleta mzigo mkubwa kwenye bajeti ya wizara ya afya, wao wanaona familia pia zinahusika katika kuchangia matibabu kwa ndugu zao kwa kiasi kikubwa, hivyo kuleta umasikini katika ngazi ya familia kutokana na kuwauguza wagonjwa hao kwa muda mrefu.
Anaitaja changamoto nyingine ni upande wa dawa. Anasema mtu akishapata ugonjwa wa shinikizo la damu anahitajika kutumia dawa kwa maisha yake yote.
Dk Kimambo anasema bado kuna safari ndefu ya kupambana na maradhi hayo kwasababu mitaani hivi sasa vimesambaa vyakula mbadala vinavyotumiwa na maelfu ya watu.
“Sisi ambao tunatoa tiba kwa wagonjwa wa shinikizo la damu na kisukari ukienda mtaani utakuta vinachukua, nafasi kubwa na wakati mwingine vikionekana ni tiba sahihi ya kupunguza presha na kisukari, nafikiri mwongozo unahitajika.
“Vingine vinaonekana ndiyo tiba sahihi ya kupunguza presha au kisukari, tungeweka mwongozo kwa wanaovisajili ili kusaidia kuvipunguza na tungeweza kuvidhibiti, vimekuwa vingi mno na vinasababisha wagonjwa wengi kuacha dawa na kuhamia kwenye vidonge hivyo mwishowe, tunapata tabu kubwa ya kuwatibu hapo baadaye.”
Anasema eneo la mama lishe linapaswa kuangaliwa kwani ni vema waelimishwe waongeze matunda kwenye chakula.
“Ukienda kwao utaona wanga ni mwingi zaidi kuliko matunda, sehemu kubwa ya mama lishe ni chakula waongeze matunda zaidi kuliko wanga Watanzania wengi wanakula kwa mamalishe wakipata hiyo itasaidia kuboresha afya zetu,” anasema Dk Kimambo.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) Profesa Yunus Mgaya anasema kuna uhusiano kati ya magonjwa yasiyoambukiza na yale yanayoambukiza uhusiano unaoangaliwa kwa namna ambavyo serikali inapeleka rasilimali fedha.
Anasema magonjwa yanayoambukiza yanapata sehemu kubwa ya bajeti na nguvu kazi kuliko yasiyoambukiza. “Wakati huu vema tudandie katika mfumo huo kwani upo vizuri ili tuweze kutumia rasilimali zilezile tupunguze katika magonjwa yasiyoambukiza hilo tumeliangalia katika tafiti zetu na kuangalia namna ya kutekeleza hilo,” anasema.
Profesa Mgaya anasema wakiwa watafiti wanafahamu kuwa wana jukumu la kuongeza uelewa wa wananchi kwenye mzigo uliopo wa magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo magonjwa ya moyo.
“Kwa sababu kwenye tafiti zetu tunaibua taarifa mbalimbali zinaoingia kwenye sera, tuna uwezo wa kutoa mchango mkubwa wa kufahamisha wananchi zaidi ya tunavyofanya sasa kuhusu magonjwa haya,” anasema.
Mkurugenzi wa Magonjwa yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya, Dk Sara Maongezi anasema kwa sasa ni muhimu kwa sekta zingine kusaidia katika malengo mengine ili kufanikisha kupambana na magonjwa hayo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Ifakara Health Institute Honorati Masanja anasema, “Sisi Ifakara tunafanya tafiti nyingi zikiwemo za haya magonjwa yasiyoambukiza, tulifanya kwenye jamii na tukagundua Watanzania hawatumii matunda na hiyo ni moja ya vyakula vinavyoongeza afya na kuleta vitamini.”
Anasema kuna changamoto katika takwimu, “nadhani hatuna tafiti kwenye magonjwa kama ya moyo na yafananyo na haya ukiangalia machapisho yamiaka 10 iliyopita ni 620 pekee ikilinganishwa na magonjwa kama Malaria ambako kuna zaidi ya machapisho 5000 kwa Tanzania peke yake. “Tunahitaji kufanya tafiti ili kuweza kuibua hizo changamoto kwa mfano kama viashiria vya magonjwa haya, kuzichambua tafiti na kuwapelekea watu mambo ambayo yatasaidia kubadili mwelekeo.” Anasema Masanja.
Upatikanaji wa dawa
Meneja manunuzi kutoka Bohari ya Dawa MSD Sylvester Maige anapendekeza ili wizara iweze kupambana na magonjwa ya moyo, hasa kwenye kuzuia maambukizi iwekeze kwenye vifaa vya mazoezi.
Anasema upatikanaji wa dawa za kutibu maradhi hayo pamoja na yale mengine yasiyo ya kuambukiza, hali ya Tanzania ni mbaya hakuna kiwanda hata kimoja ambacho kinatengeneza dawa kwa magonjwa makuu yasiyoambukiza.
Anasema changamoto kubwa wanayokutana nayo fedha zote zinazotengwa kununua dawa hizo zinakwenda nje ya nchi.
Anasema kwa ajili ya kutibu magonjwa yasiyoambukizwa MSD imekuwa ikinunua aina ya dawa zaidi ya mia tatu, huku dawa zinazotibu NCDs zilizo ghali zaidi ni dawa za kutibu magonjwa ya saratani.
“Kwa kipindi cha kuanzia Julai Mosi 2017 mpaka Juni 20, 2018 tumenunua na kupokea dawa za magonjwa yasiyo kuambukiza zenye thamani ya takribani Sh22 billion sawa na Sh1.8 bilioni kwa mwezi,” anasema.
Sababu za maradhi ya moyo
Lakini kutozingatia kanuni za ulaji bora, ni moja ya mambo yanayoongeza uwezekano wa mtu kupata magonjwa ya moyo.
Hii ni pamoja na ulaji wa vyakula vyenye mafuta, sukari, chumvi na lehemu kwa wingi, huku ulaji wa mbogamboga na matunda ukiwa ni wa kiwango cha chini, hiyo huongeza uwezekano wa kupatwa na magonjwa ya moyo.
Uzito uliozidi au kuwa na unene uliopitiliza pamoja na kutofanya mazoezi ya mwili na viungo mara kwa mara, huchochea pia uwezekano wa magonjwa ya moyo.
Licha ya historia ya ugonjwa huo kwenye familia, umri unapozidi miaka 50 kuna uwezekano pia wa kupatwa na magonjwa haya, huku wanaume wakiwa kwenye hatari zaidi ya kupatwa na tatizo hili mapema zaidi ikilinganishwa na wanawake.
Tafiti mbalimbali zinaonyeshamagonjwa haya huanza kusumbua pindi aina fulani za mafuta na lehemu katika damu. Hali hiyo inapompata mtu, mishipa ndani ya moyo huweza kufungamana kwa mafuta.
Ongezeko la lehemu huongeza hatari ya kupata magonjwa ya moyo huku wingi wa lehemu unakadiriwa kusababisha vifo vya watu takriban milioni 2.6 duniani kila mwaka.
Kuwepo kwa sukari nyingi katika damu, husababisha ugonjwa wa Kisukari, ambao unamweka mtu katika hatari ya kupata ugonjwa wa moyo au kupooza mara mbili zaidi ya asiye na kisukari.
Shinikizo kubwa la damu, maana yake ni kwamba moyo unalazimika kusukuma damu kwa nguvu ili kutosheleza mahitaji ya mwili. Kuulazimisha moyo kufanya kazi kuliko kawaida yake, kunasababisha moyo kushindwa kufanya kazi (Heart Failure).
Uvutaji wa sigara au utumiaji wa tumbaku kwa kutafuna au kunusa (ugoro), husababisha pia sehemu ya ndani ya kuta za mishipa ya damu kuharibiwa, hivyo kuongeza hatari ya magonjwa ya moyo.
Kemikali zinazopatikana kwenye tumbaku, huweza kuharibu seli za damu. Uharibifu huo wa seli, huingilia muundo na utendaji mzuri wa mishipa ya damu. Aidha, kuharibika kwa mishipa ya damu, kunachochea mafuta kuganda kwenye mishipa ya damu.