Tujikumbushe kuhusu saratani ya kizazi-2
Wiki iliyopita nilieleza kwamba saratani ya shingo ya uzazi ni aina ya ugonjwa unaoongoza kuua wanawake wengi kuliko aina nyingine ya saratani.
Zaidi ya nusu ya wanawake wanaopimwa na kukutwa na saratani ya shingo ya kizazi wanakuwa kwenye umri wa kuanzia miaka 30 hadi 60.
Pia, huwapata waliopo kwenye umri wa wastani wa miaka 20 japo ni mara chache, lakini inakadiriwa takribani asilimia 20 ya wanaopatikana na aina hii ya saratani ni wanawake wenye kuanzia miaka 60 na kuendelea.
Hata hivyo, tukiachana na sababu ya jinsia, kuna vihatarishi vingine vya ungonjwa huu ambavyo baadhi vinasababishwa na mwanamke mwenyewe na vingine vinakuwa nje ya uwezo wake.
Baadhi ya sababu hatarishi zinazomuweka mwanamke hatarini kupata ugonjwa wa saratani wa shingo wa uzazi ni kama vile; uvutaji wa sigara na aina yeyote ya tumbaku kwa ujumla, maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU), maambukizi ya magonjwa mengine ya ngono na hasa yanayojirudia rudia, kuwa na uzito wa mwili uliopitiliza, hali duni za kimaisha zinazosababishwa na umaskini na sababu za kurithi zinazotokana na historia ya magonjwa ya saratani kwenye familia na vizazi vilivyopita.
Mwanamke wakati wote anashauriwa kuwa makini na dalili kuu za ugonjwa huu kwani kupitia hizo zitampa msukumo wa kuwahi hospitali kuwaona wahudumu wa afya na kupata vipimo ili kuiwahi saratani hii kwenye hatua za awali.
Dalili kuu za saratani ya shingo ya kizazi ambazo mwanamke hapaswi kuzifumbia macho ni pamoja na kutokwa na damu ukeni kusikoendana na ratiba ya mzunguko wake wa hedhi; kutokwa na damu ukeni wakati au baada ya tendo la ndoa, kutokwa na damu ukeni wakati wa kujisafisha, na hedhi zinazoendelea kwa mwanamke ambaye kiumri hawezi tena kushika mimba na kuzaa.
Dalili nyingine ni pamoja na maumivu chini ya kitovu ya mara kwa mara, kutokwa na ute na uchafu mwingine ambao unakuwa na rangi ya maziwa au njano na wakati mwingine unaambatana na harufu mbaya na maumivu wakati wa haja ndogo.
Mwandishi wa makala haya ni daktari kutoka Hospitali ya TMJ SUPER SPOECIALIZED POLYCLINIC.